Huwa nakipenda kipengele hiki cha “unamtambua” kwa sababu moja kuu.Historia.Nilipokuwa shule(shule ya kawaida kwa sababu ya maisha haiishi),nilipenda sana somo la historia.Bahati nzuri nilipata waalimu ambao walilipa somo la historia uhai(they gave it life).Walikuwa wakifundisha na kukupeleka kinadharia katika kitu wanachokiongelea.

Ni katika kipindi hicho ambapo tulikwenda kwenye Empires mbalimbali barani Afrika kama vile Mwanamutapa,Ashati,Zulu nk. Tukaona jinsi kina Dedan Kimathi walivyojipanga na kumpinga mkoloni nchini Kenya.Tukaona jinsi ambavyo Mau Mau warriors walivyokuwa makini katika mapambano yao.Nilimpenda Shaka Zulu kutokana na simulizi za waalimu wangu kabla hata sijaiona filamu ya Shaka Zulu ambapo Henry Cele alikuja kuwa ufafanuzi wangu kumhusu Shaka Zulu(Pumzika kwa amani Henry Cele)

Nakumbuka jinsi nilivyomsikiliza kwa makini na shauku mtunza mapango ya Amboni (Amboni Caves) kule Tanga alivyokuwa akitupa simulizi za jamaa aliyeitwa Osare Otango ambaye aliishi ndani ya yale mapango katika hekaheka za kumkimbia mkoloni na kuendesha kampeni ya kumuondoa.

Nisiendelee sana mwisho nisahau ninachotaka kukisema.Je,unamtambua aliyepo pichani?

dilingabc

Muziki ni lugha ya ulimwengu(universal language). Bila shaka umeshawahi kusikia msemo huo. Mimi binafsi nakubaliana kabisa na msemo huo. Kuna nyakati nimewahi hata kujiuliza,hivi dunia ingekuwaje kama kusingekuwa na muziki? Tunapokutana na kusheherekea tukio fulani,vigelegele na mayowe vingetosha?

Wakati kazi ya kubwa ya kutuletea burudani ya muziki inaanzia kwa msanii mwenyewe,pembeni yake, kwa miaka nenda rudi, amekuwepo mtu muhimu katika kukamilisha safari hiyo. Mtu huyo ni DJ au Deejay au Disco Jokey kwa wale wenzangu na mie tuliokula chumvi kidogo!

Mwanamuziki/Msanii anapomaliza kazi yake kwa kushirikiana na producer wake, hukimbilia kwa DJ kwani anatambua kabisa kwamba huyo ndiye kiungo kikuu kati yake na mashabiki au wapenzi wa muziki kwa ujumla.

Miongoni mwa DJs ambao sio tu wameifanya kazi yao kwa ustadi mkubwa bali pia waliowahi kujizolea sifa na mashabiki wa kutosha ni DJ John Dillinga Matlou au maarufu kama DJ JD. John ana historia ndefu katika muziki. Mwenyewe anasema,aliianza safari yake tangu akiwa mtoto kabisa. Mpaka hivi leo bado anaendelea kuwapa watu burudani. Hivi sasa anaendesha kampuni ya JD Entertainment ambayo inashughulika na masuala yote ya burudani,promotions na kadhalika.

Nilipofanya naye mahojiano  ambayo utayasoma hivi punde,niligundua mambo kadhaa muhimu;DJ JD ni mbunifu wa aina yake. Aina za vipindi alivyovianzisha na kuviendesha(hususani redioni) ndivyo pengine vilivyochangia mafanikio ya baadhi ya vituo vya redio vya FM tunayoyaona hivi sasa.Pia niligundua kwamba huyu ni miongoni mwa wale DJs ambao wanaifanya kazi yao sio kwa ajili ya kutafuta pesa peke yake bali kwa sababu anaupenda muziki na yote yale yatokanayo na muziki mzuri wenye kuleta burudani na starehe.

Fuatana nami katika mahojiano haya ambapo,pamoja na mambo mengine,DJ JD anaelezea hisia zake kuhusu ulimwengu wa muziki na burudani hivi sasa. Pia anajibu swali ambalo wapenzi wengi wa muziki wamekuwa wakitaka kumsikia akijibu; Je yeye na DJ Bonny Luv ni mahasimu au ni watu wawili wanaoipenda kazi yao na pia kushirikiana kwa karibu? Je unajua kwamba baba mzazi wa DJ JD sio mtanzania bali raia wa…? Endelea kusoma

BC: Karibu sana ndani ya BC. Tunafurahi kupata fursa hii ya kufanya nawe mahojiano haya.Mambo vipi?

JD: Mambo sio mabaya kusema ukweli.Namshukuru Mungu.

BC: Kwa sababu hii ni mara yetu ya kwanza kufanya nawe mahojiano na kwa sababu tunatambua kiu ya wengi(hususani mashabiki wako) labda ungeanza kwa kutueleza kwa kifupi historia ya maisha yako.Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi na mambo kama hayo. read more

Tafadhali naomba usinichoke kwa kupenda kutundika masuala/hotuba za Obama.Nafanya hivyo kwa kuamini kwamba kila siku binadamu tunajifunza au tunatakiwa tujifunze mambo mapya.Hotuba za Obama zawezekana kuwa hazikufunzi mambo mapya ila kwa mapana na marefu naaamini zinatukumbusha mambo mbalimbali.Pia namfuatilia Obama kwa sababu angalau yeye ndio mwanasiasa ambaye namuona hapendi “kuongopa waziwazi”.Obama hawezi kukuambia kesho atakujengea daraja wakati moyoni mwake anajua kabisa hela za daraja alishakula. Hawezi pia kutoa ahadi za maisha bora kwa wote bila kukumbusha kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo.

Obama anaweza kuwa anaongea na kundi fulani tu la watu lakini akawa anatoa ujumbe mkali kwa jamii mbalimbali.Cha msingi labda ni kusikiliza kwa makini na kufanya tathmini makini. Hivi majuzi Obama alialikwa na kutoa hotuba wakati wa kusherekea miaka 100 ya chombo muhimu cha Wamarekani Weusi kinachoitwa NAACP(National Association for the Advancement of Colored People)

Katika hotuba yake,Obama aliongelea mengi.Muhimu zaidi ambalo naamini hata sisi watanzania tunaweza kujihusisha nalo ni suala la elimu kwa watoto wetu,jamii zetu. Ulimwengu wa leo,wa ushindani wa namna hii,unahitaji elimu makini.Je tunafanyaje katika hilo? Viongozi wetu wanatupeleka wapi? Hebu tujiulize, tangu marais wetu waliofuatia baada ya J.K.Nyerere wametusaidia kujenga maktaba ngapi? Hivi unajua jiji la Dar-es-salaam lina maktaba ngapi?

You need to a flashplayer enabled browser to view this YouTube video

jkmbc

Binadamu huwa na wakati wa kilio na pia wakati wa kucheka(furaha).Pichani ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete akifurahia jambo na Mkuu wa Majeshi wa Tanzania,Davis A.Mwamunyange wiki iliyopita wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 47 ya Uhuru wa Tanganyika zilizofanyikia katika Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.

Photo Credit/Yahya Charahani

Historia ya muziki wa kizazi kipya au Bongo Flava kama unavyojulikana miongoni mwa wengi hivi leo una historia ndefu. Ni historia ndefu kiasi kwamba hivi leo wengi hatukumbuki tena hata muziki huu ambao hivi leo umetokea kuwa kipenzi cha wengi ulianzaje,ukapitia hatua na harakati gani mpaka kufikia hapa ulipo hivi leo.

Miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo wa harakati za mwanzo kabisa za muziki wa bongo flava ni aliyewahi kuwa DJ maarufu nchini Tanzania kwa jina Mike Pesambili Mhagama(pichani).Mike sio tu miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo bali pia ni miongoni mwa watu wachache walioamini katika muziki wa kizazi kipya tokea mwanzo.Kumbuka hizo ni zile enzi ambapo muziki huo ulikuwa ukichukuliwa kama “uhuni” tu na sio aina mpya ya muziki au burudani.Ni watu wachache sana walioweza kutabiri hatua ambazo muziki huo ungepiga miaka kumi au kumi na tano baadaye.
Lakini pia Mike amekuwa akikerwa na jinsi ambavyo kumekuwepo na upotoshwaji au upindishwaji wa vipengele fulani fulani muhimu vya historia ya muziki huo. Katika kujaribu kuiweka vyema historia hiyo,Mike Mhagama ameandika kwa mapana na utulivu wa kina kuhusu harakati za mwanzo za muziki wa kizazi kipya,suluba walizopitia yeye na watangazaji wenzake katika kuutambulisha muziki huo,wadau mbalimbali anaowakumbuka katika harakati hizo,wanamuziki wenyewe,promoters wa muziki nk.

Pia Mike Mhagama,anaweka wazi kitu ambacho watu wengi wamekuwa wakijiuliza;Nini chanzo cha neno Bongo Flava? Nani mwanzilishi wake?Kwa jibu hilo na historia nzima,kwa jinsi anavyoikumbuka Mhagama, msome kuanzia hapo chini,kwa maneno yake mwenyewe, kama tulivyoyanakili kutoka katika blog yake(kwa ruhusa na baraka maalumu).Habari imegawanyika katika sehemu nne ili iwe rahisi kwako kuzisoma na  kuelewa vyema anachokizungumzia Mike Mhagama. Mwenyewe anasema yawezekana kabisa asiwe sahihi kwa asilimia zote na ndio maana anapenda kukaribisha hoja,maoni na masahihisho yoyote kutoka kwako msomaji.Mike Mhagama hivi sasa anaishi huko Los Angeles,California nchini Marekani.

CHIMBUKO LA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA TANZANIA NA MAANA HALISI YA NENO BONGO FLAVA.

Na Mike Mhagama-Los Angeles,Marekani.

SEHEMU YA KWANZA

M
oja kati ya mambo niyapendayo mno maishani ni muziki.Nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa muziki si tu ule wa nje lakini kwa karibu ule wa nyumbani hasa muziki wa dansi na ule wenye umaarufu sana hivi sasa ujulikanao kama Bongo Flava (Muziki wa Kizazi Kipya).Katika mapenzi hayo imekuwa kama bahati kuwa mmoja wa vijana wengi tuliobahatika kuuona muziki huu wa kizazi kipya ukizaliwa na pengine bahati zaidi bila kusita kusema;kuwa mmoja kati ya wale tulioanzisha kusukuma gurudumu la muziki huu kufikia hapa ulipo na nafasi yake kutambulika si tu Afrika Mashariki bali pia kwa sasa duniani kwa ujumla.

Kama ilivyo kwa aina zingine za muziki Tanzania,mfano muziki wa dansi basi utakuwa mkosefu wa fadhila bila kujumuisha majina kama Patrick Balisidya,Mbaraka Mwaruka Mwinshehe,Salum Abdalah na hata Remmy Ongara.Hawa ni vinara na walifanya kila wawezalo kuja na ubunifu si tu kuvutia wateja wao bali kuutangaza muziki wao ndani na nje ya nchi na kuipa Tanzania kitambulisho chake kwenye jukwaa la sanaa ya muziki.Kazi za wanamuziki hawa zilifana sana kwa ushirikiano mkubwa na chombo ambacho kwa Tanzania ni muhimu sana katika kueneza au kutambulisha kitu kipya,RADIO.Watangazaji kama Mzee Ibrahim Chimgege,Enock Ngombale,Timothy Pata,Abisai Stephen,Seif Salum Nkamba na Julius Nyaisangah chini ya ma-bwana mitambo mahiri kama akina James Mhilu na Crispin Lugongo wanastahili pongezi kwa kiasi kikubwa katika kurekodi na kusimamia mitambo wakati wanamuziki hawa wakitafuta majina na namna ya kujitambulisha kwa jamii itakayosikiliza muziki wao.Bahati mbaya huwasikii sana watu hawa katika zinazoitwa historia kwa sababu wengi ni rahisi kuwasahau lakini mchango wao ni mkubwa sana na unastahili heshima hasa unapoandika au kuizungumzia historia ya muziki wa dansi Tanzania. read more

 

Kama kawaida yetu,tunapotumiwa swali/maswali na baadhi yenu ambayo kimsingi tunahisi hatuwezi kuwa na jibu/majibu yenye uhakika au yanayojitosheleza,huwa hatuna budi kuomba msaada kutoka kwako msomaji.Katika mfulululizo huo huo; msomaji wetu mmoja ametuandikia akiomba kupata maoni kuhusu nani unadhani ndiye amewahi kuwa Waziri Mkuu bora kushinda wengine wote katika historia ya nchi yetu ya Tanzania mpaka hivi sasa?

Msomaji wetu huyu, anasema, kwa upande wake,Hayati Edward Moringe Sokoine (pichani) ndio aliwahi kuwa Waziri Mkuu bora. Unakubaliana naye?Kwa upande wako,ni Waziri Mkuu yupi ambaye unadhani ni bora kushinda wengine mpaka hivi leo?

 

Pichani ni Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania na miongoni mwa wanasheria mahiri ambao Tanzania inajivunia.Pamoja na hayo katika siku za hivi karibuni amekuwa akitoa kauli mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinawachanganya wananchi.Mfano ni kauli yake ya hivi karibuni kuhusiana na suala la kujiuzulu kwa Lowassa na jinsi ambavyo tume ya Mwakyembe “haikumuita” EL ili kumpa nafasi ya kujitetea.

Jaji Warioba alizaliwa tarehe 3 Septemba mwaka 1940 huko wilayani Bunda mkoani Mara. Alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia tarehe 5 Novemba mwaka 1985 mpaka tarehe 9 Novemba mwaka 1990 alipompisha John Samuel Malecela.Unaweza ukapata zaidi CV yake kwa kubonyeza hapa.

 

Jiji la Dar-es-salaam lina historia ndefu sana.Tangu enzi hizo likiitwa Mzizima mpaka wajanja walipolibatiza jina maarufu la “Bongo” ingawa baadaye “Bongo” imekuja kuwa sio tu jiji la Dar-es-salaam bali Tanzania nzima.

Katika historia mbalimbali za jiji la Dar,mojawapo ni kuwa na wakuu wake wa mkoa ambao huwa na machachari na mbwembwe za aina yake.Nani anaweza kusahau kwamba kuna wakati jiji la Dar-es-salaam lilikuwa linajulikana kama “Jiji la Makamba” kutokana na uongozi wa Mheshimiwa Yusuf Makamba?

Historia ya Dar bado inaendelea kuandikwa.Kila kukicha Dar inazizima na mambo mapya.Kila siku kuna geni jijini Dar.Kila siku maelfu ya wananchi wanatoka mikoani na kuhamia jijini Dar kwani inasemekana Dar ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.Haishangazi kwamba mpaka hivi leo,kuhamia Dodoma kwa serikali kumebakia kuwa sera isiyotekelezeka.

Hivi sasa jiji la Dar-es-salaam lipo chini ya uongozi wa Mheshimiwa Abbas Kandoro.Hivi sasa anapumua baada ya jiji lake/letu kufikwa na ugeni mzito wa George W.Bush.Historia yake ndio hivyo inaandikwa.

Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Dar,Abbas Kandoro(kushoto) na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo kabla ya Kandoro,Mheshimiwa Yusuf Makamba.Makamba hivi sasa ndiye Katibu Mkuu wa CCM taifa.

Ukiachilia mbali blogs au tovuti mbalimbali zinazojitahidi kuhifadhi historia au kumbukumbu za watu wetu mashuhuri mtandaoni,mradi kama Wikipedia ndio pengine unaongoza hivi sasa katika kuhifadhi historia mbalimbali,kuelimishana,kupashana habari nk.Uzuri ni kwamba Wikipedia inaandikwa katika lugha mbalimbali ikiwemo yetu ya Kiswahili. Burudani zaidi inakuja pale ambapo wote,mimi na wewe,tunaweza kuchangia katika kuziandika historia za watu wetu mashuhuri.Hapo hakuna mjuzi zaidi ya mwingine.Kila mtu anajua kitu fulani kwa hivyo anachangia. Kama nitaandika kwamba Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1962,nitakuwa nimekosea.Bila kutoana ngeu,unaingia unanirekebisha tunapata ukweli.Huo ni mfano tu,Wikipedia ina maarifa mengi zaidi.

Kwa mfano; Hayati Bibi Titi Mohamed,pichani kushoto akiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni mtu mashuhuri na muhimu sana katika historia ya nchi yetu achilia mbali juhudi za ukombozi wa mwanamke.Pamoja na hayo,ukienda kwenye ukurasa wa Wikipedia wa Kiswahili,utakuta kwamba habari za Bibi Titi zimeandikwa kwa kifupi sana. Ni kama vile hakuna anayejua mengi kuhusiana na Bibi Titi,si watu wa enzi zake wala wa enzi hizi.Mbali na uchache wa habari za Bibi Titi kwenye Wikipedia,kwa ujumla mtandaoni habari zake zipo kwa uchache sana.Tunaishi katika nyakati mpya,za habari na mawasiliano ya hali ya juu.Ni muhimu tukazitumia katika kuhifadhi historia pia.Sio za Bibi Titi tu bali wengineo wengi waliowahi kutokea,waliopo na watakaoendelea kutokea nchini mwetu.

“Bibi Titi Mohammed ni mmoja wa wanawake wa kwanza kushika nafasi za ubunge na uwaziri nchini Tanzania na pia ni kati ya wanawake wa kwanza kujiunga na harakati za kugombea uhuru wa Tanganyika.

Mwaka 1969 Bibi Titi Mohammed alikamatwa na mwaka uliofuata alifikishwa mahakamani kwa kosa la kula njama ya kutaka kupindua serikali. Katika kesi hiyo, Bibi Titi alikuwa ni mwanamke pekee katika washtakiwa 7. Baada ya kesi hiyo kusikilizwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Hata hivyo, mwaka 1972 alisamehewa na rais Julius Nyerere

Ukienda kwenye ule ukurasa wa Wikipedia wa Kiingereza kumhusu Bibi Titi,utagundua kwamba pameandikwa mambo mengi kidogo kumhusu Bibi Titi. Kwanini? Mara nyingi tumekuwa tukiacha historia yetu,ya watu wetu,iandikwe na watu wengine.Wakiandika wanavyotaka wao,kwa kuipotosha, tunalalamika.Ajabu huwa hatuna muda wa kuirekebisha. Zamani tulikuwa na sababu,hatuna tena.

Kupitia kurasa kama Wikipedia,tunaweza rekebisha historia zetu.Kwanini leo usijiandikishe katika Wikipedia na kuanza kuchangia chochote unachokijua kuhusu historia,siasa,jamii zetu? Unaonaje kama tukianza na kupanua zaidi historia ya Bibi Titi Mohamed? Kumbuka unapohifadhi historia huhifadhi kwa ajili yako tu bali vizazi na vizazi vijavyo.Binadamu asiyejua historia yake ni….

Picha kwa msaada wa Issa Michuzi.

 

Kwa miaka nenda rudi, tangu miaka ya sabini,jina la Freddy Macha (pichani) limekuwa sio geni miongoni mwa wasomaji mbalimbali wa magazeti, vitabu vya hadithi fupifupi,wapenzi wa muziki na pia sanaa ya ushairi nchini Tanzania. Iwe unamfahamu Freddy kupitia muziki wake,makala zake au mashairi yake, utakubaliana nasi kwamba Freddy ni mojawapo ya hazina tulizonazo linapokuja suala zima la usanii. Wengi miongoni mwa wasomaji wa makala zake katika magazeti ya The Guardian na Mwananchi nchini Tanzania, wanakiri kwamba makala za Freddy huwa ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wakati mwingine wadamke asubuhi na mapema ili mradi tu wasikose nakala za magazeti hayo hususani siku zinazochapishwa makala zake.

Wapenzi wengi wa muziki,ushairi, tamthiliya na ngoma mtakuwa mnamkumbuka Freddy Macha tangu alipokuwa na kundi la Sayari. Kundi hilo ambalo lilitamba sana mwanzoni mwa miaka ya themanini, ni mojawapo ya vikundi vichache vya sanaa nchini Tanzania vilivyopata mafanikio sio tu nchini Tanzania bali pia katika medani za kimataifa. Sayari liliwahi kufanya ziara kadhaa za kimaonyesho katika nchi mbalimbali za nje hususani za Ulaya enzi hizo.

Kwa upande wa uandishi,Freddy Macha alianza kunoa kalamu katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo na baadaye kuwa mwanasafu(columnist) wa gazeti la kila jumapili la Sunday News hadi mwaka 1984.Freddy amewahi kushinda tuzo kadhaa za uandishi ikiwemo ile ya Ushairi ya BBC mwaka 1981 na hadithi fupi fupi ya Jumuiya ya Madola( Commonwealth of Nations) ya mwaka 1996.

Hivi karibuni, baada ya kumsaka kwa muda mrefu, tulipata nafasi ya kufanya mahojiano ya kina na mwandishi/mwanamuziki/mwalimu huyu ambaye hivi sasa anaishi London nchini Uingereza. Sasa kutokana na ukweli kwamba Freddy ni mmojawapo miongoni mwa wale watu ambao tunaweza kuwaitwa “wenye vipaji vingi”,tumeamua kuyagawa mahojiano yetu naye katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza, ambayo ndiyo hii unayoisoma leo, tumeongea naye zaidi kuhusu kazi zake za uandishi.Sehemu ya pili ambayo itawajieni baadaye kidogo,tuliongea naye kuhusu muziki,jamii na mengineyo kadha wa kadha.

Unataka kujua Freddy ametokea wapi?Amepitia mambo gani mpaka kufikia hapo alipo? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uandishi wa leo akilinganisha na ule wa zamani? Kwanini kitabu chake cha hivi karibuni amekiita Mpe Maneno Yake? Unafahamu kwamba Freddy aliwahi “kuzamia meli”?Ilikuwaje? Anasemaje kuhusu dhana za mawasiliano kama blogs? Kwa hayo na mengineyo mengi, fuatana nasi katika sehemu hii ya kwanza ya mahojiano yetu naye; read more

Read the Next Page →

↑ Go Back to Top of Page