MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Happy New YearBC

Happy New Year! Kheri Ya Mwaka Mpya! Naam ni mwaka 2010,karne ya 21.Binafsi napenda kukupa pongezi kwa kuumaliza mwaka 2009 na kuingia mwaka 2010.

Nakupa hongera nikiwa na sababu nyingi.Baadhi yake ni kwamba,kwa wengi mwaka 2009 ulikuwa ni mgumu kupita kiasi.Hali mbaya ya kiuchumi iliyoikumba dunia,ni sababu tosha ya kuufanya mwaka 2009 kuwa mgumu.

Isitoshe,tumepoteza wapendwa wetu wengi,ndugu,jamaa na marafiki.Mfano ni hivi leo,tunaomboleza kifo cha Mzee wetu,Rashid Mfaume Kawawa. Maradhi mbalimbali,mengine yakiwa mapya kama vile H1N1 (homa ya mafua ya nguruwe),yaliikumba dunia na kuleta mtikisiko wa aina yake.Hofu ikatanda ulimwenguni.Wengi wamepoteza maisha katika vita na mashambulizi ya kigaidi na kujitoa mhanga.

Wakati bado tunatafakari yaliyojiri katika mwaka 2009,naukumbuka msemo wa wahenga wetu.Yaliyopita si ndwele,tugange yajayo.Ni mwaka mpya na ni nafasi nyingine ya kuanza upya,kuweka malengo mapya,kumalizia ya zamani.Ni wakati wa kujipanga upya kuzikabili upya changamoto mbalimbali za maisha na ubinadamu.

Unapouanza mwaka mpya na kama unataka au umeshajiwekea malengo, kumbuka yafuatayo;

  • Orodhesha malengo yako. Tafuta mahali penye utulivu.Chukua kalamu na karatasi kisha orodhesha malengo yako.Kisha pembeni ya malengo,orodhesha mambo ambayo unatakiwa kufanya(actions) ili kutimiza malengo uliyoorodhesha.Jaribu kuorodhesha malengo machache.Kumbuka mtaka yote,hukosa yote.
  • Weka malengo halisi.Je malengo uliyoorodhesha hapo juu ni halisi? Ninaposema halisi namaanisha weka malengo yanayokabilika.Usiweke malengo yaliyozidi kiwango au yasiyotimia kimsingi.Kwa mfano,ukiweka malengo kwamba mwaka huu unataka kuwa tajiri kupita watu wote duniani wakati hivi leo akiba yako benki ni ya kiwango duni,utakuwa unaweka malengo yasiyo halisi.
  • Jiamini kwamba unaweza kutimiza lengo/malengo yeyote uliyojiwekea.Kujiamini kunaenda sambamba na imani.Ukiamini kwamba inawezekana,utaweza.Kama sio leo basi kesho.Piga taswira kichwani kwako jinsi itakavyokuwa ukitimiza malengo yako.
  • Fanya tathmini ya mara kwa mara juu ya malengo yako na mwenendo mzima wa kuyatimiza.Ukiona hauelekei kuyatimiza,usiingiwe na hofu ya kuyafanyia marekebisho.Siku hazifanani na mazingira hubadilika.Malengo pia yanaweza kubadilika.
  • Mwambie ndugu au rafiki wa karibu kuhusu malengo yako.Naelewa…unataka malengo yako ya mwaka huu yabakie siri.Ninachotaka kukuambia ni kwamba unapomwambia ndugu au rafiki yako wa karibu unayemwamini kuhusu malengo yako,unakuwa umejipatia msaada.Ndugu au rafiki huyo atakuwepo kukukumbusha au kukusaidia,kwa njia moja au nyingine,kutimiza malengo yako.Isitoshe,kwa kumwambia ndugu au rafiki,unakuwa umejitilia chachu ya kutimiza malengo yako.Utaonekanaje kama mwisho wa mwaka utakuwa hujatimiza yale uliyotaka kutimiza? Binadamu tumeumbwa na soni.Itumie.
  • Orodhesha watu wa kukusaidia. Kutimiza malengo kunaweza kuwa kitu kigumu.Unaweza kuhitaji msaada ili kutimiza malengo.Usisite kufanya hivyo.Weka mahali orodha ya watu ambao unadhani wanaweza kukusaidia pindi utakapohitaji msaada katika kutimiza malengo yako.Wengine wanaweza kukusaidia kimawazo au kimtazamo(role models).Watumie ipasavyo.
  • Jipongeze. Kutimiza lengo au malengo ni jambo la furaha.Linastahili pongezi.Kila unapotimiza lengo au malengo fulani,usisahau kujipongeza.
  • Usisahau kumweka Muumba mbele. Hata kama huna imani,huamini wala kuabudu kufuatana na dini au dhehebu lolote,bila shaka tunakubaliana kwamba yupo aliye juu,aliyetuumba.Usimsahau.

Nakutakia kila la kheri katika mwaka mpya wa 2010. Enjoy.

Xnas

Kwa niaba ya timu nzima ya BC,napenda kuchukua nafasi hii kukutakia kila la kheri katika wakati huu wa kusherekea sikukuu ya Christmas.Utumie wakati huu kuwa karibu na wale uwapendao na pia kupumzika kidogo kama inawezekana.

Pia ni wajibu wetu kukumbushana; Usiendeshe gari kama umekunywa.Ni hatari kwako binafsi,abiria wako na watumiaji wengine wa barabara.

Jizuie.Ikishindikana kabisa,tumia kinga.Tunakupenda.

Christmas Njema.

bc-logo-officialbc

Leo ni siku ya furaha. Ni siku ya kufurahi na kutafakari. BC imetimiza miaka miwili hivi leo tangu ianzishwe! Ni vigumu kuamini kwamba siku na miaka zinakwenda kwa kasi ya namna hii.

Hatuna mengi ya kusema hivi leo zaidi ya kukushukuru wewe mtembeleaji na mchangiaji wa BC. Mtandaoni zipo blogs nyingi sana na katika lugha mbalimbali ikiwemo hii yetu ya Kiswahili. Lakini kwa sababu umechagua kila mara kututembelea na kuchangia mawazo na mtizamo wako hapa, hatuna budi kukushukuru sana sana.Tunaamini kwamba hiyo ni kwa sababu unaipenda BC na unathamini mchango wake katika ulimwengu wa habari na mawasiliano. Asante sana. Shukrani nyingi pia ziwaendee ninyi nyote ambao mara kwa mara mmekuwa aidha vyanzo vya habari zetu,burudani zetu. Pia shukrani kwa wale ambao wamekuwa wakitukosoa pale tunapoteleza. Tungependa kukuhakikishia kwamba tunathamini sana michango hiyo ikiwemo kukosolewa.

Pamoja na hilo, BC kama mojawapo ya vyanzo vya habari au kisima cha kusambaza habari, si kitu bila ushirikiano wa vyombo vingine vya habari na mawasiliano. Kwa hali hiyo ni lazima na sharti tuseme shukrani nyingi sana kwa vyombo vyote vya habari nchini Tanzania zikiwemo radio,magazeti na hata luninga.

Juu ya yote shukrani sana kwa bloggers wenzetu.Bila ninyi kazi ingekuwa ngumu maradufu.Asante sana.

Tunauanza mwaka mwingine. Kama ambavyo umeshuhudia katika kipindi kilichopita, kikubwa ambacho tunajaribu kujitahidi nacho ni kuboresha kazi zetu. Ni kazi kubwa na yenye gharama zake lakini tumedhamiria kuifanya kwa sababu tunathamini na kuamini katika ulimwengu huru wa habari na mawasiliano. Asanteni.

dar-explosionImekuwa ni wiki ngumu kwa watanzania hususani waishio jijini Dar-es-salaam na zaidi waishio maeneo ya Mbagala. Milipuko kadhaa ilitetemesha jiji.Hofu ikatanda. Ikawa mshikemshike Mbagala kwenyewe mpaka katikati ya jiji na maeneo mengine. Wengine wakajua vita nyingine labda ndio imeshawadia.Penye wengi pana mambo mengi. Maneno mitaani nayo yakazidi. Hofu ikawa hofu.

Wananchi kadhaa ambao walikuwa katika siku yao ya kawaida,ya mihangaiko ya kawaida ya maisha wakapoteza maisha. Ama kweli kifo kikija hakipigi hodi! Ndio maana tunaambiwa kila siku kwamba tujiandae. Wengi wengine wakajeruhiwa. Wengi bado wapo mahospitalini.

Vifo vinapotokea au maafa ya namna hii, huwa ni wakati wa simanzi kubwa. Kifo ni kitu cha mwisho ambacho binadamu yeyote anataka kukabiliana nacho.Kinaogopesha. Lakini kifo ni sehemu inayokwenda sambamba kabisa na maisha. Ni sehemu ya maisha na sote tutapitia njia hiyo hiyo.Tunachoweza kufanya ni kutoa pole tu kwa wote walioondokewa na wapendwa wao. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi! Pole nyingi pia ziwaendee wote waliojeruhiwa.Ni matumaini yetu kwamba Mwenyezi Mungu atawaponya na kukupeni tena afya njema.

Nini kilitokea? Ni ajali au uzembe tu wa mtu au watu fulani? Kama ni uzembe je walioathirika aidha kwa kuumia au kupoteza ndugu,jamaa na marafiki watafidiwa? Je tunavyo vitendea kazi na watendaji wa kutosha kutupatia majibu ya maswali hayo? Hayo ni baadhi ya maswali ambayo serikali ni lazima iyapatie majibu yanayoeleweka,ya wazi bila kificho. Tusipofanya hivyo,kesho bado ni tete. Yanaweza kutokea tena na tena matukio kama hili la wiki hii. Kama hali ile ilitokana na uzembe wa mtu au watu,basi hatua kali zichukuliwe. Ni wakati mwingine muafaka kwa serikali kuonyesha jinsi “inavyowajibika” kwa wapiga kura,walipa kodi na wananchi wake kwa ujumla.

Naam,kwa sababu leo ni Ijumaa na kawaida ni kwamba huwa tunaburudika na zilipendwa na kutokana na hali ya majonzi tuliyonayo,kibao cha Dr.Remmy Ongala cha Kifo ndicho ambacho nadhani ni muafaka. Kimsingi kibao hiki sio cha kuburudisha bali kutusaidia kuungana na wenzetu waliopoteza ndugu,jamaa na marafiki katika maombolezo.

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Leo pia ni Mei Mosi. Ni sikukuu ya Wafanyakazi katika sehemu nyingi za ulimwenguni ikiwemo Tanzania yetu. Nachukua nafasi hii kukutakia wewe mfanyakazi na watanzania wote kwa ujumla sikukuu njema.

bc-makassyWeekend hii,watanzania sehemu mbalimbali za dunia wataungana kusheherekea Sikukuu ya Muungano.Ni miaka 45 sasa imepita tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana! Kama hujaalikwa mahali kusheherekea Sikukuu ya Muungano basi tambua kwamba umejitenga sana na watanzania wenzako.Huna budi kurejea kwa wenzako kwani hata ukiendelea kukataa,wewe bado ni mtanzania.Isitoshe mkataa kwao ni….

Sasa kama ilivyo kwa miungano mingine yeyote ikiwemo hata ile ya binafsi kama vile ndoa,haikosi kasoro zake.Migogoro hutawala nyakati zingine.Kila mmoja,kwa njia moja au nyingine,huona kwamba mwenzake anampunja,anamuonea.Anadhani au kuamini kwamba angekuwa peke yake angefanya vizuri zaidi nk.Anasahau nguvu ya umoja.Anaota ndoto zake mwenyewe.Shauri yake,shauri yao.Na mara nyingi huwa tunabobea katika kutoa kasoro tu bila kuangalia yaliyo mema.Kwa vyovyote vile yapo mafanikio ya Muungano.Zipo kasoro pia.Lakini je kasoro zinazidi mema au mafanikio?Lazima tuketi chini na kujiuliza.Tukipata jibu tunaweza kuendelea na malumbano yetu ya kawaida kuhusu muungano.Tutakuwa na pa kuanzia na kuishia ikibidi.

Katika kuadhimisha sikukuu hii,nimeona nikuwekee kibao kinachoitwa Muungano. Ni kutoka kwao Orchestra Makassy.Nakutakia weekend njema na sikukuu njema ya Muungano.

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

pasakabc

Ni majira ya Pasaka.BC inapenda kukutakia msimu mwema wa Pasaka.Tumia muda huu kujumuika na ndugu,jamaa au marafiki.Tumia muda huu kwa toba na mapumziko.Pasaka Njema.

BC itakuwa mapumzikoni kiduchu!

womens_day_greeting

Leo ni siku ya Wanawake Duniani(Women’s Day).Ni siku ambayo husheherekea mafanikio na mchango wa wanawake katika nyanja zote za maendeleo ya binadamu iwe ni kiuchumi,kijamii au kisiasa.Ni siku ambayo inatukumbusha sote umuhimu wa kipekee wa wanawake duniani.Hapa tunawazungumzia mama zetu,dada zetu,wake zetu,watoto wetu,shangazi zetu,binamu zetu,majirani zetu wanawake,marafiki zetu,maadui zetu nk.

Mwanamuziki maarufu kutoka nchini Marekani,James Brown, aliwahi kuimba “It’s A Man’s World but It Would Be Nothing Without a Woman”. Hilo halina ubishi.Dunia tuionayo leo kama dunia,inatokana na mchango mkubwa wa wanawake.Dunia si dunia bila mwanamke.Haipo.

BC inaungana na wote katika kusheherekea siku hii na pia kuwasihi wanawake,popote pale ulimwenguni, waendelee kufanya ambacho wamekuwa wakikifanya tangu mwanzo wa dunia hii.Happy Women’s Day.

Mtizame James Brown na Luciano Pavarotti hapo chini wakiimba Its A Man’s World.Mungu azilaze roho zao mahali pema.

You need to a flashplayer enabled browser to view this YouTube video

valentino

Leo ni siku ya wapendanao duniani au maarufu kama Valentine’s Day.Ni sikukuu ambayo zamani ilikuwa ya “kimagharibi” zaidi kabla ya kuenea ulimwenguni kote.Sina mengi sana zaidi ya kuwaambieni wasomaji na watembeleaji wote wa BC kwamba tunawapenda na tunawatakia sikukuu njema.Enjoy!

header1

Hatimaye siku 365 za mwaka 2008 zimefikia ukingoni.Ninavyoandika ujumbe huu tayari kuna sehemu mbalimbali za dunia ambapo tayari sekunde za mwisho za mwaka huu zimeshahesabiwa na tayari takwimu mpya zimeshaandikwa.Kwa maana hiyo leo ni mwaka mpya. Kwa heri mwaka 2008 karibu mwaka 2009.Kwa wengi leo huwa ni siku nzuri kwa maazimio mapya ndani ya matumaini mapya.Kwa jinsi hali ya uchumi duniani ilivyoishia mwaka tunaoupa kisogo,basi sio ajabu kwamba malengo ya wengi ni kulinda zaidi mifuko yetu kwa kuwa makini zaidi na matumizi hesabu za mapato na matumizi na pia kulinda zaidi kazi zinazotuingizia kipato.Nakutakia kila la kheri katika hilo.

Bila kujali hali ya kiafya,kiuchumi,kisiasa wala kijamii, ukweli kwamba mwaka mpya umewadia huku wewe na sisi sote hapa BC tukiwa hai, ni jambo la kufurahia na kumshukuru Muumba.Ukivuka mwaka unakuwa umeandika historia mpya katika maisha yako. Vitabu vya kumbukumbu vitaandika kwamba uliuona mwaka 2009! Ni jambo la kumshukuru muumba kwani ni wazi wapo wengi sana waliotamani kuuona mwaka huu na wasifanikiwe.Kama huamini, fikiria kidogo tu ni watu wangapi ambao umehudhuria mazishi yao au kusikia habari juu ya misiba yao?Unaona? Hatuna budi kumshukuru Mungu.

Wakati huu tunapoingia mwaka mpya wa 2009,tungependa kwanza kukutakia kila la kheri wewe msomaji,mtembeleaji au mchangiaji wetu.Mwenyezi Mungu akuongoze na kukubariki katika kila jambo utakalolifanya ndani ya mwaka huu wa 2009.Kama mwaka 2008 haukuwa wenye mafanikio kwako au haukutimiza malengo yako,usikate tama.Fungua ukurasa mpya huku ukiwa na fikra chanya zaidi na utaona mabadiliko.

Tungependa pia kukupa shukrani zetu za pekee kwa kuwa mtembeleaji,msomaji au mchangiaji mzuri wa BC.Kama kuna mafanikio yoyote ambayo tumeyapata tangu kuanzishwa kwa blog/site hii,ni wazi kabisa kwamba mafanikio hayo yametokana na mchango wako wewe msomaji,mtembeleaji na mchangiaji wetu.

Shukrani nyingi ziwaendee celebrities mbalimbali ambao bila maringo,kinyongo wala ngendembwe walikubali aidha kufanya nasi mahojiano au kutokuwa na kinyongo nasi pale tulipoweka picha zao na kukaribisha mvua ya maoni kutoka kwa wasomaji huku wengine wakiwa chanya na wengine hasi.Celebrities kama hao wanakuwa wametambua vyema nafasi au mchango wao katika jamii.Wametambua pia kwamba haiwezekani kuwa bondia ulingoni halafu ukawa unaogopa ngumi za uso.Tunawashukuru na kuwaomba tuendelee kushirikiana.

Shukrani za pekee ziwafikie bloggers wenzetu mbalimbali,vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Tanzania,wapiga picha mbalimbali na wengineo wote ambao wanaendelea kushirikiana nasi katika jukumu hili zito la habari na mawasiliano.Asanteni sana.Bila ninyi,haiwezekani.BC inathamini sana mchango wenu.

Kama binadamu inawezekana kabisa kuna wakati tunatokea kutoelewana au hata kukwazana.Bila shaka hata sisi hapa BC inawezekana kuna wakati tulikukwaza.Yawezekana hatukuweka maoni yako kwa sababu moja au nyingine,yawezekana tulichelewa kuruhusu maoni yako yaonekane,yawezekana wewe ni celebrity na tuliruhusu maoni ambayo kimsingi uliona kama umetusiwa nk.Mifano ipo mingi.Lakini kwa wote hao,tunaomba samahani.Yote hayo ni katika kujitahidi kuitenda vyema kazi yetu.

Tunapouanza mwaka mpya wa 2009,tunakusihi uendele kututembelea,kuchangia,kutukosoa tunapokosea na pia kumwambia mwenzako kuhusu uwanja huu ili naye asipitwe na yanayojiri.Tunakutakia kila la kheri.HAPPY NEW YEAR 2009.

comedi-orijinobc

Naam!Xmas kwa mwaka 2008 ndio imeshaisha.Kwa bahati mbaya siku kama hizi huwa hazirudi tena.Ilivyokuwa Xmas mwaka huu sivyo itakavyokuwa mwaka ujao na mingine itakayofuata.Ulipokuwa mwaka huu si ajabu hutokuwepo mwakani.Ndio maana huwa tunasisitiza kwamba Make The Most Use of It when/whenever you can(nimetia kizungu hapo kuonyesha msisitizo).

Najua wengi wenu bado mpo kwenye hali ya sikukuu.Wengine nasikia bado wanatibu mning’inio wa ziada(hangover).Kwa wengine huu ni wakati wa kutafakari jinsi matumizi yalivyokwenda.Ni wakati wa kukagua risiti huku macho yakiwa yamekutoka na simanzi likiwa limetanda usoni.Usijali,ndio maisha.Si ushasikia ule msemo usemao Ponda Mali kwani Kufa Kwaja?Sasa?

Lazima pia nikiri kwamba hata sisi wenyewe tupo kwenye holiday mood bado.Ndio maana mwendo kidogo unakuwa taratibu ingawa sio kama wa kinyonga.Bahati nzuri hatubadiliki rangi pia.Tunajongea huku tukiandaa mambo makubwa zaidi kwa ajili ya mwaka ujao ambao kimsingi tunataka uwe mwaka wa BC!

Sikukuu ilikuwaje?Uliserebukia wapi?Mambo yalikwendaje?Tungependa kusikia kutoka kwako msomaji.Wakati unatafakari jinsi sikukuu ilivyokwenda,hatungependa kukuacha hivi hivi.Burudika na wimbo Ndoa Fungo la Imani kutoka kwa Bima Lee.Pata burudani

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Tumeshindwa kupata maelezo au caption ya hiyo picha.Unaweza kutusaidia?

Read the Next Page →

↑ Go Back to Top of Page