Imetangazwa: Prince Harry Kamchumbia Meghan Markle

Mwana wa ukoo wa kifalme wa nchini Uingereza, Prince Harry(33), amepata mchumba. Yupo mbioni kuoa. Hayo yametangazwa mapema hii leo katika taarifa maalumu iliyotolewa na ukoo huo wa kifalme nchini Uingereza.

Prince Harry ambaye kiutaratibu ni mrithi namba tano wa kitu cha ufalme, anatarajiwa kumuoa rafiki yake wa kike wa muda sasa muigizaji wa filamu, Meghan Markle. Kama unafuatilia tamthilia ya Suits iliyosheheni masuala ya kisheria, utakuwa umeshamuona Meghan. Tamthilia ile hutengenezewa jijini Toronto,Canada. Kwa wakazi wa Canada, Meghan ni kama mtoto wao ingawa kiuraia ni Mmarekani.

/ AFP PHOTO / Daniel LEAL-OLIVAS (Photo credit should read DANIEL LEAL-OLIVAS/AFP/Getty Images)

Mimi sina kawaida ya kufuatilia koo za kifalme. Siamini kwenye familia fulani kuwa ya kifalme. Kwangu kila mtu ni mfalme au malikia. Lakini kinachoifanya habari hii kuwa ya kipekee ni kwamba kwanza Prince Harry ameamua kuchukua jiko nje ya Uingereza. Meghan ni raia wa Marekani.

Kingine kinachoifanya habari hii kuwa tofauti ni kwamba Meghan ni half-cast wa kizungu na mweusi. Mama yake ni Mmarekani mweusi na baba yake ni mzungu. Kwa maana hiyo atakuwa mtu mwenye damu nyeusi wa kwanza kuolewa au kuingia ndani ya familia ya kifalme ya Uingereza.

Wawili hao ambao mapema leo wamejitokeza mbele ya waandishi wa habari na mashabiki huku Meghan akiwa amevalia tayari pete ya uchumba, wameelezea kuwa wenye furaha kubwa kufikia hatua hii. Harusi yao inatarajiwa kufungwa mwakani 2018.

 

Copyright © Bongo Celebrity