Umewahi kusoma makala zake,vitabu vyake na pia kusikiliza muziki wake.Jina lake sio geni.Nimeshawahi kufanya naye mahojiano. Anaitwa Freddy Macha,mtanzania mwandishi,mwanamuziki mwenye makazi jijini London nchini Uingereza.
Mwezi wa Mei mwaka huu,Freddy aliitikia wito wa kurudi nyumbani Tanzania na kugawana na wengine ujuzi mbalimbali alionao katika masuala ya uandishi,fasihi, muziki, maisha ya ughaibuni, mazoezi,afya na chakula bora. Alifanya hivyo kupitia semina mbalimbali alizoziendesha pale British Council,Soma Cafe(Mikocheni), Shule ya Sekondari Mwandege na Nyumba ya Sanaa.
Semina alizozifanya Macha ziliandaliwa na Jarida jipya la Lucky-Ideas For Living.Freddy anatarajiwa kurudi tena Tanzania mwezi Septemba mwaka huu ili kuendesha semina zingine.Usikose

Freddy Macha akiongelea uandishi wa vitabu na makala.Hapa ilikuwa Nyumba ya Sanaa jijini Dar-es-salaam.

Freddy akimuelekeza mmoja miongoni mwa waliohudhuria semina jinsi ya kufanya mazoezi ya tumbo.
Leo ni siku ya ukimwi duniani.Ni mwaka wa ishirini sasa tangu maadhimisho ya siku hii yaanze hapo mwaka 1988.Ni siku ambayo dunia nzima inajumuika kukumbuka ndugu,jamaa na marafiki zetu wote walioathirika na hata kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huu hatari ambao mpaka hivi leo bado unaendelea kuwa tishio.
Lakini muhimu kabisa ni kwamba maadhimisho ya siku hii hutumika pia kutafakari mambo mbalimbali kuhusiana na ugonjwa huu.Ni siku ya kutizama kwa makini maendeleo ya tafiti mbalimbali za tiba kuhusiana na ugonjwa huu,hatua ambazo tumeshapiga katika mapambano ya kuutokomeza ugonjwa huu na mipango ya mbeleni katika vita hii.Zaidi ya watu milioni 33 duniani wanaishi na virusi vya ukimwi.Ni siku nzuri pia kudhamiria,wewe na mimi,kwamba tutaongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huu.
Takwimu mbalimbali za kitaalamu zinaonyesha kwamba maambukizi ya ukimwi yameanza kupungua ikilinganishwa na miaka kadhaa nyuma. Hili ni jambo la kujivunia ingawa halitakiwi kuachwa kuwa kama mafanikio ya mbalamwezi ambayo hupotea pindi tu jua linapoanza kuchomoza.Kazi kubwa bado ipo.Ukimwi bado upo,ni hatari na unaua.Sote tuna jukumu la kujilinda,kuwalinda tuwapendao na kuilinda dunia yetu.Dunia bila watu si dunia!Kama unampenda,utamlinda!

