jeffbcNaweza kusema nimeshazoea kuhoji wenzangu.Kuhoji watu ambao ndio chachu hasa ya BC bila kusahau msomaji ambaye ni wewe.Kumbe wakati nawawinda watu wa kufanya nao mahojiano,wapo wenzangu(wenzangu katika habari na mawasiliano) ambao pia huniangazia macho ili kufanya nami mahojiano.

Naomba nikiri kwamba hiyo hutokea mara chache.Naweza kukumbuka vizuri kabisa idadi ya mahojiano rasmi ambayo nimeshawahi kuyafanya.Sio kwamba sioni thamani ya mahojiano,la!Ni kwamba hupendelea tu kuwa upande mwingine wa kamera.Usinihoji sana kwanini kwa sababu sidhani kama nina jibu moja.Tutakesha.

Hivi karibuni Freddy Macha alifanya nami mahojiano ambayo yalichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa bahati nzuri nilishawahi kufanya mahojiano na Freddy Macha kuhusu kazi zake za uandishi,muziki na historia nzima ya maisha yake.Unaweza kusoma mahojiano yangu kwenda kwake kwa kubonyeza hapa na hapa.Kwa hiyo haikuwa kazi nzito sana aliponieleza nia yake ya kufanya nami mahojiano.Freddy ni mtu mcheshi,muungwana na mvumilivu.

Ni mahojiano mafupi lakini muhimu kiasi kwani unaweza kujua kile ninachokiwaza ninapokuwa nawaza na pia ninachofikiri kuhusu suala zima la blogs na maendeleo ya ulimwengu wa habari na mawasiliano ambapo siku hizi wewe msomaji na mchangiaji ndiye mshika tochi wa habari.Unaweza kuyasoma mahojiano hayo kwa kubonyeza hapa.

Kama wewe ni msomaji mzuri wa magazeti na majarida mbalimbali kutoka Tanzania,basi sina shaka kabisa kwamba jina Maggid Mjengwa (pichani) litakuwa sio geni kwako! Makala zake za kusisimua,kuchokoza hisia na kujenga hoja za nguvu ni miongoni mwa vivutio muhimu vya wasomaji wa magazeti ndani na nje ya Tanzania. Leo hii tunaweza kabisa kuthubutu kusema kwamba Maggid ni miongoni mwa wanahabari bora tulionao kwani hana uoga wowote pale anapokuwa anaandika au kuongelea jambo ambalo analiamini kwa dhati.

Lakini Maggid,kama ambavyo pengine unafahamu tayari, haishii magazetini tu bali pia ni blogger maarufu hivi sasa. Blog yake ya picha ambayo mwenyewe anaiita “kijiji” na hivyo wasomaji wake na watembeleaji wake “wanakijiji”, imejipatia umaarufu sana kwa kuonyesha au kwenda kule ambapo ndiko kunahesabika kuwa kwenye hali halisi ya maisha ya mtanzania. Ukiitembelea na kuisoma blog yake vizuri kwa kutizama picha lukuki zinazoipamba blog yake,utaweza kuwa jaji mzuri kama “bongo ni tambarare” au bado zile ahadi za uchaguzi uliopita ni mbwembwe za kisiasa tu.Mwenyewe anasema blog yake ni kimbilio na sauti kwa wale ambao kila mara huwa wanasahauliwa!

Maggid pia ni mjasiriamali.Yeye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ijulikanayo kama Ikolo Investment Co ambao ndio wachapishaji wa Gozi Spoti; jarida la michezo, sanaa, maisha na burudani linalotoka kila Jumatano. Maggid pia ni mwanamichezo,mpenda michezo na shabiki mkubwa wa soka.

Hivi karibuni,baada ya kumsaka kwa muda mrefu kutokana na ratiba zake za kazi kumbana,tulifanikiwa kupata fursa ya kufanya naye mahojiano utakayoyasoma hivi punde.Kama ambavyo ungetegemea,Maggid anatoa “darasa” katika mahojiano haya.Mbali ya kukupa historia ya maisha yake kwa undani,Maggid anakumbusha vipengele fulani fulani vya historia ya nchi yetu ambavyo ni muhimu. Lakini kwa mapana, anaongelea kuhusu suala la uandishi na pia blog yake bila kusahau changamoto ambazo nchi yetu inakabiliwa nazo hivi leo katika nyanja mbalimbali. Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; read more

Binti aliye pichani hapo juu anaitwa Megan Fox.Kwa mapana na marefu sio bongo celebrity.Yawezekana kabisa kwamba hata Bongo hajawahi kuisikia!

Kwanini basi tumemuweka hapa leo? Sababu ni kwamba binti huyu ndiye ambaye kwa mwaka huu wa 2008, jarida maarufu la FMH, lilimtaja kama mwanamke nambari wani mwenye mvuto zaidi miongoni mwa wanawake 100 iliyowaorodhesha kama wanawake wenye mvuto zaidi duniani.

Kwa bahati nzuri au mbaya,vyombo vya habari kama hivi vikishirikiana na vitu kama filamu,muziki nk ndivyo ambavyo hivi leo vina ushawishi mkubwa kuhusiana na suala zima la uzuri,urembo au mvuto.Vikisema fulani ndio mwenye mvuto zaidi basi mabilioni ya watu wanaamini hivyo.Matokeo yake ndio watu wengi(hususani wanawake) huanza safari ndefu ya kujinyima chakula ili wapunguze saizi za miili yao na kufanana na huyo aonekanaye “mzuri” kwa mujibu wa jarida fulani.Wengine hufanya kila wawezalo ili wawe na nywele,rangi ya mwili,kucha nk kama za huyo aonekanaye “mzuri” nk.Kwa bahati mbaya hata mengi ya majarida yaliyopo au yanayoanzishwa nchini Tanzania,yanafuata mkondo huo huo wa “kutafsiri” urembo,uzuri na mvuto.

Je urembo,uzuri,mvuto ni vitu gani?Ni kweli kwamba uzuri au urembo uko katika mboni ya jicho la mtazamaji au kutoka katika akili na macho ya mhariri wa jarida?Nini kifanyike ili kumfanya kila mtu aridhike na jinsi alivyo ili kupunguza mahangaiko,watu kupoteza maisha wakati wa zoezi la kujikondesha nk?

 

Kwa miaka nenda rudi, tangu miaka ya sabini,jina la Freddy Macha (pichani) limekuwa sio geni miongoni mwa wasomaji mbalimbali wa magazeti, vitabu vya hadithi fupifupi,wapenzi wa muziki na pia sanaa ya ushairi nchini Tanzania. Iwe unamfahamu Freddy kupitia muziki wake,makala zake au mashairi yake, utakubaliana nasi kwamba Freddy ni mojawapo ya hazina tulizonazo linapokuja suala zima la usanii. Wengi miongoni mwa wasomaji wa makala zake katika magazeti ya The Guardian na Mwananchi nchini Tanzania, wanakiri kwamba makala za Freddy huwa ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wakati mwingine wadamke asubuhi na mapema ili mradi tu wasikose nakala za magazeti hayo hususani siku zinazochapishwa makala zake.

Wapenzi wengi wa muziki,ushairi, tamthiliya na ngoma mtakuwa mnamkumbuka Freddy Macha tangu alipokuwa na kundi la Sayari. Kundi hilo ambalo lilitamba sana mwanzoni mwa miaka ya themanini, ni mojawapo ya vikundi vichache vya sanaa nchini Tanzania vilivyopata mafanikio sio tu nchini Tanzania bali pia katika medani za kimataifa. Sayari liliwahi kufanya ziara kadhaa za kimaonyesho katika nchi mbalimbali za nje hususani za Ulaya enzi hizo.

Kwa upande wa uandishi,Freddy Macha alianza kunoa kalamu katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo na baadaye kuwa mwanasafu(columnist) wa gazeti la kila jumapili la Sunday News hadi mwaka 1984.Freddy amewahi kushinda tuzo kadhaa za uandishi ikiwemo ile ya Ushairi ya BBC mwaka 1981 na hadithi fupi fupi ya Jumuiya ya Madola( Commonwealth of Nations) ya mwaka 1996.

Hivi karibuni, baada ya kumsaka kwa muda mrefu, tulipata nafasi ya kufanya mahojiano ya kina na mwandishi/mwanamuziki/mwalimu huyu ambaye hivi sasa anaishi London nchini Uingereza. Sasa kutokana na ukweli kwamba Freddy ni mmojawapo miongoni mwa wale watu ambao tunaweza kuwaitwa “wenye vipaji vingi”,tumeamua kuyagawa mahojiano yetu naye katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza, ambayo ndiyo hii unayoisoma leo, tumeongea naye zaidi kuhusu kazi zake za uandishi.Sehemu ya pili ambayo itawajieni baadaye kidogo,tuliongea naye kuhusu muziki,jamii na mengineyo kadha wa kadha.

Unataka kujua Freddy ametokea wapi?Amepitia mambo gani mpaka kufikia hapo alipo? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uandishi wa leo akilinganisha na ule wa zamani? Kwanini kitabu chake cha hivi karibuni amekiita Mpe Maneno Yake? Unafahamu kwamba Freddy aliwahi “kuzamia meli”?Ilikuwaje? Anasemaje kuhusu dhana za mawasiliano kama blogs? Kwa hayo na mengineyo mengi, fuatana nasi katika sehemu hii ya kwanza ya mahojiano yetu naye; read more

 

Ni vigumu, nasema ni vigumu.Haiwezekani.Huwezi kuizungumzia fani ya uandishi wa fasihi (literature) nchini Tanzania na usimzungumzie Shafi Adam Shafi(pichani) na bado ukaeleweka unazungumzia nini. Huyu si tu mwandishi, bali hazina ya historia ya nchi yetu, mila na tamaduni zetu, uandishi wa riwaya uliobobea. Ingawa kitabu chake cha KULI ndicho ambacho wengi wanakitambua zaidi( ni mojawapo ya vitabu vinavyofundishiwa mashuleni kwenye somo la Kiswahili), Shafi anavyo vitabu vingine kama vile Kasri ya Mwinyi Fuad (ambacho kimetafsiriwa kwa Kifaransa, Kijerumani na Kirusi); Vuta n’kuvute (ambacho kilimpatia tuzo ya mwandishi bora nchini Tanzania mwaka 1998) na Haini ambacho ni cha hivi karibuni zaidi. Vitabu vyote vya Shafi ni riwaya.

Hivi majuzi alikutana na mwandishi mwingine mahiri, Freddy Macha, huko Milton Keynes nchini Uingereza. Waliketi kitako kwa zaidi ya masaa manne.Waliteta,wakazoza,wakapeana historia,wakapashana habari.Wakachambua umuhimu wa waandishi na wasanii. Lakini kabla hatujakuambia pa kwenda ili usome alichoandika Freddy Macha kuhusu “mkutano” wao, hii hapa historia fupi ya gwiji huyu wa fasihi.

Adam Shafi alizaliwa mjini Zanzibar mwaka 1940. Baada ya elimu yake ya shule ya msingi alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Seyyid Khalifa (sasa Chuo cha Ualimu cha Nkrumah) mwaka 1957 hadi mwaka 1960. Alipata Diploma juu katika fani ya Siasa ya Uchumi katika Chuo cha Fritz Heckert, katika iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani mwaka 1963. Alipata mafunzo ya uandishi wa habari mjini Prague, nchini Czechoslovakia (sasa Jamhuri ya Czech) mwaka 1964 hadi mwaka 1965, nchini Sweden mwaka 1982 na nchini Marekani mwaka 1983.

Adam Shafi alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) kuanzia 1998 hadi 2002. Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) mwaka 2002.

Haya twende sasa.Bonyeza hapa ili usome alichokiandika Freddy Macha kuhusiana na mkutano wake na Shafi Adam Shafi. Mahojiano yetu na Freddy Macha mwenyewe yatawajieni hivi karibuni.Hutaki kuyakosa mahojiano hayo!

Picha kwa hisani ya Freddy Macha.

Historia ya Shafi kwa msaada wa Longhorn Publishers.

Sekta ya burudani nchini Tanzania imekuwa ikipitia mabadiliko mwaka hadi mwaka,siku hadi siku. Kuna wakati burudani ya disko ndio ilishika hatamu.Hii ilienda sambamba na sinema,zile za yale majumba ya sinema ya enzi zile.Hapa nazungumzia kina Drive Inn Cinema,New Chox,Empress na wenzao. Kisha kuna wakati taarabu ikaja juu.Ukawa ni mwendo wa “mipasho”.Kina Nasma na Bi.Khadija wakawa ndio gumzo la mjini. Haukupita muda muziki wa kizazi kipya ukashika hatamu.Bongo Flava ikawa ndio ya kuamkia na ndio ya kulalia.

 

 

Lakini kabla Bongo Fleva haijapotea (bado inatamba) enzi za filamu za kitanzania,zenye lugha yetu wenyewe,waigizaji wetu wenyewe,zikarejea upya. Hivi sasa Bongo Fleva na Filamu za Kitanzania zinabakia kuwa burudani za aina yake nchini Tanzania. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba filamu za kitanzania zina historia ndefu.Tangu enzi zile za kina Fimbo ya Mnyonge,YombaYomba,Harusi ya Mariam nk. Kinachofanyika hivi sasa ni kurejesha enzi zile.

 

Mtu mmoja ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa kuzirudisha zama zile za filamu za kitanzania ni Sultan Tamba ambaye ni mtunzi wa hadithi,mwandishi wa magazetini na vitabuni na pia muongoza filamu. Filamu yake ya iliyoitwa Girlfriend ya mwaka 2002 ambayo aliwashirikisha wasanii kama T.I.D, kundi la East Coast na baadhi ya wacheza filamu walio maarufu sasa kama Monalisa na wengineo, ilichangia sana kuamsha upya ari ya kutengeneza tena filamu za kitanzania.Wakati huo filamu za kutoka nchini Nigeria zilikuwa zishaanza kuotesha mizizi miongoni mwa wapenda filamu nchini Tanzania.Mpaka hivi leo bado zinapendwa nchini Tanzania ingawa hivi sasa zinakumbana na ushindani mpya wa filamu za kitanzania.

 

Hivi karibuni tulifanya naye mahojiano na Sultan Tamba ambapo tumezungumzia mambo mengi kuhusiana na kazi zake za uandishi,utunzi wa hadithi za filamu,uongozaji filamu na mengineyo.

 

Muhimu zaidi alitueleza juu ya ujio wa filamu yake mpya ambayo ameiita Soka la Bongo.Filamu hiyo inatarajiwa kutoka takribani wiki tatu zijazo.Inahusu nini?Kwanini ameiita Soka la Bongo? Unawajua top six wake kwa upande wa waigizaji filamu nchini Tanzania?Ana maoni gani kuhusu wanamuziki kugeuka kuwa waigizaji? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania? Upo? Unajua ameanza kuandika tangu akiwa na umri gani? Kwa hayo na mengineyo mengi fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; read more

 

Jarida maarufu la Kitangoma kwa mwezi wa Oktoba-Novemba limeshaingia mitaani. Richa Adhia , Miss Tanzania 2007 ndiye anayepamba ukurasa wa mbele huku swali likiwa kama linavyoonekana hapo juu.

↑ Go Back to Top of Page