Wakati suala zima la nani alileta mradi wa Zinduka nchini Tanzania,nani alianzisha idea hiyo na mchakato mzima wa mradi huo likiendelea,nadhani sio vibaya kama tukajionea kile ambacho wasanii waliweza kufanya.
Kimsingi,kampeni hii ina umuhimu wa aina yake.Malaria ni tishio la uhai wa mamilioni ya watu ulimwenguni.Inaua kuliko ugonjwa mwingine wowote.Inaua zaidi ya Ukimwi!Kuna haja ya kuendelea kusambaza ujumbe.Kuna haja ya kuendelea kupeana maarifa kuhusu jinsi ya kupambana na ugonjwa wa malaria.Mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ni zaidi ya chandarua.Ni suala la mazingira.Vidimbwi vya maji yaliyotuama.Misitu ya majani inayoachwa bila matunzo.Ni pamoja na kutumia kila aina ya kinga zilizopo.Hongera kwa wasanii waliotengeneza na kushiriki katika video hii;Zinduka. Kwa msaada zaidi wa jinsi ya kupambana na malaria,bonyeza hapa.

Rais wa Zanzibar Dr Karume ametangaza kutogombea tena uraisi katika uchaguzi ujao mwakani kwa kuwa katiba ya Zanzibar haimruhusu yeye kufanya hivyo.
Raisi ameyasema hayo hapo jana kwenye hotuba yake Kwenye sherehe za Miaka 46 ya Mapinduzi Zanzibar zilizofanyika kwenye viwanja vya Gombani Pemba ambazo zilihudhuriwa na na viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwemo Rais Jakaya Mrisho Kikwete,Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa,Rais Mstaafu Mzee Alhaj Hassan Mwinyi,Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda,Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa,Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi Cuf Sheif Sharrif Hamad pamoja na Lipumba,Waziri Kiongozi wa serikali ya mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Nahodha na Wakuu wa Majeshi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
Je unadhani nini itakuwa ni hatma ya Chama Cha Mapinduzi huko Zanzibar? Wakati wa CUF umewadia?Nani atamrithi Karume?
Source: Charaz

Msomaji na mtembeleaji wetu mmoja,ameomba tumwekee hapa picha ya karibu(close-up) ya First Lady wetu,Mama Salma Kikwete.Msomaji huyo anasema tangu picha za Marais na viongozi wa nchi mbalimbali wakiwa na Rais wa Marekani Obama na mkewe Michelle Obama zitokee katika vyombo mbalimbali vya habari amekuwa akipata tabu na marafiki zake ambao wamekuwa wakimhangaisha kutaka kumuona First Lady wa Tanzania.Mama Salma Kikwete hakuwepo katika picha zile za viongozi mbalimbali na kina Obama.Msomaji/mtembeleaji wa BC,hiyo hapo juu ni picha ya karibu ya Our First Lady,Mama Salma Kikwete.
Kituo maarufu cha ABC cha nchini Marekani jana,kupitia kipindi chake cha 20/20, kiliionyesha dunia kuhusu tatizo sugu la mauaji ya Albino nchini Tanzania na pia jinsi watu waliozaliwa albino wanavyopambana na masuala mbalimbali yakiwemo ya kubaguliwa na kiafya.
Pamoja na juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali,mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi,tatizo la mauaji ya albino yanayotokana na imani za kishirikina bado lipo. Bado ni jambo ambalo linaitia doa nchi yetu,kutupaka sote matope na muhimu zaidi kupoteza wadogo zetu,kaka zetu,dada zetu,ndugu,jamaa na marafiki. Raia wenzetu wanaishi kwenye hofu.Hawalali kwa amani na hawatembei kwa amani katika nchi yao wenyewe.Wanawindwa kama wanyama.Hali hii ni lazima ikomeshwe.
Bonyeza katika links hizo hapo chini ili kutizama video hizo.Kwa kusaidia albinos nchini Tanzania,bonyeza hapa.
Picha kwa niaba ya ABC News.
Kama umewahi kusoma kitabu maarufu cha mwandishi Shafi Adam Shafi kinachoitwa Kuli, bila shaka utakuwa unakumbuka sentensi iliyofunga kitabu kile. Alisema; Yana mwisho haya.Kuli ni mojawapo ya vitabu ambavyo mpaka hivi leo namshauri mtu yeyote ambaye hajawahi kukisoma kufanya hivyo.
Kumbukumbu ya kitabu hicho ilinijia wiki hii nilipokuwa namsikiliza Katibu Mkuu wa CUF,Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari pale Buguruni ambapo aliweka wazi kwamba endapo viongozi wa chama tawala wanataka na kweli wana nia ya kuona amani inaendelea kuwepo visiwani Zanzibar,basi hawana budi kubadili mienendo yao na hususani sera na utaratibu mzima wa wananchi kujiandikisha tayari kwa kuwa wapiga kura katika uchaguzi mkuu hapo mwakani.Maalim anasema CCM inafanya njama ovu za kuwazuia wananchi kujiandikisha.
Katika kupambana na njama hizo za kiovu,Maalim anawaasa wananchi wa visiwani kusimama imara ili kutetea haki zao za msingi. Kwa msemo huu Maalim ananikumbusha yule mwanaharakati wa nchini Marekani, Malcolm X, aliyewahi kuwaasa watu weusi kwa msemo wake maarufu wa :By any means necessary”.Tayari kumeripotiwa mapambano ya silaha za moto baina ya wananchi na vyombo vya dola.
Nakiri kwamba historia ya ndani ya visiwa hivyo imenipiga chenga.Bado naisoma. Lakini kwa juu juu inaelekea kwamba lipo kundi la watu fulani ambalo linaamini kwamba ni lazima libakie madarakani milele.Kundi hilo linaamini kwamba bila wao,hakuna uongozi.Bila wao, mambo mengi yatakwenda mrama. Hilo tumeshalishuhudia tangu mfumo wa vyama vingi ulipotinga.Kwanini kundi hilo linaamini linavyoamini? Jibu kwa sasa sina.Naendelea kufanya utafiti.Anayejua tafadhali anisaidie. Kama una pendekezo la kitabu cha kusoma, usisite.
Pamoja na hayo, kama Maalim Seif anaongelea suala la kuchukua silaha,kuweka begani na kuingia msituni na kisha kurejea juu ya vifaru,sikubaliani naye. Sijashuhudia bado mahali ambapo amani ya kweli ilipatikana kwa ubabe uliokithiri. Nafasi ya kuambiana ukweli,kuketi mezani bado ipo.Demokrasia ni suala linalochukua miaka mingi sana.Sisi bado ni wachanga sana.Tusitegemee miujiza au majibu ya siku moja au mbili.Tupande na kisha tuhakikishe mizizi imeota.Tusichoke kusema,kukosoa na kuambiana ukweli bila uoga.Kama anavyofanya Maalim Seif.Yana mwisho.

Hivi karibuni,tajiri bilionea mmiliki wa timu maarufu ya soka ya Chelsea FC ya nchini Uingereza, Roman Abramovich, alitinga nchini Tanzania na akiwa na nia ya kutalii na kuupanda mlima mrefu kupita yote barani Afrika yaani Mlima Kilimanjaro.
Safari ya Bilionea Abramovich kuja kupanda Mlima Kilimanjaro ilikuwa ni habari kubwa iliyoripotiwa na vyombo lukuki vya habari hususani nchini Tanzania na Uingereza.Kilichoifanya habari hiyo kuwa kubwa hakutokani tu na ukweli kwamba Abramovich ni miongoni mwa watu matajiri sana ulimwenguni bali pia ni ule uhusiano uliopo miongoni mwa mchezo wa soka ulimwenguni huku mashabiki wa timu ya Chelsea anayoimiliki Abramovich ya Chelsea ikiwa na mashabiki kibao ulimwenguni wakiwemo pia wale wanaoishi na kuitazama timu hiyo kutokea Tanzania.
Ingawa Roman Abramovich hakufika kileleni, ni wazi kwamba,kwa namna moja au nyingine,amesaidia kuinua soko la utalii la Tanzania na hususani upandaji wa Mlima Kilimanjaro.
Lakini ni nani aliyemuongoza njia Roman Abramovich? Kuna wadadisi wameuliza swali hili na tuna furahi kwamba jibu lake tumelipata. Aliyekuwa guide wa Roman na rafiki zake anaitwa Isaac Kitindi(pichani juu ndiye anayeonekana kushoto akiwa na Roman.
Isaac ni Mhitimu wa Advanced Diploma katika masuala ya Wildlife Management kutoka Chuo cha Elimu na Utawala wa Wanyamapori cha Mweka kilichopo Moshi,Kilimanjaro. Isaac alikuja Tanzania maalumu kwa shughuli ya kumsindikiza Roman Abramovich mlimani kwani hivi sasa anasomea masuala ya Huduma ya Kwanza (First Aid Training) katika chuo kikuu maarufu cha Havard nchini Marekani.
Isaac Kitindi ambaye wenzake hupenda kumuita Mountain Madness kutokana na umahiri wake wa kuupanda Mlima Kilimanjaro hivi sasa yupo njiani kurejea Havard huku kukiwa na habari kwamba atapitia nchini Uingereza ambapo ataonana tena na Roman Abramovich kwa mazungumzo ya kuileta Tanzania timu ya Chelsea FC hapo mwakani.
Ukitaka kujua ilikuwaje mpaka Roman Abramovich akashindwa kufika kileleni,bonyeza hapa.
Wiki hii mwanasiasa aliyevuma zaidi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete.Kama umefuatilia vizuri kwenye vyombo mbalimbali vya habari,habari kubwa ilikuwa kuhusu utaratibu mpya aliouanzisha Rais Kikwete wa kuongea na wananchi na pia kuwapa nafasi ya kuuliza maswali ya papo kwa hapo.
Ingawa wananchi wengi wakiwemo pia viongozi wa vyama vya upinzani kama vile Mhe.Dr.Slaa,wanasema Rais Kikwete alipinga chenga au kujibu juu juu sana maswali ya wananchi,mimi nampongeza kwa kuanzisha utaratibu huu. Kama utadumu na kama utakuwa huru(kunawezwa wekwa mamluki wa kuuliza maswali;hakuna linaloshindikana karne hii),naamini ni njia nzuri ya Rais kuwasiliana na wananchi na japo kujua kwa mbali,yanayowakera.Hongera JK! Bado tu kufungua blog na account za twitter,facebook na myspace.Watanzania wengi sana siku hizi wanatumia zana hizo za mawasiliano.Obama yeye anazo zote tayari.
Pamoja na sifa hizo,kuna kitu ambacho kinanifanya nigune kidogo.Kwanini Mheshimiwa Rais amesubiri mpaka umebakia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi ndio aanzishe utaratibu huu?Nia ni kusikia kweli hoja na maswali ya wananchi au ndio “kujiweka sawa” kabla ya uchaguzi?
Nini maoni yako kuhusiana na utaratibu huu mpya wa Rais Kikwete?Na je kama uliangalia zoezi zima la hotuba,maswali na majibu,unasemaje?Unampa alama gani Mheshimiwa Rais?A,B,C,D au…?

Kila kukicha,watanzania mbalimbali waliotapakaa ulimwenguni kote wanazidi kuwa wabunifu na watu wanaothubutu kufanya mambo fulani fulani ambayo sio tu yanazidi kuiweka Tanzania mahali inapostahili katika ramani ya dunia ,bali pia kuongeza ujuzi,kuingiza vipato halali na zaidi to make us proud!
Hayo yanatokea katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya filamu!Bila shaka ulifuatilia filamu za Kibira za Bongoland.Ukipenda unaweza kusema ule ulikuwa ni mwanzo tu.Wengine wamefuata nyayo hizo na wanakuja na filamu inayokwenda kwa jina la BABY POWDER. Ni watanzania wanaoishi jijini Atlanta,GA.
Filamu hii inatarajiwa kuonekana kwa mara ya kwanza kabisa ndani ya jiji la Atlanta lililopo jimboni Georgia nchini Marekani tarehe 14 November,2009.Baada ya hapo itaonyeshwa jijini Houston huko Texas tarehe 26 November,2009 na kisha jijini Washington,DC tarehe 5 December 2009. Baada ya hapo itakuwa zamu ya watu wa Minnesota kuiona tarehe 19 December 2009 kabla ya tour ya Europe na Africa haijaanza tarehe 25 December 2009. Tarehe na miji itakapoonyeshwa filamu hiyo zitatangazwa baadaye.
BABY POWDER ni filamu inayogusa maisha ya kweli . PHILIP NKASA (Lambert “LBT” Tibaigana) ni kijana wa kitanzania ambaye anakwenda Marekani kwa matumaini ya kupata elimu ili kuweza kuboresha maisha yake na ya familia yake nyumbani. Philip ananzaa maisha yake ndani ya Marekani katika mji mdogo wa Wichita,KS na baada ya kumaliza shule na kushindwa kupata kazi ,Philip anakata shauri kwenda kujaribu bahati yake katika jiji la Atlanta, GA.
Mambo hayawi kama Philip alivyotegemea.Upatikanaji wa kazi jijini Atlanta unakua wa shida.Ili kuendesha maisha Philip anachukua kazi ya malipo kidogo pamoja na kuwa tayari ni msomi mwenye shahada ya kwanza(degree)Hali ya maisha ya wazee wake inaendela kuwa mbaya kutokana na mapato yake kuwa kidogo na hivyo kushindwa kuwasaidia.
Tizama Trailer hapa;
Baada ya kugundua mfanyakazi mwenzake Mamdo (Albert Levasseur) anafanya biashara haramu, Philip anaona hiyo ndio nafasi ya kutatua matatizo yake.Baada ya kuonja asali anachonga mzinga. Anaingia katika biashara haramu kwa nguvu zote. (more…)

Mwanasiasa wetu wa wiki hii ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.Kama ambavyo pengine umeshasikia,kwa mara nyingine wanachama wa CHADEMA,wameonyesha imani waliyonayo na Nd.Freeman Mbowe kwa kumchagua tena kukiongoza chama hicho katika miaka minne ijayo akiwa kama Mwenyekiti.
BC inaungana na wapenzi wote wa demokrasia ulimwenguni katika kumpongeza Freeman Mbowe kwa kuchaguliwa kwake na pia kuwapongeza wote wa CHADEMA (hususani wajumbe wa mkutano mkuu) kwa kutekeleza zoezi hilo muhimu kwa demokrasia na uhai wa chama.
Mtakumbuka kwamba hapo mwanzo mwanachama mwingine wa CHADEMA,Mbunge/Mheshimiwa Zitto Kabwe, alikuwa ameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo kabla hajajitoa dakika za mwisho jambo ambalo limeacha minong’ono kwamba aliamriwa kujitoa na hivyo kuzusha maswali kedekede kuhusu ‘demokrasia” iliyopo ndani ya chama hicho na pia msimamo wa Zitto Kabwe katika maamuzi mbalimbali kisiasa na kibinafsi.
Kama Zitto alijitoa kwa shinikizo basi hilo ni kosa.Ni sumu katika demokrasia. Lakini kama alijitoa kwa uamuzi wake mwenyewe,basi nadhani ni haki yake,ni uamuzi wake na kama ataujutia katika siku za mbeleni,hilo ni suala la kusubiri na kuona.Bado namtafuta ili atupe ufafanuzi kuhusu uamuzi wake wa kujitoa katika kugombea nafasi ya mwenyekiti na pia hali yake ya kisiasa katika siku zijazo.
Kwa upande wa Freeman Mbowe;kuchaguliwa kwake kulikwenda sambamba na kutangaza baadhi ya sera za chama hicho ukiwemo mfumo mpya unaotumia tekinolojia zaidi katika kuongeza idadi ya wanachama “hai” na pia kuinua kipato cha chama hicho.
Kichwa kimoja cha habari kilichosindikiza kutangazwa kwa sera hiyo kilinivutia zaidi. Kiliandika “CHADEMA yafuata nyayo za Obama“. Hivi ni kweli kwamba hivi sasa ukitaka mambo yako yaende sawa katika anga za kisiasa basi jina la Obama ni sharti liwemo kwenye vocabulary yako?Bila shaka katika mwaka ujao(mwaka wa uchaguzi) tutasikia sana maneno kama “mabadiliko,change” nk.Tusubiri tutaona.
Hata hivyo nawapongeza CHADEMA kwa maendeleo hayo na pia uamuzi huo wa kwenda sambamba na tekinolojia.Wasiwasi wangu ni mmoja tu;tupo tayari?CHADEMA wapo tayari au ni mbwembwe tu za kisiasa?
Nasema hivyo kwa sababu ninaamini kwamba maendeleo kama hayo ya kitekinolojia ni lazima yaende sambamba na uwezo wa kimiundo mbinu ya tekinolojia na wataalamu wa kuendesha vitu hivyo.
Mpaka ninapoandika habari hii,tovuti ya CHADEMA bado haina habari za uchaguzi wa Mwenyekiti Freeman Mbowe kitu ambacho, kwa maoni yangu,kinaashiria kutokuwepo tayari kwa sera za matumizi ya tekinolojia alizozitangaza mwenyekiti.Ushabiki wa siasa lazima uwekwe kando hapa.Maandalizi ya kweli yapewe kipaumbele. Nasikia jamaa wa chama tawala tayari wameanza kukuna vichwa ni jinsi gani watakabiliana na mfumo huu mpya wa CHADEMA.
Je unasemaje kuhusu kuchaguliwa tena kwa Freeman Mbowe kukiongoza Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)? Is it a right move or another wrong move?Nini maoni yako kuhusu mfumo wa kuandikisha wanachama na kukusanya fedha uliotangazwa na Freeman Mbowe?
Kama lipo jambo ambalo liliamsha hisia tofauti kwenye ulingo wa siasa,basi ni tamko au kitendo cha mwanasiasa kijana,Zitto Kabwe,kutangaza nia ya kugombea uenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)
Zitto Kabwe ambaye hivi sasa anashikilia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu katika chama hicho,anasema pamoja na kwamba anaamini na kuafiki kwamba Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho,Freeman Mbowe,ni kiongozi mzuri na kwamba amekitoa mbali chama hicho,wakati umefika wa kuwa na mabadiliko.Zitto anasema chama kimetawaliwa na “kufukuzana” uanachama. Jambo hilo lazima lifikie kikomo,anasema Zitto.
Kisha anasema lazima CHADEMA kijiandae kuchukua dola. Kwa maana hiyo labda tunaweza kusema Zitto anamaanisha kwamba CHADEMA ilivyo hivi sasa,hakiwezi au hakistahili kushika dola.Kinahitaji maandalizi!Hapa ni muhimu kukumbuka kwamba uchaguzi mkuu ni 2010 na sio 2011 au 2012.
Kama utakumbuka,miezi kadhaa iliyopita Zitto Kabwe alitangaza nia yake ya kutogombea tena nafasi ya Ubunge wa Kigoma Kaskazini anayoishikilia.Alisema anataka kujikita zaidi kwenye taaluma yake na hivyo kuachana kidogo na mambo ya siasa.Sasa tunajua kwamba hakuwa akimaanisha alichokuwa anakisema.Alijivika uhalisi wa siasa.
Je unasemaje kuhusiana na uamuzi wa Zitto Kabwe kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA?Unadhani atakuwa ni nahodha bora wa chama hicho cha upinzani zaidi ya Mwenyekiti aliyepo madarakani hivi sasa?
***Niliwahi kufanya mahojiano na Zitto Kabwe takribani miaka miwili iliyopita.Bonyeza hapa usome mahojiano yale ili pengine upate picha zaidi juu ya Zitto Kabwe.

