Mchezaji wa timu ya Manchester City mwenye makeke na ukorofi unaokera mara nyingine,Mario Balotteli amefungiwa na Chama cha Soka Uingereza kucheza mechi nne baada ya kumpiga/kumchezea faulo mchezaji wa Tottenham, Scot Parker.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya mwamuzi wa mchezo kurudia mkanda wa mchezo huo.. Mmoja wa viongozi wa Man City amesema bado hawajakutana ili kuzungumzia suala hlo na kuangalia namna ya kukata rufaa.

Hii ni kwa mujibu wa Gazeti la  The Sun la Uingereza

Mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Cameroon,Samuel Eto’o ambaye hivi sasa anachezea timu ya Anzhi Makhachkala ya huko Urusi amesema hana tena mpango wa kuhamia kwingine na kwa maana hiyo atamalizia career yake katika medani ya soka akiwa na timu hiyo.

Samuel Eto’o ,kapteni wa Timu ya Taifa ya Cameroon,mchezaji anayelipwa mshahara mnono kushinda wote duniani na ambaye sasa ana umri wa miaka 30 anasema, ” Nina furaha kucheza hapa Anzhi na nimejipanga kushinda kitu kikubwa nikiwa na timu hii.Labda kwenye Ligi ya Mabingwa kama tukiwa na bahati ya kutosha.Natumaini kucheza kama miaka mitano au sita zaidi nikiwa hapa kabla sijatundika viatu vyangu”

Habari hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la NFP

Manny Pacquiao

Floyd Mayweather

Hivi karibuni bondia kutoka nchini Marekani,Floyd Mayweather,alizua balaa la mtandaoni pale alijitoa mhanga kupitia mtandao wa Twitter alipotuma ujumbe ambao moja kwa moja ulikuwa umeelekezwa kwa bondia mpinzani wake,Manny Pacquiao.Katika ujumbe wake,Floyd Mayweather aliandika “Nakuita,tupigane tarehe 5 Mei,tuipe dunia inachotaka kuona

Kilichofuata baada ya hapo ni kusubiriwa kwa majibu kutoka katika kambi ya Manny Pacquiao. Sasa muda mfupi uliopita wamesema kwamba wapo tayari kupigana na Mayweather lakini sio katika tarehe hiyo ya Mei 5 kama anavyotaka Mayweather.

Katika majibu ambayo yametolewa na mshauri wa masuala ya kifedha wa Manny, kambi hiyo inasema wao wanasubiri kwanza uwanja/ukumbi ambao unamaliziwa kujengwa wenye uwezo wa kuingiza watu 45,000 huko Las Vegas

Mshauri huyo,Michael Koncz,anasema “Ni upuuzi katika msimamo wa kibiashara kupeleka pambano la Manny na Mayweather katika ukumbi mdogo wakati kuna uwezekano wa kupigania katika ukumbi mkubwa”.

Mayweather yupo tayari kupigana tarehe 5 Mei katika ukumbi maarufu wa MGM Grand Garden baada ya Jaji kusogeza mbele tarehe yake ya kuanza kutumikia kifungo baada ya kupatikana na hatia katika kesi iliyokuwa inamkabili.Alihukumiwa kwenda jela kwa siku 87 lakini kuna uwezekano mkubwa akatumikia sehemu ndogo tu ya kifungo hicho.

Ukumbi wa MGM Grand Garden una uwezo wa kuingiza watu 17,000 tu na hivyo kuwa na uwezo wa kuingiza takribani dola milioni 20($20 million) wakati endapo pambano hilo litafanyikia katika ukumbi mkubwa zaidi kuna uwezekano wa kuingiza dola milioni 30 zaidi(additional $ 30 million)

Katika mahojiano mengine ambayo Manny amefanya na chombo kingine cha habari huko Ufilipino,amesema endapo Mayweather atakubali kwamba wagawane fedha nusu kwa nusu(50-50) basi yeye hana tatizo na anaweza kupigana naye tarehe hiyo.

Sisi kama mashabiki hatuna budi kusubiri kuona.Kinachotokea hivi sasa ni masuala ya kiuchumi zaidi yaliyo nyuma ya pazia la mpambano huo unaosubiriwa kwa hamu sana na mashabiki wa ndondi ulimwenguni kote.

 


Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa ameteua wachezaji 28 kuunda kikosi hicho kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chalenji inatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Novemba 25 mwaka huu.

Wachezaji walioteuliwa ni Juma Kaseja (Simba), Deo Munishi (Mtibwa Sugar) na Shabani Kado (Yanga). Mabeki wa pembeni ni Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).

Mabeki wa kati ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United). Viungo ni Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Haruna Moshi (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Rashid Yusuf (Coastal Union), Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars) na Mohamed Soud (Toto Africans).

Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Gaudence Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Daniel Reuben (Coastal Union) na Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada).


Upo uvumi kwamba mchezo wa ngumi za kulipwa ulimwenguni siku hizi umepoteza umaarufu uliokuwa nao tangu enzi za kina Mohamed Ali na kisha enzi za kina Mike Tyson,Lenox Lewis na wengineo. Upande unaopingana na hoja hiyo unadai kwamba wanamasumbwi wa leo kama vile kijana mwenye mbwembwe za aina yake,FLOYD Mayweather Jnr bado ni kivutio kikubwa katika mchezo huo ambao unaaminika kuwa wa pili kwa umaarufu baada ya mchezo wa soka.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mshawasha ambao umeshaanza kulipamba pambano linalotarajiwa kupigwa wiki ijayo tarehe 17 Septemba,2011 kati ya Floyd Mayweather na Victor Ortiz

Atapambana na Victor Ortiz kuwania ubingwa wa dunia wa WBC uzani wa welter mjini Las Vegas wiki ijayo.

Pambano hilo litaonyeshwa katika Primetime na Mayweather anatarajia kuweka kibindoni pauni milioni 25 kwa kupitia televisheni hiyo.Je,ni kweli mchezo wa ndondi umepoteza umaarufu?Subiri tuone wikienda.

Mcheza Soka wa Kimataifa,Nazir Khalfan,ambaye yupo nchini baada ya kuitumikia nchi yake katika mchezo kati ya Tanzania(Taifa Stars) na Algeria,hapo jana alipata nafasi ya kumtembelea Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Dar-es-salaam ili kumsalimia na kumpa shukrani kwa jinsi ambayo Rais huyo amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza soka nchini.Nazir Khalfan hivi sasa anachezea timu ya Vancouver Whitecaps ya nchini Canada inayoshiriki katika ligi ya Major League Soccer(MLS) ya nchini Marekani na Canada.Mbali na kumshukuru Rais Kikwete,Nazir alimpa zawadi ya jezi yenye jina lake(Kikwete)

Baada ya kumwania mara mbili bila mafanikio, hatimaye Shirikisho la Soka nchini Marekani hapo jana limefanikiwa kumuajiri aliyewahi kuwa nyota wa soka wa Ujerumani na ulimwenguni, Juergen Klinsmann, kuwa kocha wa timu ya taifa ya kandanda ya taifa hilo ili kuisuka upya timu hiyo.

Klinsmann ndiye aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani iliyoishia katika nafasi ya tatu katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006. Tofauti na Steve Sampson, Bruce Arena na Bob Bradley, watangulizi wake wa karibu, alikuwa mchezaji wa kimataifa wa timu ya taifa ya Ujerumani.

Yeye aliajiriwa siku chache baada ya Bradley kutimuliwa.Mechi yake ya kwanza akiwa kocha wa Marekani dhidi ya Mexico katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa tarehe 10 August huko Philadelphia.

Katika taarifa aliyoitoa hapo jana, Klinsman amesema anayo furaha na heshima kubwa ya kukabidhiwa dhamana ya kuinoa timu hiyo hususani inapoanza mchakato wa kujiandaa kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 zitakazofanyikia nchini Brazil. Klinsmann, ambaye leo Jumamosi anatimiza miaka 47,anaishi na familia yake huko Kusini mwa California.

Timu ya soka ya Yanga(watoto wa Jangwani),jana wamechukua Ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara baada ya kuichapa timu ya Toto Africa ya Mwanza kwa jumla ya mabao 3-0 na hivyo kuwavua rasmi ubingwa watani wao,timu ya Simba Sports Club kwa tofauti ya magoli.

Tofauti na ligi zilizopita,ligi ya safari hii ilibidi kusubiri mpaka michezo ya mwisho ili kujua nani atatwaa ubingwa.Hongera Yanga!

Mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa ya Ulaya, timu ya Inter-Milan kutoka Italia wamejiweka katika mazingira magumu sana ya kutetea ubingwa wao baada ya kukubali kipigo ambacho hakikutarajiwa na wengi cha mabao 5-2 dhidi ya e timu ya Schalke kutoka nchini Ujerumani.

Wakicheza katika uwanja wao wa nyumbani wa San Siro, Inter walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Schalke kunako sekunde za mwanzo tu za mchezo kupitia bao lililofungwa na Dejan Stankovic.Dakika chache baadae,Schalke walisawazisha goli hilo kupitia goli lililofungwa na Joel Matip kunako dakika ya 17.

Kunako dakika ya 34,Diego Milito aliifungia Inter goli la pili na hivyo kuamsha hisia kwamba mabingwa hao watetezi huenda wangeibuka washindi katika mchezo huo wa robo fainali.

Hata hivyo dakika sita baadae kunako dakika ya 40 Mbrazil Edu alisawazisha na hivyo kufanya timu zote kuelekea kwenye mapumziko zikiwa zimefungana 2-2.

Kipindi cha pili ndicho kilichokuwa muhogo wenye sumu kwa Inter kwani kunako dakika ya 53,mshambuliaji mkongwe,raia wa Hispania,Raul aliandika bao la tatu kwa Schalke kitu ambacho kilionekana kuwachanganya kabisa Inter kwani dakika tatu baadae,kunako dakika ya 57 mchezaji wao Andrea Rannochia alijifunga mwenyewe na hivyo kuwaweka Schalke mbele kwa bao 4-2.

Kama hiyo haitoshi alikuwa ni Edu tena aliyefunga kitabu cha magoli cha siku kwa bao safi kunako dakika ya 75.

Katika mchezo huo Schalke ilicheza bila wachezaji wake muhimu kama vile Klaas Jan Huntelaar, Christoph Metzelder, Mario Gavranovic na Rika Kluge.

Mchezo wa marudiano utapigwa wiki ijayo huko Gelsenkirchen nchini Ujerumani. Kwa matokeo ya leo,Inter itawabidi kufanya kazi ya ziada na karibu na muujiza ili kuitoa Schalke ambayo inaonekana wazi kuwa imepania kuutwa Ubingwa wa Ulaya katika msimu huu

Magoli mawili yaliyowekwa kimiani na Emmanuel Adebayor katika kila kipindi na mengine mawili yaliyoweka kimiani na Di Maria pamoja na Christiano Ronaldo, yalitosha kupeleka kipigo cha mabao 4-0 kwa timu ya Tottenham Hotspurs katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Adebayor aliifungia timu yake bao la kwanza kunako dakika ya nne tu tangu kuanza kwa mchezo kwa goli la kichwa kilichokuwa kikali kiasi cha kumshinda nguvu mlinda mlango wa Tottenham, Heurelho Gomes na kumpita katikati ya miguu mlinzi wa Tottenham Luka Modric na kuingia kimiani.

Kunako dakika ya 15 mambo yalizidi kuonekana wazi kuwa magumu kwa Tottenham baada ya mshambuliaji wao tegemezi,Peter Crouch kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Lilikuwa ni kosa la pili la kadi ya manjano kwa Peter Crouch.

Kunako dakika ya 57 alikuwa ni Adebayor tena aliyezidi kupigilia msumari wa moto katika ngome ya Tottenham baada ya kuandika bao la pili kufuatia pasi safi kutoka kwa Marcelo kabla ya Angel Di Maria na Christiano Ronaldo kuyaweka wazi matumaini ya Real Madrid kuingia nusu fainali baada ya mchezo wa marudiano wiki ijayo pale White Hart Lane yalipo makazi ya Tottenham Hotspurs.

Read the Next Page →

↑ Go Back to Top of Page