Niliwahi kusikia mahali fulani watu wa nchi jirani na Tanzania wakisema kwamba Tanzania huwa inachelewa kidogo kuanza mambo lakini pindi wanapoanza huwa wanakuja juu kwa kasi ya ajabu! Bila kuingilia mazungumzo yao,jamaa wakawa wanataja mifano kama vile jinsi ambavyo Tanzania imepiga hatua kwenye shughuli za kisanii kama vile muziki na hivi sasa filamu.
Kuna ukweli ndani yake; tunaweza kuanza mwisho lakini tukawa vinara. Yote inategemea jinsi ambavyo tunaamua kujiweka na kusonga mbele. Mojawapo ni kukubali kwamba kuna kukosea na pia kujirekebisha. Hivi sasa sanaa ya filamu inazidi kukua nchini Tanzania. Inatia moyo sana kuona watu wa mataifa mengine wanaangalia filamu ambazo zinaitwa “za kibongo”.
Pamoja na hayo kazi kubwa bado ipo mbeleni.Kama alivyowahi kusema Steven Kanumba tulipohojiana naye,kuna haja ya serikali kutoa support ya kutosha ili kuzidi kuinua sanaa hiyo. Marekani ipo hapo ilipo kwa sababu ilitangaza sanaa na sera zake za mambo ya nje kupitia kwenye filamu. Ikulu ya Marekani ina kitengo cha kushughulikia masuala ya filamu.Kama filamu itaonekana haijakaa “vizuri” kwa mujibu wa taratibu zao,basi haitoki.Mradi unakufa.
Lingine ni hili ambalo muigizaji Mohamed Mwikongi(pichani) almaarufu kama Frank katika uigizaji ameliongelea majuzi alipofanya mahojiano na jamaa wa Global Publishers. Frank anasema lazima wasanii na washika dau wote katika nyanja za filamu wakubali kukosolewa. Wazungu wanaita hii constructive criticism. Unapokubali kukosolewa unajipa nafasi ya ushindi kwani maana yake ni kwamba kesho utafanya kizuri zaidi.Lakini pia ipo haja ya wakosoaji kutokuwa “wabezaji”. Unapokosoa basi useme pia sababu zako na utoe ushauri wa kujenga kwamba nini kifanyike.Kwa mwendo huo filamu za kibongo zitazidi kupata jina na sio ajabu kabisa siku moja nasi tukaona Slumdog Millionare za kikwetu.
Naweza kusema nimeshazoea kuhoji wenzangu.Kuhoji watu ambao ndio chachu hasa ya BC bila kusahau msomaji ambaye ni wewe.Kumbe wakati nawawinda watu wa kufanya nao mahojiano,wapo wenzangu(wenzangu katika habari na mawasiliano) ambao pia huniangazia macho ili kufanya nami mahojiano.
Naomba nikiri kwamba hiyo hutokea mara chache.Naweza kukumbuka vizuri kabisa idadi ya mahojiano rasmi ambayo nimeshawahi kuyafanya.Sio kwamba sioni thamani ya mahojiano,la!Ni kwamba hupendelea tu kuwa upande mwingine wa kamera.Usinihoji sana kwanini kwa sababu sidhani kama nina jibu moja.Tutakesha.
Hivi karibuni Freddy Macha alifanya nami mahojiano ambayo yalichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa bahati nzuri nilishawahi kufanya mahojiano na Freddy Macha kuhusu kazi zake za uandishi,muziki na historia nzima ya maisha yake.Unaweza kusoma mahojiano yangu kwenda kwake kwa kubonyeza hapa na hapa.Kwa hiyo haikuwa kazi nzito sana aliponieleza nia yake ya kufanya nami mahojiano.Freddy ni mtu mcheshi,muungwana na mvumilivu.
Ni mahojiano mafupi lakini muhimu kiasi kwani unaweza kujua kile ninachokiwaza ninapokuwa nawaza na pia ninachofikiri kuhusu suala zima la blogs na maendeleo ya ulimwengu wa habari na mawasiliano ambapo siku hizi wewe msomaji na mchangiaji ndiye mshika tochi wa habari.Unaweza kuyasoma mahojiano hayo kwa kubonyeza hapa.

UMAHIRI wa Mrisho Mpoto umekuwa ukiwakuna wengi hasa anapokuwa jukwaani akidondosha mashairi yake na mwaka jana alifanikiwa kushinda moja ya tuzo kubwa katika sanaa kwa Afrika ijulikanayo kama Slam, ambayo ilikuwa inashikiliwa na mmoja wa wasanii mahiri aitwaye, Steff H2K kutoka Mauritius.
Ushindi wa Mpoto umemfanya apate nafasi ya kushiriki fainali za tuzo za Slam za dunia, ambazo zinafanyika nchini Ufaransa Machi, mwaka huu lakini hiyo haitoshi wala haimzuii yeye kuendelea kusaka nauli ya kwenda Ikulu.
Baada ya kuwa ameshiriki katika wimbo wa ‘Salamu Zangu’ na kuweza kuchukua nafasi kubwa huku akimfunika mmliki wa wimbo huo Irene Sanga, Mpoto ameamua kuibukia upande wa pili na kutoa wimbo wa ‘Nikipata Nauli’.
[Usikilize wimbo "Nikipata Nauli" kwa kubonyeza player hapo chini kisha ndio uendelee kusoma makala hii hapo chini]JM
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Historia ya muziki wa kizazi kipya au Bongo Flava kama unavyojulikana miongoni mwa wengi hivi leo una historia ndefu. Ni historia ndefu kiasi kwamba hivi leo wengi hatukumbuki tena hata muziki huu ambao hivi leo umetokea kuwa kipenzi cha wengi ulianzaje,ukapitia hatua na harakati gani mpaka kufikia hapa ulipo hivi leo.
Miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo wa harakati za mwanzo kabisa za muziki wa bongo flava ni aliyewahi kuwa DJ maarufu nchini Tanzania kwa jina Mike Pesambili Mhagama(pichani).Mike sio tu miongoni mwa mashuhuda wa mwanzo bali pia ni miongoni mwa watu wachache walioamini katika muziki wa kizazi kipya tokea mwanzo.Kumbuka hizo ni zile enzi ambapo muziki huo ulikuwa ukichukuliwa kama “uhuni” tu na sio aina mpya ya muziki au burudani.Ni watu wachache sana walioweza kutabiri hatua ambazo muziki huo ungepiga miaka kumi au kumi na tano baadaye.
Lakini pia Mike amekuwa akikerwa na jinsi ambavyo kumekuwepo na upotoshwaji au upindishwaji wa vipengele fulani fulani muhimu vya historia ya muziki huo. Katika kujaribu kuiweka vyema historia hiyo,Mike Mhagama ameandika kwa mapana na utulivu wa kina kuhusu harakati za mwanzo za muziki wa kizazi kipya,suluba walizopitia yeye na watangazaji wenzake katika kuutambulisha muziki huo,wadau mbalimbali anaowakumbuka katika harakati hizo,wanamuziki wenyewe,promoters wa muziki nk.
Pia Mike Mhagama,anaweka wazi kitu ambacho watu wengi wamekuwa wakijiuliza;Nini chanzo cha neno Bongo Flava? Nani mwanzilishi wake?Kwa jibu hilo na historia nzima,kwa jinsi anavyoikumbuka Mhagama, msome kuanzia hapo chini,kwa maneno yake mwenyewe, kama tulivyoyanakili kutoka katika blog yake(kwa ruhusa na baraka maalumu).Habari imegawanyika katika sehemu nne ili iwe rahisi kwako kuzisoma na kuelewa vyema anachokizungumzia Mike Mhagama. Mwenyewe anasema yawezekana kabisa asiwe sahihi kwa asilimia zote na ndio maana anapenda kukaribisha hoja,maoni na masahihisho yoyote kutoka kwako msomaji.Mike Mhagama hivi sasa anaishi huko Los Angeles,California nchini Marekani.
CHIMBUKO LA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA TANZANIA NA MAANA HALISI YA NENO BONGO FLAVA.
Na Mike Mhagama-Los Angeles,Marekani.
SEHEMU YA KWANZA
Moja kati ya mambo niyapendayo mno maishani ni muziki.Nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa muziki si tu ule wa nje lakini kwa karibu ule wa nyumbani hasa muziki wa dansi na ule wenye umaarufu sana hivi sasa ujulikanao kama Bongo Flava (Muziki wa Kizazi Kipya).Katika mapenzi hayo imekuwa kama bahati kuwa mmoja wa vijana wengi tuliobahatika kuuona muziki huu wa kizazi kipya ukizaliwa na pengine bahati zaidi bila kusita kusema;kuwa mmoja kati ya wale tulioanzisha kusukuma gurudumu la muziki huu kufikia hapa ulipo na nafasi yake kutambulika si tu Afrika Mashariki bali pia kwa sasa duniani kwa ujumla.
Kama ilivyo kwa aina zingine za muziki Tanzania,mfano muziki wa dansi basi utakuwa mkosefu wa fadhila bila kujumuisha majina kama Patrick Balisidya,Mbaraka Mwaruka Mwinshehe,Salum Abdalah na hata Remmy Ongara.Hawa ni vinara na walifanya kila wawezalo kuja na ubunifu si tu kuvutia wateja wao bali kuutangaza muziki wao ndani na nje ya nchi na kuipa Tanzania kitambulisho chake kwenye jukwaa la sanaa ya muziki.Kazi za wanamuziki hawa zilifana sana kwa ushirikiano mkubwa na chombo ambacho kwa Tanzania ni muhimu sana katika kueneza au kutambulisha kitu kipya,RADIO.Watangazaji kama Mzee Ibrahim Chimgege,Enock Ngombale,Timothy Pata,Abisai Stephen,Seif Salum Nkamba na Julius Nyaisangah chini ya ma-bwana mitambo mahiri kama akina James Mhilu na Crispin Lugongo wanastahili pongezi kwa kiasi kikubwa katika kurekodi na kusimamia mitambo wakati wanamuziki hawa wakitafuta majina na namna ya kujitambulisha kwa jamii itakayosikiliza muziki wao.Bahati mbaya huwasikii sana watu hawa katika zinazoitwa historia kwa sababu wengi ni rahisi kuwasahau lakini mchango wao ni mkubwa sana na unastahili heshima hasa unapoandika au kuizungumzia historia ya muziki wa dansi Tanzania. (more…)

Binti aliye pichani hapo juu anaitwa Megan Fox.Kwa mapana na marefu sio bongo celebrity.Yawezekana kabisa kwamba hata Bongo hajawahi kuisikia!
Kwanini basi tumemuweka hapa leo? Sababu ni kwamba binti huyu ndiye ambaye kwa mwaka huu wa 2008, jarida maarufu la FMH, lilimtaja kama mwanamke nambari wani mwenye mvuto zaidi miongoni mwa wanawake 100 iliyowaorodhesha kama wanawake wenye mvuto zaidi duniani.
Kwa bahati nzuri au mbaya,vyombo vya habari kama hivi vikishirikiana na vitu kama filamu,muziki nk ndivyo ambavyo hivi leo vina ushawishi mkubwa kuhusiana na suala zima la uzuri,urembo au mvuto.Vikisema fulani ndio mwenye mvuto zaidi basi mabilioni ya watu wanaamini hivyo.Matokeo yake ndio watu wengi(hususani wanawake) huanza safari ndefu ya kujinyima chakula ili wapunguze saizi za miili yao na kufanana na huyo aonekanaye “mzuri” kwa mujibu wa jarida fulani.Wengine hufanya kila wawezalo ili wawe na nywele,rangi ya mwili,kucha nk kama za huyo aonekanaye “mzuri” nk.Kwa bahati mbaya hata mengi ya majarida yaliyopo au yanayoanzishwa nchini Tanzania,yanafuata mkondo huo huo wa “kutafsiri” urembo,uzuri na mvuto.
Je urembo,uzuri,mvuto ni vitu gani?Ni kweli kwamba uzuri au urembo uko katika mboni ya jicho la mtazamaji au kutoka katika akili na macho ya mhariri wa jarida?Nini kifanyike ili kumfanya kila mtu aridhike na jinsi alivyo ili kupunguza mahangaiko,watu kupoteza maisha wakati wa zoezi la kujikondesha nk?

Katika anga za siasa duniani hivi leo,lipo jina ambalo dunia nzima inaendelea kulizungumzia.Hilo si lingine bali lile la Rais wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe.Kwa wengine mtu huyu ni shujaa,kwa wengine mtu huyu ni kinyume kabisa cha neno shujaa.Kwako wewe je?Je viongozi wa Afrika wanaohudhuria kikao cha Umoja wa Afrika huko Misri(na Mugabe naye anahudhuria) wataweza kumnyoshea vidole Mugabe?Nini hatma ya siasa za Afrika?
Pichani ni Rais Mugabe akiwa na mkewe,Grace Mugabe.Wengi wanasema wakati wao wanatafuna keki,wananchi wengi wa Zimbabwe wanakufa njaa.
Photo/New York Times
Yapo mambo ambayo pindi yakitokea kila binadamu hushikwa na butwaa na kutokutambua mara moja kwamba nini kimetokea,kinatokea au kinaelekea kutokea. Mojawapo ya mambo kama hayo ni kama kitendo kilichotokea hivi majuzi pale katika hospitali ya Muhimbili ambapo mtoto mwenye umri wa miaka 12 ajulikanaye kama Ramadhani Mussa(pichani) alikamatwa akiwa na kichwa cha mtoto mdogo, Salome Yohana (miaka 3) alichokuwa amekibeba kwenye mfuko wa Rambo!

Tukio hilo la aina yake,la kusikitisha na hata kuchosha akili limeandikwa na blogs mbalimbali na pia vyombo karibuni vyote vya habari nchini Tanzania.Kwa sababu habari yenyewe bado inazua mijadala mbalimbali, tumeona sio vyema kukunyima wewe msomaji na mtembeleaji wetu, fursa ya kutoa maoni yako kuhusiana na tukio hili.Nini maoni yako kuhusiana na tukio hili? Ni uchawi, imani za kishirikina, matatizo ya akili au ni nini hasa? Kwanini watoto?
Isitoshe,mtoto Ramadhani Mussa, ambaye hivi sasa anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Ilala, Kanda Maalumu ya Dar-es-salaam akiendelea kuisaidia polisi na uchunguzi, yawezekana ndio jina au tukio lililotawala vinywa vya watu wengi hivi sasa.
Kama hujapata fursa ya kusoma habari mbalimbali kuhusu tukio hili,unaweza kufanya hivyo kwa kubonyeza hapa na hapa na hapa.
Wakati huo huo,gazeti la Uwazi(mojawapo ya magazeti ya Global Publishers), hivi leo wametoa habari ya kina ya tukio hili kama ambavyo unaweza kuiona katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo hapo chini.Unaweza kuisoma habari hiyo kamili kwa kubonyeza hapa.

Mbali na kuwa na utajiri wa asili wa aina yake,Tanzania ni nchi ambayo inajivunia kuwa na wasomi maarufu ambao wametapakaa kote ulimwenguni wakifundisha katika mashule na vyuo mbalimbali au kuongoza vitengo nyeti katika idara za kimataifa na zenye uzito wa ki-dunia nzima.
Mmojawapo miongoni mwa wasomi hao ni Prof.Joseph Mbele(pichani),mtanzania anayefundisha katika Chuo cha St.Olaf kilichopo Northfield jimboni Minnesotta nchini Marekani.Miongoni mwa wasomi na wafuatiliaji wa mambo mbalimbali ya kitaaluma jina la Prof.Mbele sio geni hata kidogo.Prof.Mbele ni mtunzi wa kitabu maarufu sana kiitwacho Africans and Americans:Embracing The Cultural Differences.Kitabu hicho ndicho kinachotumika zaidi hivi leo mashuleni na katika taasisi mbalimbali(zikiwemo balozi mbalimbali) wanapokuwa wanawaandaa watu wao kuja kusoma, kutembea tu,kufanya kazi au tafiti mbalimbali barani Afrika.
Kutokana na kwamba kumekuwepo na mijadala mingi sana kuhusiana na masuala yote yahusuyo mila,tamaduni,desturi,maisha ya ughaibuni nk,BC tuliamua kumtafuta Prof.Mbele ambaye ni msomi anayetambulika kimataifa na mwenye mamlaka ya kutosha kuhusiana na maeneo yaliyotajwa hapo juu ili kupata maoni na mitizamo yake.Katika mahojiano haya,Prof.Mbele anafafanua mambo mengi sana kama vile’je kuna kitu kama mila,tamaduni na desturi za kitanzania?Kwanini watu wengi hivi leo hususani vijana wanazidi kubobea kwenye tamaduni za kimarekani?Kwanini aliandika kitabu hicho kilichotajwa hapo juu? Kama wanajamii tunakubaliana kwamba tumepoteza dira na muelekeo katika tamaduni,mila na desturi zetu,nini kifanyike?Kwa majibu ya maswali hayo na mengineyo mengi,fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; (more…)
Kwa kila mtanzania,iwe anajitambulisha kama mzalendo au asiye mzalendo,matukio ya wiki hii nchini Tanzania yanatia simanzi,tena sana.Inakuwaje watu fulani fulani,wachache tu,wamuumize kila mtu kwa sababu ya uroho wa kujilimbikizia mali usio na kifani?Hivi kuna raha gani kuwa na mabilioni ya pesa halafu ukitoka tu getini kwako unakutana na ombaomba? Kuna raha gani ya maisha kutoka getini kwako kisha ukakumbana na barabara zilizojaa mashimo na mavumbi eti kisa umekula rushwa na hivyo kuzuia mradi mzima wa utengenezwaji wa barabara? Kuna raha gani kulala huku jenereta likiunguruma usiku kucha(kwako,tena kwa sababu unaweza kulinunua hilo jenereta) huku karibuni nchi nzima ikiwa kizani kwa ukosefu wa umeme eti kwa sababu wewe umeamua kuneemesha mfuko wako kwa njia isiyo halali?Kuna raha gani….?
Kama tulivyodokeza kidogo juma hili,swali sasa sio tena tunaelekea wapi bali tumefikaje hapa? Sasa leo kwa sababu ni Ijumaa na piga ua,jadi lazima iendelee,burudani ya mziki ipo pale pale.Lakini leo tuna ujumbe mahsusi kabisa.Ni kutoka kwao The Ngoma Afrika Band(pichani),bendi ya watanzania chini ya uongozi wa Ras Ebby Makunja na yenye makao yake makuu kule Oldenburg,Germany.Wao wanasema Rushwa Ni Adui wa Haki.Pengine hapa ndipo tunapoweza kuanzia katika kujibu swali Tumefikaje Hapa?
BC inaanda mahojiano rasmi na The Ngoma Africa Band.Yatawajieni yatakapokamilika.Ila kwa sasa pata burudani ya wimbo wao huu wenye ujumbe murua hususani katika mazingira tuliyonayo hivi sasa.Bonyeza tu player hapo chini.Ijumaa Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Lakini subiri kidogo,yaani zilipendwa leo hamna BC?Haiwezekani,wasikilize Western Jazz Band wakisema Sasa Tutacheza Cha Cha Cha.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Tangu tuweke hewani sehemu ya kwanza ya mahojiano yetu na Freddy Macha wiki chache zilizopita,siku imekuwa haipiti bila kupokea barua pepe,simu au ujumbe mfupi kupitia simu za viganjani nk.kutoka kwa baadhi yenu wasomaji na wachangiaji wa BC mkitaka kupata uhondo wa sehemu ya pili.Hatuwezi kuwalaumu,tunaelewa ni jinsi gani Freddy Macha,iwe ni kupitia uandishi,ushairi na pia muziki,anagusa hisia za wengi.
Kama tulivyoahidi,hii hapa sehemu ya pili ya mahojiano yetu na Freddy Macha akizungumzia zaidi kazi zake za muziki,mambo mbalimbali ya kijamii na mengineyo kedekede.Kama ilivyo katika uandishi na ushairi,kwa upande wa muziki Freddy Macha pia kajaa tele.Anayo mengi ya kusimulia na kuweka wazi kuliko unavyoweza dhania.
Unataka kujua Freddy ametokea wapi mpaka kujikita kwenye sanaa ya muziki? Je una habari kwamba huyu bwana ni mtaalamu na mcheza karate wa kutupwa? Anasemaje kuhusu muziki wa kizazi kipya?Ana ushauri gani?Nini chanzo cha Kitoto Band?Je…
Mwisho wa mahojiano haya,utaweza kusikiliza baadhi ya nyimbo za Freddy akiwa na kundi lake lijulikanalo kama Kitoto Band.Hiyo ni zawadi maalumu kutoka kwa Freddy Macha na BC kwako msomaji,mchangiaji na hususani mpenzi wa muziki.Kwa hakika,kama wengi wenu mnavyopenda kusema,haya ni “mahojiano-shule”.Fuatana nasi; (more…)

