
Majuzi shindano maarufu la Big Brother Africa limemalizika huku Afrika ikishuhudia ushindi,kwa mara ya pili mfulululizo,ukienda nchini Nigeria.Mshindi wa safari hii akiwa ni Uti Nwachukwu,ambaye amejizolea kitita cha dola za kimarekani laki mbili ($ 200,000)
Wakati tukimpongeza mshindi,yapo mambo kadhaa ambayo yamejitokeza hususani kupitia katika maoni ya wengi katika mitandao ya kijamii(Social Networks). Fikra tofauti tofauti zimekuwa zikitolewa kuhusiana na ushindi wa Uti na pia kushindwa kwa Mwisho Mwampamba ambaye ndiye alikuwa akiiwakilisha Tanzania ndani ya jumba la Big Brother.
Kumekuwepo na maoni kwamba Mwisho hakushinda kwa sababu watanzania wengi,hususani wale waliokuwa na uwezo wa kupiga kura,hawakufanya hivyo na badala yake kuishia kumtakia kheri bila kutimiza kitendo muhimu cha kupiga kura za kuwatoa wengine ili Mwisho abakie na hatimaye kuibuka mshindi.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini Kenya, nchi zilizopiga kura ili kumuokoa Uti zilikuwa ni Angola, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mozambique, Nigeria na Uganda wakati mshindi wa pili, Munya, kutoka Zimbabwe, alikingiwa kifua na Botswana, Malawi, Namibia, South Africa, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Mwisho Mwampamba.
Kama takwimu hizo ni za kuaminika, lipo jambo ambalo watanzania inabidi tujifunze.Ushindi hauletwi na maneno peke yake.Ni sharti maneno yaambatane na vitendo.Ushabiki bila vitendo ni kazi bure.
Hivi sasa, kupitia mitandao mbalimbali, tunashuhudia kampeni za nguvu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 nchini mwetu.Kuna mwamko wa aina yake ambao haujapata kutokea. Hakuna anayezembea.Ndio maana tunaona kila mtu yuko “busy”.Wananchi wengi wanatoa maoni yao.Kuna wanaotaka mabadiliko na kuna ambao bado wanasema “Jini likujualo,halikuli likakwisha”.
Hali niliyoieleza hapo juu inatia moyo.Binafsi naamini kwenye mseto wa kiserikali ambapo hakuna chama kinachoweza kupitisha kila kitu bungeni ati kwa sababu tu, kufuatana na demokrasia, basi “mwenye nyingi mpe”.Naamini kwenye check and balance yenye kufanya kazi kivitendo na sio maneno ya kwenye kamusi na katiba.
Basi ushabiki wa kampeni za kisiasa,usiishie kwenye maneno tu.Kama una uwezo wa kupiga kura,basi tarehe 31 Octoba,damka nenda katimize wajibu.Tujifunze kutokana na tulichokiona majuzi katika Big Brother Africa.Ushabiki na kutakiana kheri bila vitendo ni kazi bure.
Pichani juu:Uti(mwenye rasta) akifurahia ushindi wake.

Kwa mujibu wa jamaa wa Technorati,inakadiriwa kwamba blog mpya zaidi ya mbili huanzishwa katika kila sekunde,kila siku.Mpaka tarehe 31 Julai mwaka 2006 kulikuwa tayari na blog zaidi ya milioni 50!
Pamoja na mafanikio hayo ya uandishi huu unaoitwa uandishi wa kiraia (Citizen Journalism) ,bado hakuna takwimu za uhakika zinazoonyesha ni blogs ngapi “zinakufa” kila siku au kutelekezwa.Lakini ni wazi kwamba ni nyingi pengine kupita kiasi.Mtu anaanza kublog kwa kasi ya aina yake.Baada ya siku chache haonekani tena hewani.Amekosa muda au amekosa hamasa.Lengo alilokuwa nalo limempotea. Hawezi tena.Kila mtu ana majibu yake.
Ndio maana inapotokea mtu akadumisha blog yake kwa angalau mwaka mmoja inasemekana hawezi kuacha tena ku-blog.Kimsingi mtu huyo anastahili sio tu pongezi bali heshima.
Mmojawapo miongoni mwa watu hao ni mwanadada anayeonekana pichani hapo juu.Kwa wengi anajulikana kama TK lakini jina lake halisi ni Teddy Kalonga.TK ni miongoni mwa watu wanaotambulika kirahisi nchini kwetu ambao hawajabaki nyuma kunako tekinolojia hii ya blog.Hivi majuzi alisheherekea mwaka mzima tangu aanzishe blog yake inayopatikana kwa kubonyeza hapa.
Tunaungana na wengine wote kumpongeza TK na kumtakia kila la kheri katika kuendeleza “libeneke” kama anavyopenda kusema mwanablogu mwingine maarufu,Muhidini Issa Michuzi.Bonyeza hapa uone jinsi Teddy alivyosheherekea mwaka wake mmoja wa ku-blog.Hongera.
NB: Kama na wewe una blog yako na unasheherekea mwaka au miaka,usisite kuujulisha umma kupitia hapa hapa ndani ya BC.

Kama tulivyoahidi,huyu hapa ndio mwakilishi wetu huko South Africa katika shindano la Big Brother Africa III. Jina lake anaitwa Latoya.Ana miaka 21.Ni Katibu Muhtasi.Ukitaka kuwaona washiriki wenzake bonyeza hapa.

Lile shindano maarufu lijulikanalo kama Big Brother Africa linaloendeshwa na kituo maarufu cha televisheni cha Afrika Kusini(M-Net) linaanza tena leo nchini Afrika Kusini huu ukiwa ni msimu wa tatu tangu kuanzishwa kwake.
Jumla ya washiriki 12 wataingia leo kuanzia saa moja jioni tayari kuishi ndani ya jumba la Big Brother kwa siku 91 huku kila wanachokifanya kikirekodiwa kwenye kamera.Mshindi anatarajiwa kupata dola za kimarekani laki moja.
Kama mtakumbuka mshindi wa mwaka shindano lililopita alikuwa Richard Bezuidenhout (pichani) kutoka Tanzania.Majina au sura za washiriki wa mwaka huu bado ni siri ya waandaji na watajulikana pindi shindano litakapokwenda “live”.Pamoja na siri iliyopo kuna habari kwamba safari hii Tanzania inawakilishwa na msichana.Nani atamrithi Richard? Mwakilishi wa Tanzania ni nani?Tutawapasha punde.

Irene Sanga(kushoto) akiwa jukwaani na Elidadi Msangi.
Kama ikitokea ukawa umechoshwa na kusikiliza nyimbo au miziki inayoelemea upande mmoja tu(mara nyingi upande wa mapenzi) basi hutojutia kubadilisha frequency na kusikiliza wimbo uitwao Salamu Zangu ukiwa ni utunzi mahiri wa msanii Irene Sanga ambaye ameuimba wimbo huo kwa kuwashirikisha msanii maarufu wa mashairi,Mrisho Mpoto na Elidadi Msangi. Salamu Zangu ni mojawapo ya vibao ambavyo vilitokea kupendwa sana nchini Tanzania na kimebakia kuwa gumzo mpaka hivi leo.
Akiongea na BC hivi karibuni, Irene Sanga,alisema aliamua kutunga au kuandika mashairi kama unavyoweza kuyasikia katika wimbo huu,baada ya kukerwa na jinsi ambavyo wasanii wengi wa muziki wanavyokuwa wameegemea zaidi upande wa nyimbo za kimapenzi peke yake na hivyo kusahau kabisa pande zingine za maisha ya jamii kwa mfano umasikini,uonevu nk.Kwake yeye,anasema, muziki au sanaa sio chombo cha kuburudisha tu bali kuonya,kukosoa,kukumbusha nk.

Mshairi Mrisho Mpoto akituma Salamu zake kwa mjomba.
Wimbo huu umo ndani ya albamu iitwayo “Utandawazi” ambayo Irene anasema bado hajaamua kuitoa rasmi sokoni kutokana na sababu mbalimbali.Nyimbo zingine ndani ya albamu hiyo ni kama vile Utandawazi(inayobeba jina la albamu), Pangisheni,Maureen,Usivunje,Ndoto,Afrika Yote na huu Salamu Zangu/Salamu kwa Mjomba.Albamu hiyo imetengenezwa ndani ya Mawingu Studio jijini Dar-es-salaam.
Wimbo huu ambao leo ndio unatupa burudani ya wiki ni ombi rasmi kutoka kwa Pius Mikongoti.Pata Burudani.Wikiendi Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Picha zote na Bob Sankofa.

Kampuni ya kitanzania ya Beatiful Tanzania Agency inayojihusisha na mambo ya urembo hapo jana imewataja washiriki watano bora kutoka katika shindano linalojulikana kama Face of Tanzania, ambao watakwenda nchini Afrika Kusini hapo kesho kwa ajili ya kupata uzoefu mbalimbali katika fani hiyo. Kampuni hiyo ipo chini ya usimamizi wa warembo maarufu wa kitanzania, Irene Kiwia na Nancy Sumary.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo kwa vyombo vya habari, warembo hao watano ambao wametajwa kuwa ni Edna Makanzo,Emmy Malau,Irene Shirima,Neshino Laizer na Yvone Joseph. Warembo hao ni miongoni mwa warembo 16 walioanza shindano hilo kabla ya kuchujwa na kubakia warembo 10 na hatimaye 5 hivi sasa ambao ndio wanaelekea Afrika Kusini kwa uzoefu zaidi.Warembo hao ndio wanaotarajiwa kushiriki katika fainali tarehe 26 Aprili katika ukumbi wa Ubungo Plaza.
Wakiwa nchini Afrika Kusini, washiriki hao wanatarajiwa kutembelea makampuni kadhaa ya uwakala wa urembo kama vile O-Model Afrika na pia kufanya mazungumzo mbalimbali na warembo wa kitanzania wafanyao shughuli zao huko kama vile Happiness Magessa na wengineo ili kujua zaidi undani wa shughuli hizo.
Pichani juu ni warembo hao watano wakiwa na maboss wao Irene Kiwia(mbele kulia) na Nancy Sumary(kushoto) wakati wa utangazwaji wa majina ya warembo hao katika hoteli ya Regency Mikocheni jijini Dar hivi leo. Warembo hao waliosimama kutoka kushoto ni Edna Makanzo,Emmy Malau,Irene Shirima,Neshino Laizer na Yvone Joseph.Mikononi wameshikilia pasi zao za kusafiria

Shindano la kumtafuta star mpya wa Tanzania(Bongo Star Search) kwa upande wa muziki lilifikia ukingoni jana kwa mwanadada aitwaye Misoji Mkwabi kuibuka mshindi.Fainali za shindano hilo zilifanyika hapo jana ndani ya ukumbi wa Ubungo Plaza.
Misoji alijinyakulia kiasi cha Tshs. milioni 15,Furniture,TV ya LG pamoja na masomo ya kompyuta katika chuo cha Desktop Computer na masomo ya uandishi wa habari kwenye chuo cha DSJ (Dar es salaam School of Journalism.
Pichani juu ni Mc Jimmy Kabwe akiwa na Misoji Mkwabi jukwaani.

Kwa picha na habari zaidi za tukio hili mtembelee MichuziJR.Kwa mahojiano tuliyowahi kufanya na mwanzilishi na mmojawapo wa majaji wa shindano hili,Rita Paulsen, bonyeza hapa.


sending...