Ninapoandika post hii,Afrika Kusini wapo uwanjani wakimenyana na Mexico.Wanaongoza goli 1-0.
Kwa bahati mbaya,Mzee Madiba ameshindwa kuhudhuria ufunguzi wa fainali hizo kutokana na kifo cha kitukuu wake,Zenani Mandela,kilichotokea jana usiku kwa ajali ya gari.

(AP Photo/Nelson Mandela Foundation, Debbie Yazbek)
Pichani juu ni Mandela na wajukuu zake.Kutoka kushoto ni Thembela Mandela,Zenani Mandela(aliyefariki) na Mbuso Mandela.
Unaweze kutizama video kidogo ya Mandela na kitukuu wake aliyefariki kwa kubonyeza hapa.
UPDATE: Mchezo kati ya South Africa na Mexico umekwisha.Matokeo ni 1-1. Goli la South Africa lilifungwa na Siphiwe Tshabalala kunako dakika ya 55.Mexico walisawazisha kunako dakika ya kwa goli rahisi lililofungwa na Rafael Marquez kunako dakika 79.
Kiungo mchezeshaji wa Timu ya Taifa ya Soka ya Ghana na klabu ya Chelsea ya Uingereza,Michael Essien(pichani), atazikosa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Chama cha Soka cha Ghana(GFA),kiungo huyo ambaye kwa muda sasa amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya goti,hatoweza kupona mpaka hapo mwishoni mwa mwezi wa saba(Julai) na hivyo kumaliza kabisa matumaini ya kuweza kucheza katika fainali hizo.
Uamuzi wa mwisho wa kumuondoa Essien katika kikosi cha Ghana(Black Stars) ulifikiwa na chama hicho cha soka kwa kushauriana kwa karibu na timu yake ya Chelsea pamoja na daktari wake na pia madaktari wa Timu ya Taifa ya Ghana.
Pamoja na kwamba hatocheza,habari zinazidi kupasha kwamba Michael Essien ataambatana na timu hiyo kwenda Afrika Kusini na kwamba atasaidia katika masuala mengine ya kiufundi.Ghana wapo kundi D pamoja na Ujerumani, Australia na Serbia. Wataingia uwanjani kwa mara ya kwanza tarehe 13 Juni kupambana na Serbia.
Hii ingekuwa mara ya pili kwa kiungo huyo kucheza katika fainali za Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo miaka minne iliyopita katika fainali zilizofanyikia nchini Ujerumani. Je,Ghana wataweza kufanya vizuri bila kiungo wao mahiri Michael Essien?
Zimebaki takribani siku 15 kabla kipute cha kugombea Kombe la Dunia la Soka hakijaanza huko nchini Afrika Kusini au “bondeni” kama ambavyo wengine wanapaita.
Jumla ya timu 32 zinashiriki fainali za kombe la dunia la mwaka huu ambazo kwa mara ya kwanza kabisa,zinafanyikia barani Afrika. Wawakilishi wa bara la Afrika katika fainali za mwaka huu ni wenyeji Afrika Kusini, Nigeria, Ghana,Ivory Coast, Cameroon na Algeria.
Licha ya hii kuwa mara ya kwanza kwa nchi yeyote ya bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, hakuna timu ya Afrika iliyowahi kuchukua ubingwa au hata kufikia nusu fainali.Mafanikio ambayo bara la Afrika linajivunia nayo mpaka hivi leo ni kufikia hatua ya robo fainali ambapo Senegal(ilifika hatua ya robo-fainali mwaka 2002 kabla ya kutolewa na Uturuki kwa goli kwa 1-0) na Cameroon(mwaka 1990 ilifikia hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa na Uingereza kwa jumla ya goli 3-2)
Wachambuzi mbalimbali wa soka hawaipi Afrika nafasi ya kufanya vyema japokuwa ni wenyeji kwa sababu mbalimbali kama vile kuwa katika makundi magumu;mfano hapa unatolewa kwa kundi G ambalo ndani yake kuna Ivory Coast,Brazil,Portugal na Korea Kaskazini. Wengi hawaipi Ivory Coast nafasi ya kuendelea raundi ya pili na kwa maana hiyo kuziacha ama timu za Brazil na Portugal ambazo zinapewa zaidi nafasi ya kusonga mbele.
Sababu zingine zinazotolewa ni ukosefu wa uzoefu(Ghana na Ivory Coast zinashiriki kwa mara ya pili wakati Algeria inashiriki kwa mara ya tatu baada ya kutofanya hivyo kwa muda mrefu)
Pamoja na hayo, kwa upande mwingine wale wanaozipa nafasi timu kutoka barani Africa wanajitia moyo wa ushindi kwa sababu ukweli ni kwamba bara la Afrika lina wachezaji lukuki katika ligi za Ulaya jambo ambalo linatuhahakishia kwamba timu za Afrika zilizofuzu zinao wachezaji wengi tu wenye ufundi na uzoefu(skills and experience) na mikikimikiki ya mashindano makubwa kama ya Kombe la Dunia.
Je, Africa tutacheka au tutaendelea kulia na kununa? Miongoni mwa timu hizi ambazo picha zake zipo hapo chini ni ipi ambayo unaishabikia? Ni ipi ambayo unaipa nafasi ya juu kufanya vyema zaidi kuliko zingine? Kwanini unaipa nafasi hiyo?

South Africa

Cameroon

Algeria

Ivory Coast

Ghana

Nigeria
Editor’s Note: World Cup 2010 ni tukio kubwa na la kipekee ambalo bila shaka litafuatiliwa na mabilioni ya watu ukiwemo wewe msomaji na mtembeleaji,msomaji na mchangiaji wetu.Kwa kutambua hilo,BC itakuwa,kwa msaada na ushirikiano wa wapenzi,wataalamu na wafuatiliaji wa soka,itakuwa ikikuletea chambuzi mbalimbali kuhusu fainali hizi.Asanteni

Taifa Stars

Brazil
Brazil are to play Tanzania on 7 June in a World Cup warm-up match ahead of this summer’s finals in South Africa.
The Brazilians have become the first non-African team to schedule a friendly in Africa in the build-up to the tournament, which kicks off on 11 June.
Tanzanian Football Federation (TFF) spokesman Florian Kaijage told BBC Sport that a contract would be signed within the next two to three days. For more information,click here.
Klabu ya Simba maarufu kama Watoto wa Msimbazi au Taifa Kubwa,wamepata mwenyekiti mpya wa klabu yao.Si mwingine bali ni Ismail Aden Rage(pichani) ambaye sio jina jipya katika medani ya soka nchini Tanzania. Aliwahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini Tanzania katika zama ambazo ziligubikwa na rushwa na matumizi mabaya ya fedha kitu ambacho kilipelekea Rage kushtakiwa na kutiwa ndani.Kwa habari zaidi na picha kuhusu uchaguzi huu bonyeza hapa.

Machupa ni mfungaji hodari. Usemi huo pekee unatosha kumuelezea Athuman Iddi Machupa (pichani) mshambuliaji kijana ambaye kwa upande wa Tanzania, aliwika zaidi alipokuwa akichezea timu ya soka ya Simba maarufu kama “Watoto wa Msimbazi”.
Hivi leo Machupa anasakata kabumbu nchini Sweden akiwa na timu ya Vasalund IF.
Niliwasiliana na Machupa hivi karibuni na kumuuliza maswali machache. Haya hapa mahojiano yetu;
BC: Mpaka sasa mambo yanakwendaje hapo Sweden?Unachezea timu gani na ipo daraja la ngapi?
Machupa: Kwa upande wangu hapa Sweden maisha yanakwenda poa kaka.Ninachezea timu inayoitwa Vasalund IF ilikuwa katika ligi ya Superettan (ligi ya pili kwa ukubwa hapa Sweden) lakini kwa bahati mbaya tumeshuka daraja hadi la kwanza..
BC: Umeshakaa Sweden kwa muda wa kutosha sasa.Unapaonaje na zaidi unaonaje nafasi za kuendeleza soka lako?
Machupa: Kwa sasa kaka napeleka mwaka hapa na kwa upande wangu mi naona maisha ni mazuri na hata nafasi ya kusonga mbele kwangu ni kubwa mno.Nazidisha bidii katika kila kitu na inshallah nitafanikiwa zaidi na zaidi.
BC: Kama mgeni katika nchi ya watu,ni mambo gani ambayo ilibidi ukabiliane nayo kwanza? Hapa nazungumzia mambo kama vile lugha,vyakula nk
Machupa: Of coz lugha kaka ni ngumu. Lakini nashukuru jamaa wamenishughulikia masuala yote ya muhimu ikiwa ni pamoja sehemu ya kujifunza lugha yao.Na kuhusu chakula; kwa kusema ukweli ni kizuri tu. Hakina tofauti sana na cha nyumbani Tanzania kwa sababu najipikia mwenyewe chakula ninachojisikia kula.Hali ya hewa nayo ilikuwa changamoto lakini taratibu ninazoea.
“Hebu ngoja nicheki kama vitu vishaiva”
BC: Una ujumbe gani kwa vijana wengine wanaosakata soka nyumbani Tanzania?
Machupa: Ujumbe wangu kwa vijana wanaosakata soka na hususani waliopo nyumbani ni kwamba waheshimu soka kwani soka ni kazi kama zilivyo kazi zingine zozote.Ukiheshimu soka hakika utafanikiwa.
BC: Mwakani ni mwaka wa kombe la dunia.Safari hii kipute kipo Africa.Nini matarajio yako kwa nchi za Afrika?
Machupa: Ni changamoto kubwa kwa timu za Africa ambazo zimefanikiwa kuingia katika finali hizo. Tusubiri tuone kwa sababu nina uhakika watajiandaa vizuri. Nina uhakika hatutosikia madai ya posho. Nina imani watatuwakilisha vyema kabisa,sina wasiwasi na hilo. Ila nahisi Ghana watafanya vizuri. Nawa-support.
Machupa akiwa mazoezini na timu yake.Anaonekana kulia katika picha akijaribu kutuliza mpira chini.
BC: Una lolote la kuongeza kwa mashabiki wako?
Machupa: Mashabiki ndio kila kitu.Nawapenda na ninawaheshimu sana na hakika bila wao hatuwezi songa kwa sababu wao ndio wanaotukosoa pale tunapokosea.I love all my fans popote walipo.

Kombe la Dunia lipo ziarani nchini Tanzania. Ziara hiyo imezinduliwa rasmi leo jioni nchini Tanzania na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Ziara ya kombe hilo katika sehemu mbalimbali duniani, ni ishara ya kuwapa fursa mashabiki mbalimbali wa soka ulimwenguni,nafasi ya kuliona kombe hilo “live” na hata kupiga nalo picha kwa kumbukumbu nk. Hizo zote ni miongoni mwa shughuli mbalimbali kuelekea South Africa 2010.
Wakati nikimuangalia Rais Kikwete akiwa amejawa na tabasamu wakati akilinyanyua kombe hilo na kulibusu,nilijiuliza, hivi itakuja tokea kweli siku moja Rais wa Tanzania(yeyote yule atakayekuwa madarakani) kulinyanyua Kombe la Dunia baada ya kulipokea toka mikononi mwa nahodha wa Taifa Stars baada ya kulitwaa?
Well…naamini kila kitu kinawezekana. Sina tu uhakika kama tuna mipango madhubuti(ya mbali au karibu) ya kutimiza ndoto hizo.Tusiishie tu kuliona kombe kwa mbali au kulinyanyua pale tusipostahili.
Picha/Yahya Charahani

Hivi karibuni,tajiri bilionea mmiliki wa timu maarufu ya soka ya Chelsea FC ya nchini Uingereza, Roman Abramovich, alitinga nchini Tanzania na akiwa na nia ya kutalii na kuupanda mlima mrefu kupita yote barani Afrika yaani Mlima Kilimanjaro.
Safari ya Bilionea Abramovich kuja kupanda Mlima Kilimanjaro ilikuwa ni habari kubwa iliyoripotiwa na vyombo lukuki vya habari hususani nchini Tanzania na Uingereza.Kilichoifanya habari hiyo kuwa kubwa hakutokani tu na ukweli kwamba Abramovich ni miongoni mwa watu matajiri sana ulimwenguni bali pia ni ule uhusiano uliopo miongoni mwa mchezo wa soka ulimwenguni huku mashabiki wa timu ya Chelsea anayoimiliki Abramovich ya Chelsea ikiwa na mashabiki kibao ulimwenguni wakiwemo pia wale wanaoishi na kuitazama timu hiyo kutokea Tanzania.
Ingawa Roman Abramovich hakufika kileleni, ni wazi kwamba,kwa namna moja au nyingine,amesaidia kuinua soko la utalii la Tanzania na hususani upandaji wa Mlima Kilimanjaro.
Lakini ni nani aliyemuongoza njia Roman Abramovich? Kuna wadadisi wameuliza swali hili na tuna furahi kwamba jibu lake tumelipata. Aliyekuwa guide wa Roman na rafiki zake anaitwa Isaac Kitindi(pichani juu ndiye anayeonekana kushoto akiwa na Roman.
Isaac ni Mhitimu wa Advanced Diploma katika masuala ya Wildlife Management kutoka Chuo cha Elimu na Utawala wa Wanyamapori cha Mweka kilichopo Moshi,Kilimanjaro. Isaac alikuja Tanzania maalumu kwa shughuli ya kumsindikiza Roman Abramovich mlimani kwani hivi sasa anasomea masuala ya Huduma ya Kwanza (First Aid Training) katika chuo kikuu maarufu cha Havard nchini Marekani.
Isaac Kitindi ambaye wenzake hupenda kumuita Mountain Madness kutokana na umahiri wake wa kuupanda Mlima Kilimanjaro hivi sasa yupo njiani kurejea Havard huku kukiwa na habari kwamba atapitia nchini Uingereza ambapo ataonana tena na Roman Abramovich kwa mazungumzo ya kuileta Tanzania timu ya Chelsea FC hapo mwakani.
Ukitaka kujua ilikuwaje mpaka Roman Abramovich akashindwa kufika kileleni,bonyeza hapa.

Mshambuliaji hatari wa timu ya soka ya Yanga, Mrisho Ngassa hapo jana alijipatia “jiko”. Amemuoa Latifah Abdulhaman. Ndoa ilifungiwa huko Tabata Kisiwani.
Hivi karibuni Ngassa alikuwa nchini Uingereza kufanya majaribio ya kuchezea timu ya West Ham. Habari zinapasha kwamba sehemu ya kwanza ya majaribio hayo ilikwenda vizuri na kwamba kunako majaaliwa Ngassa atarejea tena nchini Uingereza kwa majaribio mengine.
BC inawatakia Mr.& Mrs Ngassa kila la kheri katika ndoa yao.
Photo/Michael Jamson via Charaz

Tuende mbele turudi nyuma,ukipata nafasi ya kuchezea Yanga au Simba basi suala la umaarufu au u-celebrity halina mjadala sana.Wapo watu lukuki ambao watalijua jina lako,wataitambua sura yako na ukiwa mitaani watapenda kupiga japo stori kidogo na wewe.Ndio maana zinapokuja habari kwamba ama Yanga au Simba wametwaa ubingwa nchini,basi hiyo huwa ni habari kubwa iwe mtaani au kwenye vyombo vya habari.Mpaka hivi leo mchezo wa Yanga na Simba huwa ni gumzo kubwa mtaani.
Kwa bahati nzuri au mbaya,safari hii ni Yanga tena.Yanga wameutwaa ubingwa wa ligi ya soka nchini Tanzania kabla hata ya ligi hiyo kumalizika.Kwa maana hiyo wanastahili pongezi.
Lakini ubingwa wa soka nchini Tanzania,umaarufu,pesa nk vinakuwa na raha yake kama angalau vitakumbuka walipolala na kuamkia mashabiki wao.Tumekuwa tukiona jinsi ambavyo wanamichezo katika nchi zilizoendelea wanajitolea kwa namna mbalimbali ili kuboresha jamii zilizowazunguka na pia mashabiki wao.Wengi wanajitolea kwa namna mbalimbali kama vile kujitolea muda wao,pesa zao,ujuzi wao .Kama sio hivyo, basi wamekuwa wakijitolea katika aidha kuhamasisha michango ya hiari,kujitegemea,kujiamini miongoni mwa vijana nk.
Nchini Marekani kuna kitu kinaitwa NBA Gives Back.Hawa ni wachezaji wa ligi ya mpira wa kikapu ya Marekani ya Kaskazini waki-toa chochote wanachoweza au walichopata kwa jamii zao,kwa mashabiki wao.Wachezaji wenye majina nchini Tanzania,wanaweza kuiga hili.Wadhamini wa ligi hiyo,Vodacom,wanaweza kuhamasisha hili kwa kuwatumia wachezaji wa ligi ya soka Tanzania.Shirikisho la Soka nchini linaweza kusimamia au kuongoza harakati kama hizo.
Tusiishie kwenye kufurahia tu Ubingwa bila kukumbuka walikolalia au kuamkia mamilioni ya mashabiki wa soka nchini.Lakini mbali ya yote,BC inatoa Hongera kwa Yanga!


