
Timu yetu ya taifa ya soka,Taifa Stars, imerejea hapo jana kutoka huko nchini Ivory Coast ambako ilikwenda kushiriki mashindano ya CHAN (Africa Nations Championships)ambayo ni kama kombe la Afrika ila kwa wachezaji ambao wanacheza soka ndani ya bara la Afrika pekee bila kuwashirikisha wale wanaosakata kabumbu ughaibuni.Mashindano hayo yanatarajiwa kufikia kilele jumapili ijayo huko Ivory Coast.
Taifa Stars,hawakuambulia kombe ila mashabiki wengi wa soka,ndani na nje ya Tanzania,wanakubaliana kwamba Taifa Stars hivi sasa siyo ya kubeza.Sio tena kile kichwa cha mwendawazimu alichowahi kukizungumzia Rais mstaafu,Ally Hassan Mwinyi.
Miongoni mwa wachezaji ambao Tanzania hivi sasa inajivunia ni kijana mdogo Mrisho Ngassa(pichani).Ngassa ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza,Khalfan Ngassa,alizaliwa tarehe 5 mwezi wa May mwaka 1989.Bao la ushindi alilolifunga huko nchini Ivory Coast dhidi ya wenyeji Ivory Coast limeelezewa kuwa mojawapo ya mabao bora kabisa ya mashindano hayo.
Je nini kifanyike ili kuendeleza vipaji kama cha Ngassa na wachezaji wengine wengi nchini Tanzania?Kumbuka kwamba mpaka hivi leo,Tanzania bado haijatokea kupata au kutoa mchezaji ambaye akatamba hususani katika ligi kubwa za soka ulimwenguni kama ile ya Premier ya Uingereza au Seria A ya Italy au La Liga ya Spain kama ambavyo mataifa mengine(mengi ya Afrika Magharibi) yamekuwa yakifanya.
Halafu kuna mjadala ambao mwenzetu Issa Michuzi ameuanzisha.Ni kuhusu hatma ya kocha wa Taifa Stars,Mbrazil Maximo.Swali la msingi ni;Je mkataba wa Maximo usitishwe au apewe mkataba mpya.Unaweza kusoma na kuchangia mjadala huo muhimu kwa maendeleo ya soka nchini Tanzania kwa kubonyeza hapa.
BC inafanya juhudi za kumpata Ngassa kwa mahojiano rasmi.Stay tuned.

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo(pichani), alitangaza kikosi cha wachezaji 27 watakaoshiriki fainali za Afrika kwa nyota wa ndani, zitakazopigwa nchini Ivory Coast kuanzia Februari 22.Kwa habari zaidi bonyeza hapa.

Mchezaji maarufu aliyewahi kuichezea Simba Sports Club, APR ya Rwanda na ambaye kwa sasa alikuwa akiichezea timu ya Azam FC Club inayoshiriki ligi ya Vodacom Boniface Pawasa (Baba Ubaya ) amejiunga na Chuo Cha Biashara (CBE) cha jijini Dar-es-salaam mwezi mmoja uliopita ili kuongeza elimu.
Akizungumza na blog ya Full Shangwe hivi karibuni,Pawasa amesema kwa sasa umri wake umeenda hivyo anahitaji kutengeneza maisha mapya na yenye malengo ya baadae na ndiyo maana ameamua kufuata nyayo za wachezaji wenzake waliopita kwa kujiendeleza kielimu.
Pawasa amesema kwa sasa anasomea mambo ya utawala wa biashara ambapo atakuwa chuoni hapo kwa mwaka mmoja akisomea cheti katika fani ya utawala wa biashara yaani Business Administration. Pawasa pia amesema akimaliza anatarajia kuendelea na elimu yake ya Diploma mpaka atakapokamata digrii yake ya kwanza hapo ndiyo ataangalia afanye nini.
Pawasa amesema kuwa pamoja na kwamba kocha wa timu yake ya Azam Santos anamuhitaji ili arejee kundini kuipigania timu yake katika mzunguko wa pili wa ligi ya Vodacom hataweza kurejea tena kwa sababu pia ana maumivu ya misuli ambayo yatamchukua muda mrefu kupona hivyo ameona asipoteze muda kusubiri apone wakati anaweza kufanya kitu kingine cha maendeleo.
Amewashukuru wachezaji wenzake kwa kumpokea chuoni hapo na anasema kwa sasa anafurahia sana maisha ya chuoni kwani rafiki zake wa karibu Ally Mayay, Aron Nyanda na Wilfred Kidilu wamempokea na wanampa sapoti ya hali ya juu na kama wao wameweza kwa nini yeye ashindwe “najua nitaweza tu na nitasoma kama nilivyojiwekea malengo yangu” anamaliza Baba Ubaya.
Pichani juu Boniface Pawasa a.k.a Baba Ubaya(kulia) akiwa na mwenyeji wake na Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) Bw. Ally Mayay ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Yanga.
Habari na picha kwa hisani ya John Bukuku anayeendesha blog ya Full Shangwe.Mtembelee.

Hiki ndicho kikosi cha Taifa Stars kilichopambana na Cameroon mwishoni mwa wiki hii tunayoimaliza jijini Dar-es-salaam na kutoka sare ya bila kufungana.
Waliosimama mstari wa nyuma kabisa kutoka kulia ni Dan Mruanda, Nadir Haroub, Athumani Iddi, Shaaban Nditi na Salum Swedi.
Mstari wa kati kutoka kushoto ni Nizar Khalfani, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa na Amiri Maftaha.Aliyechuchumaa mbele ni Tanzania One, Ivo Mapunda.
Nini maoni yako kuhusiana na “droo” hii ya Taifa Stars na Cameroon?Unawaambia nini wachezaji wa Taifa Stars na kocha Maximo?
Photo/Mpoki Bukuku

Kwa wale wapenzi wa habari za michezo na burudani zikiwemo habari motomoto kuhusiana na ligi maarufu ulimwenguni kama vile Premier League, La Liga, Serie A na nyinginezo kijiji kipya kiitwacho Spoti na Starehe kimeanzishwa ili kukupa uhondo wa aina yake. Unaweza kukitembelea kwa kubonyeza hapa.Kazi kwenu.

Pichani ni kikosi cha kwanza cha Timu ya Soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ambacho jioni hii kimetupwa nje ya Mashindano ya kugombea Kombe la Challenge kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya kufungwa magoli 2-1 na Timu ya Taifa ya Sudan. Kili Stars imetolewa katika hatua ya robo fainali katika mashindano hayo yanayoendelea katika vituo vya Dar-es-salaam na Arusha.
Majina ya wachezaji hao wa Kilimanjaro Stars ambo wote kwa pamoja ni “celebrities” wakubwa katika michezo (soka) ni kama ifuatavyo. Walio mstari wa mbele toka kushoto, Dani Mrwanda,Amir Mafta,Ali Mustafa ‘Bartez’,Uhuru Suleiman na Nizar Khalfan.
Mstari wa nyuma toka Kulia-Salum Swedi, Shaban Nditi,Michael Chuma,Erasto Nyoni,Meshack Abel na Castory Mumbara.
Safari ya soka la bongo bado inaelekea kuwa ndefu.
Picha kwa hisani ya Issa Michuzi.

Ingawa watanzania wengi wanaendelea kuwa washabiki wa kutupwa wa timu mbalimbali zilizoko kwenye ligi kuu ya Uingereza(Premier League), nchini Tanzania msisimko fulani kwenye medani ya soka unarejea kwa kasi.
Siku hizi “utaifa” unaanza kurudi.Ukisikia Timu ya Taifa inacheza,basi kila mtanzania husubiria matokeo kwa hamu.Wapo wanaoenda viwanjani kuiunga mkono timu ya taifa na wapo wanaoishia mitaani kule vijiweni kwenye ule ubishi wa kufa mtu.
Msisimko huo mpya ndio unaomfanya Kocha wa Timu ya Soka ya Taifa,Taifa Stars,Mbrazili Marcio Maximo Barcellos(pichani) kuwa mmojawapo kati ya watu mashuhuri nchini Tanzania hivi sasa. Maximo ambaye aliwahi kuwa mmoja wa wakufunzi wa timu ya taifa ya Brazili kwa vijana chini ya miaka 17 na pia chini ya miaka 20, aliwahi pia kufundisha timu ya Livingston Football Club ya nchini Scotland (daraja la kwanza) katika msimu wa 2003/2004. Akiwa na timu hizo za vijana za Brazili aliwahi kuwafundisha wachezaji nyota wa Brazili wanaotamba hivi sasa kama Ronaldo (AC Milan) na Ronaldinho(Barcelona). Aliwahi pia kuwa mkufunzi huko Cayman Islands.
Kuhusu wapi atalipeleka soka la bongo ni suala la kusubiri na kuona. Pamoja na hayo wapo wanaosema,dalili njema zimeanza kuonekana na hivyo wanawasihi watanzania wampe muda.Unaweza pia kuitembelea tovuti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kujua mengi kuhusu soka la bongo kwa kubonyeza hapa.
Picha kwa hisani ya Mroki.

Hapo zamani kulikuwa na majina kama Athumani Mambosasa, Juma Pondamali,Joseph Fungo,Sahau Kambi, Iddi Pazi, Mohamed Mwameja na wengineo. Hao wote walikuwa ni walinda milango (makipa) waliojizolea sifa kemkem kutokana na umahiri wao katika kuzilinda nyavu zao zisitikiswe na timu pinzani.
Hivi sasa, huku watanzania wakiwa wamepata upya mwamko wa kupenda soka na kuunga mkono timu za nyumbani(hususani Taifa Stars), tunaye Tanzania One,Ivo Mapunda (pichani). Huyu ndiye kipa nambari moja wa timu ya taifa ya soka kwa upande wa wanaume,Taifa Stars na pia klabu maarufu na kongwe ya Yanga ya jijini Dar-es-salaam. Ameshatwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka nchini Tanzania mara mbili. Ushauri kwa Ivo Mapunda?
Kunako miaka ya 80 mpaka 90 ushindani wa soka nchini Tanzania ulikuwa ni wa aina yake. Ilikuwa ni kama kosa la jinai kusema wewe huna timu unayoishabikia baina ya mafahari wawili wa soka enzi hizo ; Simba na Yanga. Ilikuwa ni lazima uwe Simba au Yanga ! Kipindi cha michezo radio Tanzania cha saa mbili kasorobo usiku kilikuwa ni almasi.Hakuna anayetaka kukikosa !
Ni wakati huo huo ambapo kama ulikuwa huna fedha au muda wa kwenda uwanjani, hususani Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam, bado ulikuwa na nafasi ya kupata uhondo wa kinachoendelea taifa. Watangazaji wa Radio Tanzania walikuwa wanakupeleka « live » japo kimawazo tu uwanja wa taifa. Ulikuwa unapata msisimko wa kinachoendelea uwanjani kutokana na umahiri wa watangazaji wa mpira. Msisimko ulikuwa unazidi kutokana na vionjo na madoido ya watangazaji wenyewe. Kila kona ya nchi wapenzi wa soka ambao hawakuweza kufika Uwanja wa Taifa walikuwa wameketi chini, wameizunguka radio wakisikiliza mpira kwa makini kabisa.Ole wako upige kelele bila sababu.

Charles Hilary akiwa kazini
Mmojawapo kati ya watangazaji waliokuwa wakiturushia uhondo ule kiasi kwamba bila hata kutaja jina lake, kila mmoja aliweza kumtambua kwa sauti yake tu ni CHARLES MARTIN BARNABAS HILARY NKWANGA (pichani) ambaye wengi tunamjua tu kama Charles Hillary au « Mzee wa Macharanga ». Hivi karibuni tulifanya naye mahojiano motomoto kabisa. Hapa utapata historia nzuri ya maisha yake binafsi na yale ya utangazaji, mtizamo na ushauri wake kuhusu soka la Tanzania hivi sasa nk. Lakini pia utapata kujua ni kwanini mpaka hii leo bado tunamuita « Mzee wa Macharanga » ? Angepewa fursa ya kuwaalika wageni wanne kwa chakula cha jioni angewaalika kina nani ?Anakumbuka kitu gani kuhusu enzi zake za kutangaza soka Uwanja wa Taifa na mengineyo mengi.
Hivi sasa Charles Hilary anafanya kazi BBC London ambapo pamoja na shughuli zingine za utangazaji wapenzi wa ligi ya soka ya Uingereza (Premier League) na wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC London bado wanapata fursa ya kuendelea kufaidi umahiri wake katika fani ya utangazaji hususani wa soka. Unaweza pia kusikiliza Idhaa ya Kiswahili BBC mtandaoni kwa kubonyeza hapa. Mahojiano kamili haya hapa ; (more…)
Kwa mpenda soka ya Tanzania yeyote yule, hususani mnamo miaka ya themanini,jina Lawrence Mwalusako sio geni hata kidogo. Alikuwa sio tu kipenzi cha wapenda soka bali beki wa kutumainiwa wa timu zote alizowahi kuchezea, zikiwemo Waziri Mkuu Dodoma, Pan African, Yanga na timu ya taifa,Taifa Stars. Ndio maana yanapotajwa majina ya wachezaji soka nchini Tanzania waliowahi kuwika na jina la Mwalusako likakosekana,wadau wa soka,wanaoijua vyema historia ya soka la Tanzania,watakuambia wazi,something is missing.

Lawrence Mwalusako ni wa sita kutoka kushoto waliosimama.
Waliosimama kutoka kushoto: Marehemu Daktari wa timu Peter Manyika,Meneja John Manongi,Abeid Mziba “Tekero”,Athumani China,Yusuf Ismail Bana,Lawrence Mwalusako,Said Mrisho,Edgar Fongo,Isihaka Hasan,Golikipa Joseph Fungo,Kocha Mwinda Ramadhan.
Waliochuchumaa kutoka kushoto: Marehemu Lucias Mwanga,Rashid Idd Chama,Moshi Majungu,Allan Shomari,Ali Mchumila,Freddy Ferix Minziro,Abubakar Salum “Sure Boy”
Picha hii ilipigwa Mwaka 1987 uwanja wa taifa wakati wa mechi ya premier kati ya Yanga na Maji Maji.
Safari ya Mwalusako katika medani ya soka inaanzia kule Kyela mkoani Mbeya alipozaliwa mnamo mwaka 1960.Tulipofanya naye mahojiano hivi karibuni,Mwalusako ameongelea mambo mengi yakiwemo mtazamo wake wa soka la bongo hivi sasa,washambuliaji aliokuwa anawaheshimu,ushauri kwa wanasoka chipukizi nk.Pia anagusia jinsi “juju” ilivyo katika timu kubwa na pengine hata zile ndogo. Fuatana nasi katika mahojiano haya ambayo hata yeye mwenyewe anakiri,hajawahi kufanya na chombo chochote cha habari duniani akiwa kama mchezaji na hata baada ya kustaafu. Hivi sasa yeye ni Corporate Affairs Manager wa kampuni ya Sumaia Group Tanzania.Anaishi Dar-es-salaam.
BC: Unaweza kukumbuka wakati ulipokuwa mdogo ni nani alikuvutia katika mchezo wa soka? Kulikuwa na mtu yeyote maalumu ambaye ulimuona kama role model wako katika soka? (more…)

