MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Mara ya kwanza tuliwasiliana mwaka jana.Akanieleza mipango yake,ndoto zake na mikakati aliyonayo katika kutimiza ndoto zake.Kama ilivyokuwa kwa mamilioni ya watu ulimwenguni, Babu Sinare ambaye kisanii anajulikana kwa jina la Albino Fulani, alikerwa na kuhuzunishwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(albino) kwa imani za kishirikina. Kwake yeye,ilikuwa ni kama vile wametonesha kidonda ambacho alidhani kilishapona kwani Babu Sikare ni albino pia.

Miongoni mwa mipango yake ilikuwa ni pamoja na kuanzisha NGO yake ambayo italenga kusaidia albino wengine.Kupitia muziki wake,aliahidi kwamba atazidi kukemea mauaji ya albino.Hakuwa anatania.Alianzisha shirika lisilo la kiserikali na kuliita Afro-Bino. Matunda ya shirika hilo yameanza kuonekana.

Pichani juu ni Babu Sikare(kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Huduma za Hospitali kutoka Wizara ya Afya, Dr. Magreth Mhando (kulia) karatasi yenye maelekezo ya msaada wa mafuta ya kuzuia ngozi isiharibike na jua kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa ngozi Tanzania (Albino) yenye thamani ya dolla 1,500. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ustawi wa Jamii Bi. Magreth Njimba.

Kutoka moyoni,naomba kumpongeza Babu Sinare na shirika zima la Afro-Bino.We salute you and we support you.

Albino Fulani anatamba pia na wimbo wake Barua Kwa Mama.Bonyeza hapa kuusikia.


Sunday1BC

Nchi yetu imepitia katika awamu nne mpaka sasa katika siasa na uongozi. Kwanza ilikuwa enzi za Mwalimu Nyerere ambazo wengine hupenda kusema enzi za “mchonga”. Kisha ikaja awamu ya pili chini ya Mzee Mwinyi ambaye alikuja kujulikana sana kama “Mzee Ruhksa”. Kisha akaja Mheshimiwa Mkapa ambaye alipewa jina la “ukapa” kwani alipoingia madarakani, na shilingi ikapotea mifukoni mwa watu. Tupo katika enzi za JK. Bado sijajua akimaliza muda wake zitaitwaje enzi zake.Tusubiri.

Wakati sote tunakubaliana kwamba awamu zote ni muhimu kwa maendeleo kamili ya nchi,bila shaka tunakubaliana pia kwamba awamu ya pili,ya Mzee Mwinyi,ilifungua milango mingi sana. Hapo ndipo vitu kama vituo vya televisheni,vituo vya redio vya FM,biashara za nje na ndani,zilikuja kwa kasi.Enzi za mageuzi.

Kufunguka kwa milango hiyo kulitoa pia nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao ambavyo hapo nyuma vilikuwa vimejificha bila sehemu ya kufichuliwa. Tukaanza kupata vijana watangazaji.Tukapata vijana wenye vipaji vya kisanii kama vile tunaouita “muziki wa kizazi kipya” hivi sasa. Tukapata wazalishaji muziki (producers). Watangazaji wapya wakaambatana na wale “wakongwe” kutoka vituo kama Radio Tanzania na kutupatia ufanisi na ushindani katika masuala ya utangazaji ambao haukuwepo kabla ya hapo.

Miongoni mwa vijana waliopata fursa ya kuingia katika fani na kuonyesha vipaji vyao ni Sunday Simba Shomari.(pichani). Ghafla maisha yakabadilika,enzi za AM zikazibwa na FM.Soko la muziki wa kizazi kipya likaanza kukua. Majumba ya sinema yakatoweka.Hakuna wateja. Kila mtu yupo nyumbani akikodolea macho luninga yake. Kama kwenu hakuna TV basi unajongea kwa jirani. Muziki wa kimataifa,soka la kimataifa yakiwemo kama mashindano ya kombe la dunia yakawa ni mambo ya kawaida.

Nini kiliwasukuma vijana kama Sunday Shomari kuingia katika fani ya utangazaji wa radio na televisheni? Ilikuwaje enzi hizo ukizingatia kwamba wengi wao walikuwa hawana uzoefu katika masuala hayo? Na je anazungumziaje safari yake kutoka Radio One/ITV mpaka Voice of America alipo hivi sasa? Nilimtafuta Sunday na kufanya naye mahojiano yafuatayo;

BC: Sunday karibu sana ndani ya BC.Tunafurahi kuwa nawe hapa.Mambo yanakwendaje?

SS: Mambo safi tunamshukuru Mungu.

BC: Labda bila kupoteza muda,kwa faida ya wale ambao wanakufahamu kwa sura na jina tu,unaweza kutupatia japo kwa kifupi tu historia ya maisha yako?

SS: Mimi ni mzaliwa wa Dar-es-salaam na mwenyeji wa Tanga. Nimepata elimu ya msingi Arusha School na Muhimbili. Elimu ya sekondari Forodhani na Al-Muntazir.Halafu nimefanya kazi na Dr.Jane Goodall Institute kabla ya kujiunga na ITV na Radio One. Baadaye nikajiunga na Chuo Cha Uandishi wa Habari (TSJ) kwa kozi fupi ya uandishi. Kisha nilikuja hapa Marekani kwa kozi nyingine fupi ya uandishi wa TV kabla ya kurudi tena Tanzania na kuendelea na masomo yangu ya juu ya uandishi hapo TSJ.

Wakati huo huo nikiendelea na kazi hatimaye nilitoka kwenye uandishi nikaingia Shirika la Ndege la Alliance kabla ya kuja tena Marekani kujiendeleza kielimu na kutafuta maisha mengine. Na hivi sasa naendelea na shahada ya mawasiliano katika Chuo Kikuu Cha Maryland.

BC: Ilikuwaje ukaingia kwenye fani ya utangazaji? Nini kilikushawishi au nani alikuvutia katika fani ya utangazaji? (more…)

Sheikh Yahya

MTABIRI maarufu wa Afrika Mashariki, Shehe Yahya Hussein ametabiri kuwa Rais Jakaya Kikwete atashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao na atakayempinga ndani ya chama chake atakufa ghafla.

Sambamba na hilo, atakayeonekana kumshinda nje ya chama chake pia atapoteza maisha vivyo hivyo.

Akitoa utabiri wake jana Dar es Salaam, juu ya uchaguzi mkuu mwakani, Shehe Yahya alisema ushindi wa Rais Kikwete unatokana kurithishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995 ilipodaiwa kuwa Rais Kikwete alishinda kwenye kura za maoni lakini akamsihi amwachie Benjamin Mkapa.Kwa undani wa habari hii bonyeza hapa.

Je huu unaweza kuuita “utabiri” au ni…Unakubaliana naye ?Kwanini ?

Pichani juu ni Sheikh Yahya akiwa nyumbani kwake mapema mwaka huu.Ubavuni mwake ni mkewe Bi.Fetty

eduKwa muda mrefu Tanzania tumekuwa na tatizo la kukosa waandishi wa vitabu. Waliotakiwa kuandika wamekuwa wakilalama kwamba hata wakiandika hakuna wasomaji achilia mbali wanunuaji wa vitabu. Bila shaka aliyetoa “utani wa ukweli” kwamba ukitaka kuficha kitu na mtu mweusi asikione,basi kifiche kwenye kitabu,alikuwa ameiangalia Tanzania pia.

Tatizo hilo linaelekea kupata ufumbuzi. Pengine inatokana na mabadiliko ya kidunia ya sayansi,tekinolojia  na mawasiliano au ni wakati tu umefika wa Tanzania nayo kuzinduka na kuamua kuingia kwenye ramani ya watunzi na wasomaji wa vitabu.

Hivi karibuni,aliyewahi kuwa Gavana wa kwanza wa  Benki Kuu nchini Tanzania,Edwin Mtei, ameandika kitabu. Kitabu kinaitwa From Goatherd to Governor ambacho kwa tafsiri ya moja kwa moja ya Kiswahili ni Kutoka Mchunga Mbuzi mpaka kuwa Gavana. Ni kitabu kuhusu maisha yake kikiwa na mengi kuhusu uhusiano wake na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye kama wengi tunavyojua,hawakuelewana katika mambo mbalimbali ya sera za kiuchumi.Ukitaka kukinunua kitabu cha Edwin Mtei bonyeza hapa.

governor

Mbali ya Edwin Mtei, aliyewahi kuwa Miss Tanzania 1999,Hoyce Temu naye ametoa kitabu chake.Kinaitwa Nayakumbuka Yote.Mbali ya kuongelea kuhusu maisha yake,kitabu cha Hoyce ni muongozo mzuri kwa wasichana ambao wanataka kuingia au tayari wamo katika sanaa ya mitindo na urembo.Kinacho kipengele cha “Maswali na Majibu” kuhusu sanaa ya urembo.Kukipata kitabu hiki bonyeza hapa.

hoycetHoyce Temu wakati wa uzinduzi wa “Nayakumbuka Yote”

Huu ni mfano na muelekeo mzuri kwa nchi yetu na kwa wapenzi wa kujisomea. Bila shaka hatutaishia kwa Mtei na Temu bali katika siku za karibuni tutaona  wengine wakijitokeza na kuandika. Utamaduni huu ni miongoni mwa tamaduni ambazo mimi binafsi naona zinafaa kuiga.Wenzetu ni mabingwa wa kuandika na kujisomea.Hongera Mtei.Hongera Hoyce.

Vitabu vyote vimetolewa chini ya usimamizi wa kampuni ya Mkuki na Nyota.

master-t3bcKwa mtu yeyote ambaye anapenda fani ya utangazaji au mtu yeyote ambaye ni msikilizaji wa radio,hakuna shaka kabisa kwamba jina la Master T sio geni. Lakini Master T sio jina lake halisi. Jina alilopewa na wazazi wake ni Taji Liundi.

Yeye ni miongoni mwa watangazaji na waongoza shughuli(MCs) ambao wamejijengea jina ,kujikusanyia idadi kubwa ya mashabiki na kujijengea heshima ya aina yake katika fani hiyo maarufu. Wiki chache zijazo ndiye atakayekuwa jukwaani kusimamia shughuli nzito ya kumtafuta mrembo mpya wa Tanzania(Miss Tanzania 2009).Atashirikiana na Nancy Sumari(Miss World Africa,2005) katika zoezi hilo.

Ukimsikiliza iwe ni redioni au akiwa msimamizi wa shughuli fulani utafurahi,utajifunza,utaburudika na kisha bila shaka utakubali kwamba jamaa ana kipaji,anaipenda kazi yake,anakuthamini wewe kama binadamu na anakupenda kama msikilizaji wake. Umakini anaouweka katika kazi yake yaweza kuwa ndio siri ya mafanikio yake.

Yeye ni miongoni mwa wale watangazaji ambao licha ya kujaaliwa kuwa na sauti inayofaa kabisa kwa masuala ya utangazaji,pia ni wenye kipaji kikubwa katika masuala ya lugha.Master T anaimudu vyema lugha ya Kiswahili na pia anakipambanua vyema Kiingereza na pia huwezi kumuweka mbali na Kifaransa.Hii inamfanya akamilishe ile preamble inayosema;ukitaka kuwa mtangazaji mzuri,sharti ujitahidi sana katika masuala ya lugha.

Hivi karibuni nilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ambayo utayasoma hivi punde.Katika ufupi na ufasaha wa aina yake,Master T anaweka wazi masuala mbalimbali muhimu kuhusu historia ya maisha yake,heka heka za utotoni,kazi yake kama mtangazaji,harakati zake katika mwanaharakati dhidi ya ugonjwa hatari wa ukimwi,maoni yake kwa vijana na mengineyo mengi.

Je, unajua ni mkasa gani mkubwa wa kimaisha uliowahi kumkumba Master T? Unajua wazazi wake walitaka awe nani,afanye kazi gani badala ya utangazaji?Nini mtazamo wake kuhusiana na mapambano dhidi ya gonjwa la ukimwi?Fuatana nami katika mahojiano yafuatayo na Master T;

BC: Taji,kwanza kabisa asante kwa kukubali ombi langu la kufanya nawe mahojiano haya.Pole na majukumu.Mambo yanakwendaje?

MASTER T: Vyema Kaka, nami nashukuru kwa fursa hii.

BC: Natambua kwamba wengi wana ufahamu mkubwa kuhusu historia binafsi ya maisha yako.Lakini kwa faida ya wale ambao hawana habari,unaweza kuniambia kwa kifupi tu kuhusu maisha yako ya awali;ulizaliwa wapi,ukakulia wapi,ukasoma wapi na mambo kama hayo?

MASTER T: Nimezaliwa Dar, nilisoma shule ya Msingi Kisarawe pale Kariakoo kwa muda mfupi. Nikaelekea Uswiss (Switzerland) mwisho wa miaka ya 70′ ambapo niliendelea na shule ya msingi nikijifunza Kiingereza na Kifaransa. Tukahamia Zambia na dingi, nikamalizia darasa la saba.

Ikafuata Zimbabwe niliposoma form 1-2, nikaomba kurudi Bongo, nikapangiwa Ilboru Arusha, nikapiga mpaka form 3-6, nikafurahia mafunzo ya Oljoro JKT halafu Chuo cha Diplomasia mapema miaka ya 90′. (more…)

kj

Kila siku ya Jumanne(kama leo hivi) watanzania siku hizi hupata nafasi ya kujiongezea maarifa mbalimbali,kuburudika,kujielimisha na kujifahamisha kupitia gazeti la Kwanza Jamii kama linavyoonekana katika picha ya hapo juu.Hiyo ni taswira halisi ya gazeti la wiki hii ambalo limeshatinga mitaani.

Humo ndani utakuta makala mbalimbali kutoka kwa waandishi mbalimbali nikiwemo mimi,Jeff Msangi. Wengine ni  kama vile Maggid Mjengwa, Freddy Macha, BAP (Born Again Pagan), Subi Sabato,Prof.Joseph Mbele, Dr.Bukaza Chachage, Joseph Mihangwa, Padri Privatus Karugendo, Eliamani Laltaika bila kusahau kona ya Aunt Subira na wengine wengi.

Lakini kama uko mbali na Tanzania au kwa sababu moja au nyingine huwezi kupata kopi halisi ya Kwanza Jamii, habari nzuri ni kwamba unaweza kuperuzi habari mbalimbali kupitia mtandaoni. Bonyeza hapa.

mjengwa-jamiibc

Maggid Mjengwa sio jina geni.Bila shaka kabisa umewahi kumsikia,kumsoma na pengine hata kutembelea blog yake ambayo kimsingi ni kimbilio la yeyote yule anayependa kupata picha halisi ya maisha ya mtanzania wa kawaida hususani yule anayeishi kijijini kama ilivyo kwa babu na bibi yangu.Wasomaji,watembeleaji na wachangiaji wa blog yake wanapenda kumuita “Mwenyekiti”.

Yeye ni miongoni mwa waandishi wa makala zenye kuchoma kama sio kugusa hisia za wengi.Ukitaka kujua historia yake ya uandishi unaweza kuipata kwa kusoma mahojiano tuliyowahi kufanya naye siku za nyuma kwa kubonyeza hapa.

Maggid ni mpenzi wa michezo hususani wa soka.Ni mnazi wa Simba.Ni upenzi huo wa soka na michezo kwa ujumla ambao ulimfanya aanzishe gazeti lililoitwa “Gozi Spoti” ambalo lilidumu mitaani mpaka hivi karibuni alipoamua kulisitisha.

Jambo jema ni kwamba, kuondoka kwa “Gozi Spoti” kulifanyika kwa makusudi ili kulipisha gazeti jipya litakalojulikana kama Kwanza Jamii ambalo litaingia mitaani siku si nyingi chini ya usimamizi wa Ikolo Investment Ltd kampuni iliyo chini ya mwenyewe “Mwenyekiti”.Kwa hiyo tunaweza kabisa kuongeza cheo kimoja kwa “Mwenyekiti” na kumuita Mjasiriamali.

Kwanza Jamii ni jarida la uchambuzi wa masuala yanayohusu na kuigusa jamii.Haya ni pamoja na siasa,uchumi,elimu,michezo na utamaduni.Pia yatakuwemo masuala ya mazingira,jinsia na ukimwi . Ni jarida litakalokuwa linatoka kila siku ya Jumanne.

Tumepata nafasi ya kufanya mahojiano mafupi na ‘Mwenyekiti” kuhusiana na ujio wa jarida hili na pia kumdadisi kuhusu anachokiona kila atembeleapo vijiji na vijiji vya Tanzania.Anaona nini?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; (more…)

kawawa3

Hivi majuzi,Mzee wetu, Rashid Mfaume Kawawa, alizindua kitabu kinachoelezea maisha yake.Kitabu hicho ambacho kimeandikwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Chuo Cha Mwalimu Nyerere Cha Kivukoni,Prof.John Magoti,kimepewa jina la Kawawa.Uzinduzi huo ulifanyikia Ikulu jijini Dar-es-salaam.

Ingawa tunaweza kusema imemchukua muda mrefu sana Mzee Kawawa kuandika kitabu chake,ni lazima tumpongeze sana kwa uamuzi wake huo ambao sio tu wa busara bali pia ni mfano wa kuigwa.

Tulipofanya mahojiano na Mheshimiwa Zitto Kabwe mwaka juzi,tuliliongelea suala la kuandika vitabu na kujisomea.Mh.Kabwe alionekana kukerwa na tabia ya viongozi wetu(na hata sisi wananchi wa kawaida) kutopenda kusoma achilia mbali kuandika! Ni utamaduni ambao tupende tusipende hatuna budi kuiga.

Uandishi ukisindikizwa na usomaji ni msingi mzuri wa maendeleo.Wenzetu katika nchi zilizoendelea ni mabingwa wa kujisomea.Miji ya wenzetu imezungukwa na maktaba. Ukiingia kwenye ndege,treni au basi sio ajabu kukuta watu kadhaa wakijisomea vitabu,magazeti nk.Kwanini wanapenda kusoma?Jibu ni rahisi;wanapenda kuongeza ujuzi,kujielimisha na hivyo kuendelea kuwa mbele katika suala zima la maendeleo.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria uzinduzi wa kitabu cha Kawawa ni pamoja na maraisi wastaafu Ally Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa. Swali ambalo lilibakia kichwani kwangu ni kwamba viko wapi vitabu vyao? Ni lini tutasoma kitabu cha Mwinyi,Mkapa,Warioba au hata Edward Lowassa na wengineo?

Ni matumaini yetu kwamba Kawawa amefungua tu njia na kwamba wengine watafuata.Hongera sana Mzee Kawawa.

Pichani ni Mzee Kawawa na Rais Kikwete wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.Kwa nyuma unaweza kumuona Rais Mstaafu B.W.Mkapa.Picha kwa hisani ya Ikulu.

shivjibc

Ni wazi kwamba tukiuliza swali kwamba kwanini Tanzania bado ni nchi ambayo,pamoja na rasilimali zote ilizonazo,bado haijaweza kupata maendeleo ya kiuchumi inayostahili,majibu yatakuwa ni mengi na pengine yanayotofautiana sana.Pamoja na tofauti ambazo zinaweza kujitokeza tunapojadiliana, mijadala ya namna hiyo ni muhimu kufanyika kwani inatupa mwanga wa nini pengine kifanyike ili tusije warithisha wanetu nchi ambayo hata wakitaka kuiuza,wasipate mnunuzi.

Miongoni mwa watu ambao wanatarajiwa kuchochea mijadala kama hiyo ni pamoja na wasomi mbalimbali tulionao.Haishangazi basi kusikia kwamba leo Prof.Issa Shivji(pichani) anatarajiwa kuzindua kitabu kinachoainisha mambo mbalimbali yanayosababisha nchi yetu kutopata maendeleo makubwa ya kiuchumi tangu tupate uhuru miaka arobaini na ushee iliyopita.Kwa habari zaidi bonyeza hapa.

mengi

Miongoni mwa habari za watu maarufu ambazo bila shaka zimegubika vichwa vya wengi wiki hii ni ile ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP,Reginald Mengi kukanusha taarifa za gazeti moja kwamba amefunga ndoa mpya na mwanamke mmoja wa jijini Dar-es-salaam(Lilian Kimaro) na kulaumu uandishi wa habari unaokwenda kinyume na misingi ya taaluma hiyo.Kwa habari zaidi unaweza kubonyeza hapa.

Pia unaweza kubonyeza hapa ili kuona baadhi ya maswali ambayo waandishi wa habari walimbana nayo Mengi lakini akakwepa kwa kigezo kwamba wakatafute wenyewe ukweli!

Photo/Venance Nestory

Read the Next Page →

↑ Go Back to Top of Page