MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

ansbert-ngurumobcJina la Ansbert Ngurumo sio geni hata kidogo miongoni mwa wapenda habari na mawasiliano na hususani wapenzi wa habari za magazetini. Ansbert ni miongoni mwa waandishi wa habari mahiri nchini Tanzania ambao wamejijengea sifa na heshima kutokana na kazi zao za uandishi wa habari.

Safu yake ya Maswali Magumu,inayochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima kila jumapili inabakia kuwa safu yenye wasomaji lukuki huku kila mara ikizua mijadala ya aina yake jambo ambalo ni uthibitisho kwamba sio tu inapendwa bali pia hujibu na pia kuuliza Maswali Magumu.

Ansbert ni blogger mzoefu pia.Blog yake ambayo inaongozwa na kichwa cha habari, Utakapojua Hujui Ndipo Utakapojua, ni sehemu mojawapo nzuri ambapo unaweza kukuta kazi zake za uandishi,mitizamo na pia mikingamo.

Hivi karibuni,jamaa wa mtandao wa Rap21,walifanya naye mahojiano ambayo kwa kila hali ni “must read” kwa mtu yeyote ambaye yupo kwenye fani ya ku-blog au ni mfuatiliaji wa maendeleo ya tekinolojia hii ambayo mimi naiita mapinduzi ya karne katika ulimwengu wa habari na mawasiliano.

Katika mahojiano hayo,Ansbert ameongelea kwa mapana jinsi ambavyo blogs,ikiwemo ya kwake, zinazidi kuboresha mapinduzi hayo na pia jinsi gani blogs zinaweza kutumika katika kuboresha maisha ya wanajamii,kutunza historia zetu,kufichua maovu nk.Bonyeza hapa ili kusoma mahojiano hayo.

Blog ya Issa Michuzi hivi sasa inapatikana tena kwa kutumia anuani ile ile ya zamani ya www.issamichuzi.blogspot.com. Hiyo inafuatia matatizo ya kiufundi ambayo yamekuwa yakiikumba blog yake kwa muda wa takribani wiki nzima. Kwa hiyo kwa sasa Michuzi anapatikana kule kwa zamani mpaka hapo matatizo ya kiufundi yatakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Wakati huo huo,kama ambavyo mmeona, tovuti ya Global Publishers,nayo inakabiliana na changamoto za kiufundi kidogo kwani hivi sasa haipatikani hewani kama ilivyokuwa.Hata hivyo,Global Publishers wametufahamisha kwamba mafundi wanajitahidi kwa kila hali kuhakikisha kwamba mambo yanarejea kuwa mswano mapema iwezekanavyo.

Wote wawili,Michuzi na Global Publishers, wanakushukuru kwa uvumilivu wako.

Kama wewe ni msomaji mzuri wa magazeti na majarida mbalimbali kutoka Tanzania,basi sina shaka kabisa kwamba jina Maggid Mjengwa (pichani) litakuwa sio geni kwako! Makala zake za kusisimua,kuchokoza hisia na kujenga hoja za nguvu ni miongoni mwa vivutio muhimu vya wasomaji wa magazeti ndani na nje ya Tanzania. Leo hii tunaweza kabisa kuthubutu kusema kwamba Maggid ni miongoni mwa wanahabari bora tulionao kwani hana uoga wowote pale anapokuwa anaandika au kuongelea jambo ambalo analiamini kwa dhati.

Lakini Maggid,kama ambavyo pengine unafahamu tayari, haishii magazetini tu bali pia ni blogger maarufu hivi sasa. Blog yake ya picha ambayo mwenyewe anaiita “kijiji” na hivyo wasomaji wake na watembeleaji wake “wanakijiji”, imejipatia umaarufu sana kwa kuonyesha au kwenda kule ambapo ndiko kunahesabika kuwa kwenye hali halisi ya maisha ya mtanzania. Ukiitembelea na kuisoma blog yake vizuri kwa kutizama picha lukuki zinazoipamba blog yake,utaweza kuwa jaji mzuri kama “bongo ni tambarare” au bado zile ahadi za uchaguzi uliopita ni mbwembwe za kisiasa tu.Mwenyewe anasema blog yake ni kimbilio na sauti kwa wale ambao kila mara huwa wanasahauliwa!

Maggid pia ni mjasiriamali.Yeye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ijulikanayo kama Ikolo Investment Co ambao ndio wachapishaji wa Gozi Spoti; jarida la michezo, sanaa, maisha na burudani linalotoka kila Jumatano. Maggid pia ni mwanamichezo,mpenda michezo na shabiki mkubwa wa soka.

Hivi karibuni,baada ya kumsaka kwa muda mrefu kutokana na ratiba zake za kazi kumbana,tulifanikiwa kupata fursa ya kufanya naye mahojiano utakayoyasoma hivi punde.Kama ambavyo ungetegemea,Maggid anatoa “darasa” katika mahojiano haya.Mbali ya kukupa historia ya maisha yake kwa undani,Maggid anakumbusha vipengele fulani fulani vya historia ya nchi yetu ambavyo ni muhimu. Lakini kwa mapana, anaongelea kuhusu suala la uandishi na pia blog yake bila kusahau changamoto ambazo nchi yetu inakabiliwa nazo hivi leo katika nyanja mbalimbali. Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; (more…)

Kuanzia usiku wa leo(saa sita usiku kwa saa za Afrika Mashariki),blog maarufu ya Muhidin Issa Michuzi,itabadilisha anuani.Badala ya kupatikana kupitia www.issamichuzi.blogspot.com sasa itapatikana kupitia www.michuzi-blog.com.

Mbali na mabadiliko hayo ya anuani,yupo “mwana” mwingine ambaye naye anazaliwa.Hiyo ni tovuti nyingine chini ya usimamizi wa huyu huyu gwiji wa blog. Tovuti hiyo ambayo inapatikana kupitia www.bongotyube.com ni maalumu kwa habari,burudani,michezo nk kupitia video.

Kama kawaida yetu,tulipopata habari kuhusiana na mabadiliko hayo katika blog hiyo ya jamii pamoja na tovuti mpya inayoanzishwa,tuliona ni heri tumtafute Michuzi mwenyewe ili atupe undani kidogo kuhusu mabadiliko hayo nk.Kwa uungwana kabisa akakubali kufanya nasi mahojiano utakayoyasoma hivi punde ingawa ukweli ni kwamba yuko bize ili kuhakikisha kwamba mabadiliko yaliyotajwa hapo juu yanakwenda salama kabisa.

Lakini pamoja na kuongelea mabadiliko hayo,Issa Michuzi,ametoa mafunzo na changamoto muhimu sana kwa wanablog na pia washika dau mbalimbali katika sekta au fani ya habari na mawasiliano.Je ni changamoto na mafunzo gani?Anawaambia nini “wadau” wakati huu anapojiandaa kuendeleza “libeneke” kwa mapana na marefu zaidi? Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; (more…)

Kwa wengi siku hizi anajulikana kama Binamu.Lakini alipoingia rasmi kwenye ulimwengu wa muziki aliitwa MwanaFalsafa.Jina lake kamili ni Hamisi Mwinjuma(pichani).Ni mshindi wa tuzo maarufu za Kili.

Tangu aingie kwenye fani ya muziki,sifa moja ambayo amekuwa nayo ni kuwa na mashairi au lyrics kali. Ilikuwa ni lazima uwe na uelewa mzuri wa lugha ya Kiswahili ili upate maana halisi ya nyimbo zake.Uwezo wake wa kwenda sambamba na mapigo (beats) za kimuziki huku akighani ipasavyo mashairi yake ni jambo linguine lililomfanya awe mmoja miongoni mwa wanamuziki wa B Flava wenye mashabiki lukuki..

Hivi karibuni MwanaFA amezindua tovuti yake rasmi.BC tulipata nafasi ya kufanya naye mahojiano kuhusiana na ujio wa tovuti hiyo,muziki wake,mipango yake ya baadaye na mengineyo mengi.Kwanini ameiita tovuti yake binamu13.com? Ana mipango gani katika miaka mitano ijayo? Anasemaje kuhusu ujio wa mwanamuziki 50 Cent nchini Tanzania hivi karibuni?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; (more…)

 

Kwa miaka nenda rudi, tangu miaka ya sabini,jina la Freddy Macha (pichani) limekuwa sio geni miongoni mwa wasomaji mbalimbali wa magazeti, vitabu vya hadithi fupifupi,wapenzi wa muziki na pia sanaa ya ushairi nchini Tanzania. Iwe unamfahamu Freddy kupitia muziki wake,makala zake au mashairi yake, utakubaliana nasi kwamba Freddy ni mojawapo ya hazina tulizonazo linapokuja suala zima la usanii. Wengi miongoni mwa wasomaji wa makala zake katika magazeti ya The Guardian na Mwananchi nchini Tanzania, wanakiri kwamba makala za Freddy huwa ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wakati mwingine wadamke asubuhi na mapema ili mradi tu wasikose nakala za magazeti hayo hususani siku zinazochapishwa makala zake.

Wapenzi wengi wa muziki,ushairi, tamthiliya na ngoma mtakuwa mnamkumbuka Freddy Macha tangu alipokuwa na kundi la Sayari. Kundi hilo ambalo lilitamba sana mwanzoni mwa miaka ya themanini, ni mojawapo ya vikundi vichache vya sanaa nchini Tanzania vilivyopata mafanikio sio tu nchini Tanzania bali pia katika medani za kimataifa. Sayari liliwahi kufanya ziara kadhaa za kimaonyesho katika nchi mbalimbali za nje hususani za Ulaya enzi hizo.

Kwa upande wa uandishi,Freddy Macha alianza kunoa kalamu katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo na baadaye kuwa mwanasafu(columnist) wa gazeti la kila jumapili la Sunday News hadi mwaka 1984.Freddy amewahi kushinda tuzo kadhaa za uandishi ikiwemo ile ya Ushairi ya BBC mwaka 1981 na hadithi fupi fupi ya Jumuiya ya Madola( Commonwealth of Nations) ya mwaka 1996.

Hivi karibuni, baada ya kumsaka kwa muda mrefu, tulipata nafasi ya kufanya mahojiano ya kina na mwandishi/mwanamuziki/mwalimu huyu ambaye hivi sasa anaishi London nchini Uingereza. Sasa kutokana na ukweli kwamba Freddy ni mmojawapo miongoni mwa wale watu ambao tunaweza kuwaitwa “wenye vipaji vingi”,tumeamua kuyagawa mahojiano yetu naye katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza, ambayo ndiyo hii unayoisoma leo, tumeongea naye zaidi kuhusu kazi zake za uandishi.Sehemu ya pili ambayo itawajieni baadaye kidogo,tuliongea naye kuhusu muziki,jamii na mengineyo kadha wa kadha.

Unataka kujua Freddy ametokea wapi?Amepitia mambo gani mpaka kufikia hapo alipo? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uandishi wa leo akilinganisha na ule wa zamani? Kwanini kitabu chake cha hivi karibuni amekiita Mpe Maneno Yake? Unafahamu kwamba Freddy aliwahi “kuzamia meli”?Ilikuwaje? Anasemaje kuhusu dhana za mawasiliano kama blogs? Kwa hayo na mengineyo mengi, fuatana nasi katika sehemu hii ya kwanza ya mahojiano yetu naye; (more…)

 

Pichani ni wasanii wa muziki wa kizazi kipya,Bongo Flava, Ilunga Khalifa a.k.a C Pwaa(kushoto) na Falid Kubanda a.k.a Fid Q(kulia).

Ilunga Khalifa (CP)ni mmoja kati ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye anakwenda na wakati kwa kuhakikisha kwamba anazitumia tekinolojia za kisasa vilivyo kwa manufaa ya kibiashara na kimuziki.Tunasema hivyo kwa sababu C-Pwaa kwa kutumia kamera ya simu yake ya mkononi anaendesha blog ambayo anaiita Simu Yangu Kamera.Unaweza kuitembelea blog yake kwa kubonyeza hapa.

Picha na MichuziJR.

↑ Go Back to Top of Page