
Kuanzia usiku wa leo(saa sita usiku kwa saa za Afrika Mashariki),blog maarufu ya Muhidin Issa Michuzi,itabadilisha anuani.Badala ya kupatikana kupitia www.issamichuzi.blogspot.com sasa itapatikana kupitia www.michuzi-blog.com.
Mbali na mabadiliko hayo ya anuani,yupo “mwana” mwingine ambaye naye anazaliwa.Hiyo ni tovuti nyingine chini ya usimamizi wa huyu huyu gwiji wa blog. Tovuti hiyo ambayo inapatikana kupitia www.bongotyube.com ni maalumu kwa habari,burudani,michezo nk kupitia video.
Kama kawaida yetu,tulipopata habari kuhusiana na mabadiliko hayo katika blog hiyo ya jamii pamoja na tovuti mpya inayoanzishwa,tuliona ni heri tumtafute Michuzi mwenyewe ili atupe undani kidogo kuhusu mabadiliko hayo nk.Kwa uungwana kabisa akakubali kufanya nasi mahojiano utakayoyasoma hivi punde ingawa ukweli ni kwamba yuko bize ili kuhakikisha kwamba mabadiliko yaliyotajwa hapo juu yanakwenda salama kabisa.
Lakini pamoja na kuongelea mabadiliko hayo,Issa Michuzi,ametoa mafunzo na changamoto muhimu sana kwa wanablog na pia washika dau mbalimbali katika sekta au fani ya habari na mawasiliano.Je ni changamoto na mafunzo gani?Anawaambia nini “wadau” wakati huu anapojiandaa kuendeleza “libeneke” kwa mapana na marefu zaidi? Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; 
Kila mwaka,tarehe 14 February(Siku ya Wapendanao),yeye hukumbuka au kusheherekea siku yake ya kuzaliwa. Alipozaliwa wazazi wake walimuita Fina.Leo hii wengi tunamfahamu kama Fina Mango(pichani),mtangazaji maarufu wa kituo cha radio cha Clouds FM.
Yeye ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watano(5) kwa upande wa mama yake, Fortunata M.Mango na watoto saba(7) kwa upande wa Marehemu baba yake,,Joseph Mango.Anaye dada mmoja na kaka watatu(3) wa kuzaliwa tumbo moja na dada mmoja na kaka mmoja wa kambo.
Alianza pilikapilika za masuala ya elimu mkoani Arusha katika shule ya Mtakatifu Constantine(St.Constantine) na baadaye kujiunga na shule ya sekondari Jitegemee jijini Dar-es-salaam kwa ajili ya masomo ya O-Level.Kisha akajiunga na shule ya Shaaban Robert ya jijini Dar-es-salaam kwa masomo ya A-Level na kuhitimu mwaka 1999. Baada ya hapo akajiunga na Clouds FM ingawa kimasomo hakuishia hapo kwani baadaye alijiunga na FTC(Financial Training Centre) ambapo amesomea masuala ya biashara.Bado ana mpango wa kuendelea zaidi kimasomo.
Leo hii yeye ni Brand Manager wa kipindi cha Power Breakfast ambacho anakiendesha kwa kushirikiana na Masoud Kipanya (KP).Kipindi kinarushwa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 12 alfajiri mpaka saa 3 asubuhi.
Fina Mango pia ni mjasiriamali, yeye ndio mmiliki wa kampuni ijulikanayo kama One Plus Communication ambayo inashughulika na masuala ya Usimamizi wa Shughuli na Matukio ya Mashirika mbalimbali na Uhusiano wa Jamii (Corporate Events Management & Public Relations (PR). Ofisi za One Plus Communication zipo maeneo ya Victoria ilipo Victoria Gas Station pembezoni mwa barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Hivi karibuni tulipata fursa ya kufanya naye mahojiano ambapo tuliongelea mambo mengi kuhusiana na kazi yake ya utangazaji,maisha yake binafsi na mipango yake ya baadaye.Kumbukumbu na uwazi alionao Fina ni jambo ambalo limetuvutia sana. Unataka kujua Fina anasemaje kuhusu maendeleo ya kisayansi na kitekinolojia ulimwenguni? Asingekuwa mtangazaji angependa kuwa nani?Je umeshawahi kuona picha za utotoni za Fina? Fuatana nasi katika mahojiano haya ya pekee. 

Ukiachilia mbali blogs au tovuti mbalimbali zinazojitahidi kuhifadhi historia au kumbukumbu za watu wetu mashuhuri mtandaoni,mradi kama Wikipedia ndio pengine unaongoza hivi sasa katika kuhifadhi historia mbalimbali,kuelimishana,kupashana habari nk.Uzuri ni kwamba Wikipedia inaandikwa katika lugha mbalimbali ikiwemo yetu ya Kiswahili. Burudani zaidi inakuja pale ambapo wote,mimi na wewe,tunaweza kuchangia katika kuziandika historia za watu wetu mashuhuri.Hapo hakuna mjuzi zaidi ya mwingine.Kila mtu anajua kitu fulani kwa hivyo anachangia. Kama nitaandika kwamba Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1962,nitakuwa nimekosea.Bila kutoana ngeu,unaingia unanirekebisha tunapata ukweli.Huo ni mfano tu,Wikipedia ina maarifa mengi zaidi.
Kwa mfano; Hayati Bibi Titi Mohamed,pichani kushoto akiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni mtu mashuhuri na muhimu sana katika historia ya nchi yetu achilia mbali juhudi za ukombozi wa mwanamke.Pamoja na hayo,ukienda kwenye ukurasa wa Wikipedia wa Kiswahili,utakuta kwamba habari za Bibi Titi zimeandikwa kwa kifupi sana. Ni kama vile hakuna anayejua mengi kuhusiana na Bibi Titi,si watu wa enzi zake wala wa enzi hizi.Mbali na uchache wa habari za Bibi Titi kwenye Wikipedia,kwa ujumla mtandaoni habari zake zipo kwa uchache sana.Tunaishi katika nyakati mpya,za habari na mawasiliano ya hali ya juu.Ni muhimu tukazitumia katika kuhifadhi historia pia.Sio za Bibi Titi tu bali wengineo wengi waliowahi kutokea,waliopo na watakaoendelea kutokea nchini mwetu.
“Bibi Titi Mohammed ni mmoja wa wanawake wa kwanza kushika nafasi za ubunge na uwaziri nchini Tanzania na pia ni kati ya wanawake wa kwanza kujiunga na harakati za kugombea uhuru wa Tanganyika.
Mwaka 1969 Bibi Titi Mohammed alikamatwa na mwaka uliofuata alifikishwa mahakamani kwa kosa la kula njama ya kutaka kupindua serikali. Katika kesi hiyo, Bibi Titi alikuwa ni mwanamke pekee katika washtakiwa 7. Baada ya kesi hiyo kusikilizwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Hata hivyo, mwaka 1972 alisamehewa na rais Julius Nyerere”
Ukienda kwenye ule ukurasa wa Wikipedia wa Kiingereza kumhusu Bibi Titi,utagundua kwamba pameandikwa mambo mengi kidogo kumhusu Bibi Titi. Kwanini? Mara nyingi tumekuwa tukiacha historia yetu,ya watu wetu,iandikwe na watu wengine.Wakiandika wanavyotaka wao,kwa kuipotosha, tunalalamika.Ajabu huwa hatuna muda wa kuirekebisha. Zamani tulikuwa na sababu,hatuna tena.
Kupitia kurasa kama Wikipedia,tunaweza rekebisha historia zetu.Kwanini leo usijiandikishe katika Wikipedia na kuanza kuchangia chochote unachokijua kuhusu historia,siasa,jamii zetu? Unaonaje kama tukianza na kupanua zaidi historia ya Bibi Titi Mohamed? Kumbuka unapohifadhi historia huhifadhi kwa ajili yako tu bali vizazi na vizazi vijavyo.Binadamu asiyejua historia yake ni….
Picha kwa msaada wa Issa Michuzi.
Baraza la Kimataifa la Usafiri wa anga limemteua mtanzania Omari Nundu (pichani) ambae ni mtaalam wa masuala ya anga kuwa Rais wa tume yake ya ufundi inayoundwa na magwiji wa fani hiyo duniani. Bwana Nundu ataiongoza tume hiyo kwa mwaka 2008 na anakuwa ni mwafrika wa kwanza kushikilia wadhifa huo mkubwa katika duru za anga duniani.
Tume hiyo ndio chanzo kikuu cha sheria, hatua na viwango vya kufuatwa katika utengenezaji wa ndege, viwanja na vifaa vya kuongozea ndege na pia ndio inayotuinga na kusimamia sheria za usafiri wa anga duniani.
Nundu ni mzaliwa wa Tanga na safari yake ya Urais wa tume hiyo ya magwiji wa anga ilianza mnamo mwaka wa 2005 wakati nafasi ya wajumbe (makamishna) zilipoongezwa kutoka 15 hadi 19 ambapo Tanzania ilimteua Bwana Nundu kugombea nafasi hiyo iliyogombewa na nchi tisa na kuibuka na ushindi mkali dhidi ya mataifa mengine. Alianza kutumikia nafasi hiyo mwaka huo huo na makamishna wenzake wakamchagua kuwa Makamu wa Rais wa tume hiyo mwaka huu.
Bwana Nundu anakuwa pia ni rais wa kwanza kuchaguliwa akitokea katika nafasi ya Umakamu wa Rais.
Tume hiyo inaundwa na wataalam wa hali ya juu duniani katika fani ya usafiri wa anga na kila kamishna huchaguliwa kwa vigezo vya umahiri na mchango wake mkubwa aliowahi kutoa katika fani hiyo duniani na kila kipindi huwa na waombaji wengi kuliko nafasi ambapo makamishna hao huishia kuteuliwa kwa ushindani mkali wa kura.
Habari hii na picha imeletwa kwenu kwa hisani ya Saidi Yakubu,London.


sending...