
Kuna kitu nimekipenda katika kuitazama kwa makini picha hii.Bahati mbaya siwezi hata kuelezea vizuri ni kitu gani nilichokipenda katika picha hii ya wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) walipokuwa wakimshangilia mgombea Urais kwa tiketi ya chama hicho,Dr.Wilbrod Slaa,wakati wa ufunguzi wa kampeni za chama hicho katika viwanja vya Jangwani jijini Dar-es-salaam.
Ni matumaini, ni saa ya ukombozi,ni kwamba tumechoka sasa au?
Picha kwa hisani ya John Bukuku.
Pamoja na kwamba inasemekana kampeni za uchaguzi hazijaanza rasmi au hazitakiwi kuwa zimeanza,ukweli ni kwamba kwa namna moja au nyingine,kampeni zimeshaanza.Huu ni ukweli ambao Tume ya Uchaguzi lazima waukubali ili marekebisho yafanyike endapo wanataka kuwa makini zaidi katika kuhakikisha kwamba vyama vyote na wagombea wote wanasubiri mpaka tarehe 20 Augosti siku ambayo ndio kampeni rasmi zinatakiwa kuanza.
Tunathubutu kusema hivyo kwa sababu tayari tumesikia mara kadhaa viongozi/wagombea mbalimbali wakijinadi kwamba wamefanya nini katika miaka mitano iliyopita na wanatarajia kufanya nini endapo wananchi watawapa tena dhamana ya kuongoza nchi kwa miaka mingine mitano.
Pia tumeshasikia tambo mbalimbali kutoka kwa wanaowania kuunda serikali mpya,wakijinadi kuhusu watakachokifanya tofauti endapo “ngekewa” ya kuwaongoza watanzania itawaangukia wao.Sasa kama tambo hizo sio sehemu ya kampeni,sijui Tume ya Uchaguzi ina tafsiri ipi kuhusu maana ya “kampeni”.
Bila shaka,baada ya kuwasikia wagombea mbalimbali wakijinadi na kutokana na uzoefu wako na jinsi unavyofuatilia shughuli mbalimbali za kisiasa,umeshafanya maamuzi(japo katika fikra tu) kwamba pindi itakapofika mwezi Octoba,kura yako utampa mgombea fulani.Ndio maana tunauliza;Uchaguzi Ungefanyika Leo,Ungemchagua Nani?Kwanini? Wanaogombea nafasi ya Urais kutoka vyama mbalimbali,hawa hapa:

Civic United Front(CUF): Professor Ibrahim Haruna Lipumba(kulia) na mgombea mwenza,Juma Duni Haji.

Chama Cha Mapinduzi(CCM):Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Mwenza,Dr.Gharib Bilal.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)
r.Wilbrod Slaa akisalimiana na Mgombea Mwenza,Hamisi Mzee Hamisi.

National Convention for Construction and Reform-Mageuzi(NCCR-Mageuzi)-Hashim Rungwe(kushoto) na Mgombea Mwenza,Ali Juma.
Katika mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania,mojawapo ya mambo ambayo tumedhamiria hapa BC ni pamoja na kuvipa vyama vyote kisiasa nchini Tanzania, nafasi ya kunadi sera zao kwa watanzania walio ndani na nje ya nchi,kuwasiliana nao kupitia hapa, kufikisha ujumbe wao kwa wadau wa michakato ya kidemokrasia ulimwenguni nk.
Hivi karibuni tutafungua msururu wa mahojiano na baadhi ya waliokwisha kutangaza nia ya kugombea nafasi za kisiasa iwe ni Urais au Ubunge ili wananchi,wapiga kura wa leo na kesho,wajue kwa undani sera na ushawishi uliopelekea mtu fulani kujitokeza kama mgombea na hivyo,kama atachaguliwa,atakuwa kiongozi wao katika mapambano ya kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa miaka mitano ijayo. Kama wewe ni mgombea na ungependa habari zako,sera zako nk ziwekwe hapa,unaweza kuwasiliana nasi kwa kupitia barua pepe; info at bongocelebrity dot com au bongocelebrity at gmail dot com.
Sasa ili kupata mahojiano yaliyo bora na yenye usawa,tumekuwa tukipitia katika tovuti rasmi za vyama ili kutizama kwa makini sera,historia na habari kuhusu wagombea mbalimbali kupitia vyama hivyo ili kupata habari za uhakika,zilizopitishwa na vyama husika na hivyo kuboresha uwazi na usawa tunaojaribu kuuzingatia.
Kwa bahati mbaya,katika chambua chambua yetu mtandaoni,bado hatujafanikiwa kuziona tovuti za vyama vya Tanzania Labor Party(TLP) na Chama Cha Wananchi-CUF(Civic United Front). Juhudi zetu za kuwasiliana na vyama hivyo kupitia anuani za barua pepe ambazo tulifanikiwa kuzipata kupitia mtandaoni,hazikuzaa matunda kwani barua pepe zote ziliturudia zikiashiria kutokuwepo hewani kwa anuani hizo!
Kutoziona au kukosekana kwa tovuti rasmi za vyama hivyo mtandaoni,ndiko kulikopelekea tuje hapa uwanjani na kuuliza swali lililopo katika kichwa cha habari hii.
Je,msomaji,unaweza kutusaidia na tovuti za vyama hivyo kama zipo? Kama hazipo,yabidi tujiulize maswali ya ziada.Kwanini? Hivi katika dunia ya leo kweli vyama vikubwa vya siasa kama CUF na TLP(vyote vimesimamisha wagombea Urais),havioni umuhimu wa kuwa na tovuti zao rasmi?
Kwa upande mwingine, Chama Cha Mapinduzi-CCM kinayo tovuti rasmi ambayo unaweza kuitembelea kwa kubonyeza hapa. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA nacho kina tovuti rasmi ambayo unaweza kuitembelea kwa kubonyeza hapa. Lakini hizi nazo zina tatizo sugu la kutokwenda na wakati(updated).Taarifa na habari zilizopo,haziendi sambamba na matukio yaliyopo.
Pichani ni Logo au Nembo za Vyama husika.Nembo ya TLP haikuweza kupatikana.Tungependa sana kusikia kutoka kwa viongozi wa CUF au TLP kuhusu suala hili.Kama tovuti zipo bali kwa sababu moja ama nyingine tumeshindwa kuziona mtandaoni,tungefurahi kujulishwa.
MBUNGE wa Kasulu Magharibi, Kilontsi Mporogomyi (CCM) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kugonga na kuua papo hapo mwenda kwa miguu ambaye hakufahamika jina mara moja.
Akimsomea mashitaka yake jana mbele ya Hakimu Mkazi Hassan Momba, Mwendesha Mashitaka wa Polisi Beatrice Nsana, alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 11 mwaka huu saa 5.30 usiku eneo la Wajenzi, mjini hapa.
Nsana alisema mtuhumiwa Mporogomyi alikuwa akiendesha gari namba T288ASJ aina ya Toyota Land Cruiser akashindwa kusimama amruhusu mwenda kwa miguu huyo avuke barabara, akamgonga.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa Mbunge huyo anakabiliwa na mashitaka mawili; kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha kifo.
Alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika; mshitakiwa alikana mashitaka na kusema hamfahamu marehemu wala makazi yake.
Mtuhumiwa alipata dhamana baada ya kukidhi masharti ya Sh milioni 5 na kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 5 mwaka huu itakapotajwa.
Source:Habari Leo.
Photo Courtesy: Tanzania Parliament Website.

Chama cha Mapinduzi(CCM) leo kimemchagua rasmi Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu mwezi Octoba mwaka huu.
Baada ya mashauriano na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Rais Kikwete amemteua Dr.Mohammed Gharib Bilal, kuwa mgombea mwenza.Kwa maana hiyo tiketi ya CCM itabebwa na Jakaya Mrisho Kikwete na Dr.Mohammed Gharib Bilal.
Dr.Gharib Bilal alizaliwa tarehe 6 Februari,1945 huko Unguja. Dr.Bilal ni mwanasayansi aliyepata stashahada ya kwanza katika sayansi ya nuklia kutoka Chuo Kikuu cha Howard nchini Marekani mwaka 1967. Alipata Masters Degree katika masuala hayo hayo ya sayansi ya nuklia kutoka Chuo Kikuu Cha California mwaka 1969 kabla ya kupata PhD katika fizikia kutoka chuo hicho hicho cha California mwaka 1976. Kuanzia mwaka 1976 mpaka mwaka 1990 alikuwa Lecturer(mkufunzi) katika Chuo Kikuu Cha Dar-es-salaam-Idara ya Fizikia
Kati ya mwaka 1990 na 1995 alikuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Sayansi,Tekinolojia na Elimu ya Juu katika serikali ya Muungano.Mwaka 1982 alikuwa Mkuu wa Kitivo Cha Sayansi,Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, aliteuliwa na Rais Salmin Amour kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar. Mwaka 2000 aligombea Urais wa Zanzibar bila mafanikio. Mwaka huu alikuwemo miongoni mwa waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM kusimama kama mgombea Urais Zanzibar lakini bahati hiyo ikamuangukia Dr.Ali Mohammed Shein.Badala yake na kwa maana hii,atasimama na Kikwete kama mgombea mwenza na hivyo,endapo watashinda,atakuwa Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano.
Photo/Francis Godwin

Makamu wa Rais wa serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania,Dr.Ali Mohamed Shein,amechaguliwa kuwa mgombea Urais-Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.
Photo/Francis Godwin

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shy-Rose Sadruddin Bhanji(pichani) ametangaza kujitosa katika nafasi ya ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam kupitia CCM na lengo lake kubwa ni kuwa kiungo muhimu katika jamii ya wanakinondoni.
Akitangaza azma yake ya kuomba ridhaa kwa wanachama wa CCM katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Shy-Rose alisema kwa mtazamo wake neno ubunge kwa mwaka 2010 linahitaji tafsiri mpya kabisa. `…kwa sasa mbunge anatakiwa kuwa ni kiungo cha jamii badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo kama ilivyozoeleka` alifafanua Shy-Rose.
`Mwaka 2010 ni mwaka wa mabadiliko na ndio maana nimeona kwamba ili kila mwananchi kuweza kuwajibika, nafasi ya mbunge inahitaji kutafsiriwa upya ili iendane na wakati na matatizo ambayo yanayotukakabili wananchi` alisema.
Kwa maana hiyo amesema kwamba hata sifa za mbunge zinahitaji kutafsiriwa upya kabisa, kwani majukumu yake yamebadilika kuendana na wakati.
Ametaja baadhi ya sifa hizo mpya ni kuwa mhamasishaji, kiungo muhimu, kufanya kazi usiku na mchana na kuwa na ofisi katika kila kata ndani ya jimbo husika ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.
`naomba nitoe tafsiri mpya ya neno ubunge..mbunge anatakiwa sasa awe ni kiungo muhimu kati ya walio na kipato kikubwa, kipato cha kati na wasio na kipato kabisa ili kwa pamoja jimbo liweze kupiga hatua za kimaendeleo. Mimi nitahakikisha kwamba nina ofisi katika kila kata ili niweze kuwafikia wananchi wangu katika kata zote kwani wakati napita kuomba kura ninawafuata na baada ya kufanikiwa kutimiza azma yangu ni wakati wa kuendelea kuwafuata na si wao kunifuata` alisema.
Kada huyo amesema sera yake kubwa itakuwa ni kumshirikisha kila mwananchi wa Kinondoni katika shughuli za kuleta maendeleo ili kila mtu aweze kutoa maoni, mawazo na mchango wa hali na mali katika kuleta maendeleo ya ukweli. Amesema hata mwananchi ambaye atakuwa hana uwezo, atabeba tofali kutoka upande mmoja hadi sehemu husika.
`nimeamua kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge kwa jimbo la hili ili niweze kuleta mageuzi makubwa sana katika jimbo la Kinondoni…naomba mfahamu kwamba kila mwananchi amebarikiwa akili, vipaji uwezo na Mwenyezi Mungu lakini asiposhirikishwa hataweza kutoa mchango wake, hivyo mimi nitahakikisha kwamba kila mmoja kwa uwezo wake na nafasi yake anachangia katika kuleta maendeleo`, alifafanua.
Shy-Rose alibainisha mambo makubwa ambayo atayapigania kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ni (more…)

Kijana aliyepo pichani bila shaka unamtambua.Kama ulikuwa ukimfuatilia kwa muda,bila shaka hutoshtuka sana kusikia uamuzi wake.Kama humtambui na unataka kujua yeye ni nani na hivi karibuni ametangaza kugombea nini,usiende mbali sana,bonyeza hapa.

Huu hapa ni ujumbe kutoka kwa Zitto Kabwe(MP)
Ndugu msomaji, nimekuwa na blogu hapo kabla lakini sikuweza kuifanyi kazi kama invyostahili. Nimeamua kuanzisha blogu hii mpya ili liwe jukwaa la kujadiliana jinsi ya kuimarisha demokrasia nchini kwetu Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Karibu kwa maoni, ushauri na hata makatazo! Bonyeza hapa kumtembelea.

HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amewatisha wafanyakazi ambao wamepanga kushiriki kwenye mgomo ulioitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) uliopangwa kuanza kesho kuwa watakumbana na mkono wa sheria endapo watathubutu kutekeleza azma yao hiyo.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana jioni jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wazee wa mkoa huo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo alisema kuwa mgomo unaoshinikizwa washiriki ni batili na kinyume cha sheria kwa kuwa umeitishwa katikati ya mazungumzo.Kwa undani zaidi wa habari hii bonyeza hapa.
Sisi tunachouliza ni Je,hapa Mheshimiwa ametumia busara zote alizonazo?CCM si ilijengwa katika misingi ya wakulima na wafanyakazi?

