
Ukimuita celebrity, Bob Sankofa atatabasamu tu kama sio kuangua kicheko kabisa.Haamini sana kwenye suala zima la u-celebrity.Anaamini zaidi kwenye kazi na kufanya kile mtu unachokipenda kutoka moyoni. Pamoja na kukataa kwake kuvishwa kofia ya aina yoyote ya u-celebrity, kama wewe ni mfuatiliaji wa maendeleo ya watanzania mtandaoni na mpenzi wa kuona au kutizama picha, basi jina la Bob Sankofa litakuwa sio geni. Huyu ndiye mmiliki wa ile blog makini ya picha iitwayo Mwenye Macho au kwa kifupi MM.
Jina Bob Sankofa sio jina lake halisi lakini ndio jina ambalo siku hizi limemkaa zaidi. Jina lake halisi ni Philemon Msangi. Yeye ni mwanafotografia, mtengeneza filamu, mjasiriamali na zaidi ya yote ni mwanablogu.Siku chache tu baada ya Zimbabwe kupata uhuru wake,Bob alizaliwa.Usihangaike kupiga hesabu,alizaliwa 29/04/1980.
Ingawa blog yake iliyosheheni mapicha hajaifunga(anadai lazima iendelee kuwepo) hivi karibuni Bob amekuja na kitu kinachoitwa FotoBaraza. Kumbuka Bob ni mpenzi wa kutupwa wa sanaa ya picha.Akiona picha nzuri, anaweza kuitizama mpaka macho yaanze kumuuma ndio atashtuka na kuendelea na shughuli zake zingine.
Bob anasema FotoBaraza ni aina mpya ya mtandao.Ni vuguvugu jipya.Ni mahali pengine ambapo wanajamii wanakutana na kupasua hoja mbalimbali, kutizama na kuweka picha, kupiga soga, kuzungumza Kiswahili na zaidi kuunganishwa na wanajamii wengine kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.Jamii inaunganishwa na FotoBaraza.Kwa kuzingatia jinsi ambavyo upigaji picha siku hizi umetawala(hususani tangu ziingie simu za viganjani zenye kamera), Bob anasema FotoBaraza ni kitu muafaka kabisa katika wakati unaostahili.
Basi tusiseme mengi sana.Kwanini usitembelee FotoBaraza na kujionea mwenyewe na pia kujiunga na wanajamii wenzako? BC inatoa hongera kwa ubunifu wa namna hii. Bonyeza hapa utembelee FotoBaraza.

Kampuni ya Global Publishers imetimiza miaka kumi sasa tangu kuanzishwa kwake. Sherehe maalum za kusheherekea tukio hilo zilifanyika hivi majuzi ndani ya ukumbi wa NSSF WaterFront jijini Dar-es-salaam.Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nishati na Madini,Mheshimiwa William Ngeleja. Global Publishers ndio wachapaji wa magazeti ya Uwazi,Ijumaa,Champion,Bongo Sun,Amani na Risasi.
Pichani kutoka kushoto ni Meneja Mkuu wa kampuni hiyo,Abdallah Mrisho, Katibu Muhtasi wa kampuni hiyo Bi.Leila Bhanji na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo,Eric Shigongo.
BC inawapongeza Global Publishers na kuwatakia kila la kheri katika kazi zao.Kwa habari na picha zaidi juu ya sherehe hizo ambazo pia zilihudhuriwa na viongozi wa vyama na serikali na celebrities kibao wa bongo tafadhali tembelea tovuti yao kwa kubonyeza hapa.

Yapo mambo ya kitaifa ambayo sote hatuna budi kushirikiana katika kupambana nayo.Mojawapo ni ugonjwa wa ukimwi.Raisi wetu,Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Salma Kikwete miezi michache iliyopita,kama wanavyoonekana pichani,walituongoza kwa mfano wa kivitendo katika vita hiyo.BC leo inapenda kukumbusha kuhusu kampeni hiyo yenye kauli mbiu Tanzania bila Ukimwi inawezakana.Bila kunyosheana vidole,kutengana,kutupiana lawama wala kumnyanyapaa mwingine kila mmoja wetu ana wajibu katika vita hii.


sending...