
Pichani ni Mbunge wa Same Mashariki,Mheshimiwa Anna Kilango Malecela.Mbunge huyu katika siku za karibuni ametokea kuwa miongoni mwa wabunge wanaoonekana kuwa na dhamira nyoofu katika kuupinga ufisadi nchini Tanzania.Inatia moyo kiasi fulani kuona kwamba kumbe wapo wabunge au viongozi ambao angalau wanaonyesha kukerwa na hali halisi(hali mbaya) ya mambo nchini mwetu.
Yupo msomaji wetu mmoja ametuuliza;hivi ufisadi ni tabia inayoanzia ukubwani au ni tabia ambayo mtu anakua nayo tangia utotoni?Mazingira ya kazi ya mtu yana mchango gani katika kuendeleza au kuamsha tabia za kifisadi?Tunaomba msaada wa majibu ya maswali hayo kama unayo.

Kama kawaida yetu,tunapotumiwa swali/maswali na baadhi yenu ambayo kimsingi tunahisi hatuwezi kuwa na jibu/majibu yenye uhakika au yanayojitosheleza,huwa hatuna budi kuomba msaada kutoka kwako msomaji.Katika mfulululizo huo huo; msomaji wetu mmoja ametuandikia akiomba kupata maoni kuhusu nani unadhani ndiye amewahi kuwa Waziri Mkuu bora kushinda wengine wote katika historia ya nchi yetu ya Tanzania mpaka hivi sasa?
Msomaji wetu huyu, anasema, kwa upande wake,Hayati Edward Moringe Sokoine (pichani) ndio aliwahi kuwa Waziri Mkuu bora. Unakubaliana naye?Kwa upande wako,ni Waziri Mkuu yupi ambaye unadhani ni bora kushinda wengine mpaka hivi leo?

Kamati kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana chini ya Mwenyekiti wake,Rais Jakaya Kikwete,imemthibitisha Mchungaji Dr.Getrude Rwakatare kuwa mbunge wa viti maalumu,kurithi nafasi ilioachwa wazi na marehemu Salome Mbatia aliyefariki Octoba mwaka huu kwa ajali ya gari.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar jana mara baada ya kikao cha kamati kuu,katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM Itikadi na Uenezi,Bw.John Chiligati,alisema kufuatia uamuzi huo, mchungaji Rwakatare sasa ni Mbunge mteule akisubiri kuapishwa wakati wa mkutano ujao wa Bunge utakaofanyika januari mwakani.
Picha na habari hii kwa hisani ya MichuziJR.

Nchini Tanzania yapo majina ya wanasiasa/viongozi wa vyama na serikali ambayo huwa hayahitaji mzunguko mrefu wa kuyatambulisha.Ni majina ambayo yamezoeleka kutokana na aidha kuwa familia ya wanasiasa au kutokana na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika vyama vya kisiasa.
Umaarufu wa majina au watu wenyewe unakuja kirahisi ukizingatia uhusiano wa karibu uliopo kati ya siasa na jamii zetu.Kama ilivyo katika nchi nyingi duniani(kama sio zote) mustakabali wa maisha ya jamii unategemea sana siasa/uongozi.
Mojawapo ya majina hayo maarufu ni la Pius Msekwa(pichani) ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.Msekwa ameshawahi kushikilia nyadhifa nyingi mbalimbali,ndani na nje ya nchi.Ukitaka kujua mengi kumhusu,bonyeza hapa.

Pichani ni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania,Mh.Cleopa David Msuya (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa sasa wa Tanzania,Mh.Edward Lowassa.Hawa wote wanatokea kaskazini mwa Tanzania.
Ni wazi kwamba wiki moja iliyopita na hii tunayoelekea kuimaliza zimekuwa na ugumu wa aina yake. Kwanza zilikuwa ni habari za kuuawa kikatili mwanamuziki wa miondoko ya reggae kutoka Afrika Kusini,Lucky Dube na kisha habari za ajali mbaya ya gari iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Salome Joseph Mbatia, dereva wake (jina bado hatujalipata) na utingo wa fuso iliyogongana naye aliyekuwa anaitwa Castory Kilagwa (22).
Kwa ujumla habari za namna hii huleta simanzi na majonzi makubwa. Katika wakati huu mgumu kwa ndugu,jamaa na marafiki wote waliofikwa na misiba huku pia tukikumbuka kwamba wapo watu wengi wengine ambao nao pia wamepoteza ndugu,jamaa na marafiki (ingawa kutokana na nafasi zao katika jamii habari zao hatuzisikii kama hizi za wengine), BC inapenda kuwapa pole wafiwa wote na pia wote mnaokabiliwa na matatizo mengine yoyote ya kimaisha.
Sasa kwa sababu leo ni ijumaa na kama kawaida yetu huwa tunapata mdundo, wimbo wa leo unaitwa Three Little Birds kutoka kwa Mfalme wa Reggae duniani,Hayati Bob Marley.Wimbo huu ndio ulikuwa wimbo rasmi wakati wa mazishi ya yake. Bonyeza umsikie Bob akikukumbusha kwamba Usihofu sana, kila kitu kitakuwa sawa.Maneno ya wimbo unaweza kuyapata hapa. Ijumaa Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

MWILI wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, aliyefariki dunia mkoani Iringa juzi, unatarajiwa kuzikwa jumamosi hii huko Moshi baada ya kuagwa nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam kesho(ijumaa).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge, Mheshimiwa Samuel Sitta, nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Uganda,Oysterbay jijini Dar-es-salaam leo,mwili wa marehemu utasafirishwa kesho(ijumaa) saa 8:00 mchana kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi siku hiyo ya Jumamosi.
Hata hivyo, Sitta alisema hadi kufikia leo mchana, hakuwa na uhakika wa eneo ambako mwili wa marehemu utazikwa na kwamba, suala hilo liko ndani ya maamuzi ya familia.
Lakini akasema huenda mwili huo ukazikwa katika kijiji cha Kirua, Wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani humo ambako mume wa marehemu, Dr.Joseph Mbatia, anatoka kulingana na mila za Kichagga.
Alisema ibada (misa) ya kuuombea mwili wa marehemu, itafanyika nyumbani kwake leo(ijumaa) saa 4:00 asubuhi kabla ya kusafirishwa na inatarajiwa kuhudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwamo wabunge.
Alisema wenyeviti kumi wa kamati za Bunge zinazoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Dk Batilda Buriani, leo walikutana kupanga uwakilishi katika mazishi ya marehemu.
Akizungumzia msiba huo, Sitta alisema kifo cha Waziri Mbatia, kimeacha pengo kubwa bungeni kutokana na kumpoteza Mbunge mwenye vipaji vingi muhimu ambavyo viliwapa matumaini ya kuwa waziri kamili katika siku za baadaye.

Huwezi kuongelea haki za wanawake duniani bila kumtaja Balozi Gertrude Ibengwe Mongela (pichani) Leo hii miongoni mwa wengi anajulikana kama “Mama Beijing”. Hii ni kutokana na yeye kusimamia mkutano maarufu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na wanawake uliofanyikia katika jiji la Beijing nchini China mwezi Septemba mwaka 1995. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, raia wa Misri, Boutros Boutros Ghali ndiye aliyemkabidhi Balozi Mongela dhamana hiyo.
Leo hii ndiye mwanamke wa pili barani Afrika mwenye madaraka ya juu kabisa ya kuchaguliwa. Wa kwanza ni Raisi wa Liberia, mwanamama Ellen Johnson Sirleaf. Mama Mongela ni raisi wa Bunge la Afrika nafasi ambayo anaishikilia tangu mwezi March mwaka 2004 alipochaguliwa. Bunge la Afrika liliundwa mwaka huo huo wa 2004 na hivyo kumfanya Balozi Mongella kuwa raisi wake wa kwanza. Lakini madaraka na uwajibikaji kwa Gertrude Mongela sio jambo geni hata kidogo. Kama ambavyo utaweza kuona hapo chini kwenye CV yake, Mama Mongella sio tu mpigania haki za wanawake bali pia ni mfano ulio hai kwamba cha msingi sio jinsia bali uwezo binafasi wa mtu. Bila ubishi, Balozi Mongella ni mmojawapo kati “mabalozi” nyeti kabisa tulionao nchini Tanzania. (more…)

Sote tunaweza kuwa maarufu, tunaweza kuwa chochote tunachotaka . Pamoja na hayo, jambo moja ambalo ni dhahiri itakuwa ni vigumu sana kulifikia ni kuwa maarufu na kuheshimika duniani kote kama ilivyokuwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye hivi leo tunakumbuka miaka nane tangu afariki dunia mnamo tarehe kama ya leo mwaka 1999 kule nchini Uingereza katika hospitali ya Mtakatifu Thomas kwa ugonjwa wa saratani ya damu (leukemia).
Serikali ilipotangaza rasmi kwamba Nyerere hatunaye tena, uchungu na simanzi uliikumba nchi nzima na dunia kwa ujumla hususani kwa wale waliokuwa wanamjua Nyerere na kujua alichokuwa akikisimamia na alichokiamini. Bara la Afrika likawa limempoteza kipenzi chake, mtoto wa Afrika ambaye thamani ya mchango wake katika ukombozi wa bara la Afrika haina kipimo. Mpaka anafariki dunia alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha amani barani Afrika.Mfano mzuri ni mgogoro wa Burundi aliokuwa akijaribu kuusuluhisha. Mwenyewe aliwahi kutamka kwamba yeye ni mwafrika kwanza na kisha mjamaa.
Mpaka leo hii jina la Nyerere linabakia kuwa kitambulisho chetu kikubwa .Wakati mwingine zaidi hata ya jina la nchi yetu yaani Tanzania.Wapo watu wanaolijua jina la Nyerere na wala wasijue jina la Tanzania au hata Tanganyika. Haishangazi, alikuwa ni mwana wa Afrika kamili. Kadiri siku zinavyopita, taratibu baadhi yetu, hususani vijana wanaoitwa wa kizazi kipya, wanazidi kulisahau jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Viongozi wetu wengi wa sasa( ingawa wakati wa msiba wake waliahidi kumuenzi kwa hali na mali) wanaelekea kusahau kabisa ahadi zao! Wengi wanabakia kumuenzi kwa maneno na sio vitendo. (more…)

