Waswahili tunao msemo usemao, Siku njema huonekana asubuhi. Ni msemo wa kale ambao tafsiri yake halisi inaweza kutofautiana baina ya mtumiaji mmoja kwenda mwingine. Huo ndio utamu wa lugha na misemo ya kwetu. Tunaweza kutofautiana lakini wote tukawa sahihi, angalau kwa mapana yake.
Pamoja na tofauti kadhaa zinazoweza kujitokeza katika tafsiri, nina uhakika kwamba wengi tutaelemea katika tafsiri rahisi ambayo ni kwamba unavyoianza siku ndivyo utakavyoimaliza. Hisia na vitendo vyako unapoianza siku yako vina mengi ya kusema kuhusu itakavyokwenda na itavyofikia ukingoni.
Ukiamka na kujihisi mchovu,ukaichukia siku hata kabla haijaanza,ni wazi kwamba utakuwa umejiweka mwenyewe kwenye mtego wa kuwa na siku mbaya! Hutofanikisha malengo yako.Kazini unapokwenda mambo yanaweza kwenda mrama.Kwanini? Umeiandaa vibaya siku yako.Ikitokea mwenzako fulani iwe kazini au shuleni akakuambia mbona leo unaonekana kama unaumwa au umechoka(hata kama anakutania tu) ndio kabisaaa anakuwa amekumaliza.
Kwa upande mwingine, siku njema huonekana asubuhi unaweza kuwa msemo unaoonyesha nguvu ya utabiri tuliyonayo sisi kama wanadamu.Tunazo hisia.Unaweza kuhisi kwamba kitu fulani unachokifanya au unachoacha kukifanya kinaweza kuwa na matokeo yasiyopendeza. Kila mmoja wetu anazo nguvu za utabiri.Tofauti ni jinsi tunavyozitumia,kuziamini au kuzifanyia kazi.
Bahati nzuri ni kwamba binadamu tumepewa uwezo mkubwa wa kunyumbulisha dunia na mambo mbalimbali.Sasa ufanyeje ili uianze siku vizuri? Wataalamu mbalimbali wa mambo ya saikolojia na utabibu wanakubaliana kwamba ukiianza siku yako mapema, itakuwa nzuri! Kuanza siku mapema, kwa mapana na marefu kunajumuisha kuamka mapema na kuwaza vyema.
Leo nimeamua kuongelea umuhimu wa kuamka mapema kwani kama nilivyotangulia kusema hapo juu,wataalamu wengi wanakubaliana kwamba kuamka mapema ni msingi wa kuwa na siku nzuri,maisha mazuri na kubwa zaidi,afya nzuri.Watu wengi ambao tunawaita “waliofanikiwa maishani” na hata matajiri wakubwa hapa duniani,wanalo jambo moja linalofanana. Katika kuwafuatilia(kupitia makala za magazetini,vitabuni na hata mahojiano yao katika televisheni) wote wanakiri jambo moja.Wote ni wa kwanza kudamka(early birds). Kwanini?Bila shaka kuna sababu.
Pengine baada ya kusoma kichwa cha habari umeshajiuliza; kwanini niamke mapema? Sababu ya Kwanza ni kwamba unapoamka mapema, unapata muda mzuri wa kujiweka sawa,kuipanga siku yako vyema. Imeshawahi kukutokea ukakurupuka usingizini na kukuta muda umeshakwenda na umechelewa kwenda unapotakiwa kwenda iwe ni kazini,shuleni au kwingineko? Umeshaona jinsi mpangilio wako wa mambo unavyokwenda kombo? Unapofika ofisini kwa mfano, unakuwa hata kuamka vizuri hujaamka bado na kila mtu anakutolea macho kwa sababu hata nywele hukukumbuka kuchana? Ungeamka mapema,ukaipanga siku yako vyema yote hayo yasingekukuta.
Faida ya pili ni kuweza kutumia ukimya wa asubuhi. Umeshawahi kudamka asubuhi ukaona jinsi palivyo na utulivu wa aina yake? Amini usiamini,ukiutumia ukimya huo wa asubuhi kuwaza na kupanga mambo yako,ni wazi kwamba utafanikiwa zaidi. Akili ya binadamu imetengenezwa ifanye vizuri zaidi panapokuwa na utulivu. Wenzetu wa magharibi ndio maana wakaja na msemo wa Silence is Golden.
Tatu,wataalamu wa afya wanasisitiza sana kuhusu kifungua kinywa(breakfast). Huo ndio mlo muhimu zaidi katika siku. Ni wazi kwamba ukiamka mapema, utapata muda mzuri wa kuandaa na kisha kupata kifungua kinywa kwa utaratibu unaofaa bila papara kitu ambacho ni muhimu kwa afya yako. (more…)
Bila shaka umeshawahi kusikia msemo wa wenzetu wa magharibi usemao “Time is Money”. Yawezekana kwamba msemo huo,kwa tafsiri ya moja kwa moja, unamaanisha kwamba muda ni pesa. Lakini ninavyoelewa mimi msemo huo unaongelea au unajaribu tu kuonyesha jinsi gani muda ni kitu cha thamani! Jinsi unavyoutumia muda wako hivi leo ni ishara tosha ya jinsi kesho yako itakavyokuwa.
Kwa upande mwingine umeshawahi kusikia mtu au watu fulani fulani wakilalamika kwamba “hawana muda” wa kufanya kitu fulani. Sababu itolewayo mara nyingi ni kwamba wapo “bize”. Wapo ‘bize” na ndio maana hawana muda wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za kijamii.Ndio maana hawana muda wa kikao cha harusi cha rafiki,ndugu au jamaa.Hawana muda wa kuhudhuria msiba wa mtu. Wapo “bize” na ndio maana hawakuweza kukupigia simu nk.
Sasa inakuwaje mtu mmoja awe na muda na wakati huo huo mtu mwingine asiwe kabisa na muda wakati sote tunaishi kwenye dunia moja na siku ina masaa yale yale 24? Sababu zinaweza kuwa nyingi. Zingine zinaweza kuwa ni za visingizio tu.Zingine zinaweza kuwa za kweli na za uhakika.
Pamoja na hayo, jinsi unavyotumia muda wako, jinsi unavyopangilia mambo yako, ratiba zako nk, ni sababu ya kutosha kama una muda wa ziada wa kufanya mambo mengine mengi uyapendayo ikiwemo mapumziko, muda wa kukaa na wanafamilia yako, kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni na lolote lile ambalo unapenda kulifanya lakini umekuwa hulifanyi kwa sababu au kisingizio cha ukosefu wa muda.
Leo tutaangalia baadhi ya mambo ambayo unaweza kuyafanya ili kuokoa muda ili kujipatia muda unaohitaji kwa sababu ambazo nimezitaja hapo juu;
- Anza siku yako mapema: Hili ni la msingi sana.Amka mapema. Ukiianza siku yako mapema, sio tu kwamba kuna faida za kiafya kama ambavyo tutakuja kuziongelea katika siku za mbeleni, bali unakuwa na muda wa ziada wa kuiandaa ratiba kamili ya siku yako. Kwa ujumla binadamu anatakiwa kulala kwa muda wa masaa nane. Siri ya kuamka mapema inaanza na kwenda kulala katika muda unaofaa ili upate hayo masaa manane. Kumbuka siku njema huonekana asubuhi.Ipe siku yako mwanzo mzuri.
-
Orodhesha mambo unayotaka kufanya: Ushasikia msemo usemao; Mali bila daftari hupotea bila kujua. Hali ni hiyo hiyo hata katika suala zima la muda. Unapoianza siku hakikisha umeorodhesha mahali kwenye kikaratasi au kidaftari chako cha kumbukumbu mambo yote ambayo umedhamiria kuyafanya katika siku inayokukabili.Katika zama hizi za sayansi na tekinolojia,simu nyingi za viganjani zina huduma ya kalenda ambayo unaweza kuitumia kuorodhesha mambo unayotaka kufanya kesho,mwezi ujao au hata mwakani.Zitumie.Andika pia na muda ambao ni lazima utimize mambo hayo.
Faida za kuorodhesha mambo unayotaka kufanya ni kwamba kwanza orodha hiyo itakuwa inakusuta. Itakuwa inakuuliza,ulisema leo utafanya hivi imekuwaje? Pili orodha hiyo hiyo itakupa pia nguvu au ari ya kutimiza malengo yako. Tatu na muhimu zaidi kama mada yetu ya leo inavyodai, utaokoa muda. Utafanya kila jambo kutokana na muda uliojipangia kwani orodha itakuwa inakuonyesha kwamba siku bado haijaisha na mengine yanakungoja.
Pia wakati unaandika orodha yako, kumbuka kuweka pamoja mambo ambayo yanaweza kufanyika kwa pamoja au katika muda huo huo.Kwa mfano, leo umepanga kwenda katika benki fulani kuomba mkopo wa biashara.Wakati huo huo umepanga kwenda kwa chakula cha mchana na rafiki yako anayefanya kazi katika benki hiyo hiyo. Hayo unaweza kuyatimiza kwa pamoja. Unaweza kumuona meneja wa mikopo wa benki na kisha baada ya kumaliza ukaenda na rafiki yako kupata chakula. Hakikisha tu kwamba rafiki yako sio huyo huyo tena ndio meneja wa mikopo.Hapo kutakuwa na harufu ya ufisadi.Unajua tena jinsi mambo yalivyo nchini mwetu hivi sasa.Kuwa makini. (more…)
Ujasiriamali ndio neno jipya. Kila mtu anaongelea habari za ujasiriamali. Pengine hii inatokana na wengi wetu kutambua kwamba nyakati zimebadilika na ujasiriamali ndio njia iliyo sahihi zaidi kama mtu anatamani mafanikio ya kweli maishani.Vijana ndio chachu zaidi ya ujasiriamali au naweza kusema ndio wanategemewa zaidi kuendeleza ujasiriamali hususani katika ulimwengu wa leo wa sayansi na tekinolojia.
Pamoja na nia nzuri walizonazo vijana, pengine ukiwemo wewe unayesoma makala hii, kipo kizingiti ambacho ni lazima watu wajifunze mbinu mpya za kukivuka. Kizingiti hicho ni aina ya elimu itolewayo mashuleni. Kwa bahati mbaya elimu zitolewazo mashuleni bado hazijawekwa katika msingi unaomuwezesha kijana kujiajiri au kwa maneno mengine kuwa mjasiriamali pindi amalizapo masomo yake.
Bado tupo katika ule mfumo wa kikoloni. Ukimaliza shule unachotakiwa ni kuanza kutafuta kazi. Zunguka jijini Dar-es-salaam kwa mfano, utakutana na vijana wengi wasomi waliohitimu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini wakiwa wamebeba vyeti vyao kwenye vijifuko vya plastiki wakizurura kusaka ajira. Hakuna anayefiria kujiajiri kwa kutumia elimu aliyoipata chuoni. Kwanini? Ndivyo ilivyo. Elimu aliyopewa haikumuandaa.Utakutana na engineer wa umeme ambaye hajawahi kubadilisha hata balbu!(nimeongeza chumvi kidogo hapa lakini kuna ukweli ndani yake!) Amesomea nadharia zaidi ya vitendo. Utakutana na mwanafunzi mhitimu wa masomo ya kilimo na mazingira ambaye hajui shamba ni nini.Hilo ni kosa katika mfumo wetu wa elimu. Ni lazima serikali ichukue jukumu la makusudi kubadili mfumo huo.
Lakini wapo wengine wengi ambao wana nia ya kweli ya kuwa wajasiriamali. Wana nia ya kujiajiri. Leo tutaangalia jinsi gani mjasiriamali chipukizi aanzishe kampeni yake. Si ushasikia kwamba biashara siku hizi ni kujuana? Ujasiriamali pia. Ni muhimu sana kujua ni nani au ni wapi uende endapo mambo yatakwama. Siongelei wapi uende kutoa au kupokea rushwa.La. Nataka kuongelea kitu kinachoitwa na wenzetu wa magharibi “networking”.Kwetu sisi hiki ndicho tunachoita “mtandao”.Mitandao ya kijamii kama vile facebook,twitter,myspace nk ni sehemu nzuri ya kutengeneza network.Itumie vizuri.
Ni muhimu kutengeneza mtandao mzuri kama unataka kuwa mjasiriamali makini na hususani kama unataka kufanikiwa. Kumbuka kwamba hapa hatuongelei kubadilishana business cards peke yake bali kumjua mtu kwa nia njema ya kusaidiana.Kumbuka neno ni “kusaidiana” na sio wewe pekee kupokea msaada.Lazima pawe na nia njema ya kusaidiana.
Kabla sijaanza kuorodhesha mbinu mbalimbali za kutengeneza ‘mtandao’ wako, naomba nikwambie kwamba siri ya kwanza ya kuanza kuwa mjasiriamali ni maandalizi.Jiandae kwa mtaji,elimu(ya darasani na mtaani),mbinu za kibiashara nk. Pili hakikisha kwamba una mapenzi ya dhati na hicho unachotaka kufanya.Usiingie kwenye biashara au ujasiriamali kwa sababu tu umemuona fulani amefanya hivyo.Kuna umuhimu mkubwa wa kujitambua katika suala zima la ujasiriamali. Baada ya kusema hivyo,sasa tuingie kwenye maeneo ya kutengeneza mtandao wako kama mjasiriamali;
- Washindani wako: Biashara ni ushindani lakini sio uadui.Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio ni vizuri sana ukawajua washindani wako wa kibiashara.Pata vipeperushi vyao,tembelea tovuti zao,wajue wateja wao na kwanini hao watu ni wateja wao.Kisha jitambulishe kwao.Najua hapa unasema;nijitambulishe?!! Ndio,jitambulishe.Kama nilivyosema ni washindani lakini sio maadui zako. Mshindani wako anaweza kukufaa pia.Anaweza kuzidiwa na kazi akakusukumia zingine.Jitambulishe,jenga uhusiano mzuri wa kibiashara.Isitoshe nyote mpo kwenye biashara moja,sekta moja.Ya kesho hamyajui.Kama kuna chama au ushirika wa watu waliomo kwenye eneo lako la ujasiriamali,jiunge. (more…)
Kuanzia wiki hii BC inaanzisha kitu kitakachokuwa chini ya kipengele cha BC MAARIFA.Kila mwisho wa wiki(jumamosi au jumapili)kutakuwa na makala kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo ya kimaisha na kibinadamu katika nyanja mbalimbali kama vile mahusiano,kazi,pesa,afya,familia nk.Kutakuwa kunatolewa dondoo mbalimbali zinazohusiana na maendeleo binafsi ya mtu(Personal Development.
Nia ni kupeana maarifa au ujuzi fulani fulani ambao unaweza kutusaidia sote kama watu binafsi au jamii.
Naomba tu niweke wazi kwamba hii ni Pilot Project kwa maana ya kwamba ni kitu ambacho tunakifanyia majaribio.Kama unapenda kipengele cha namna hii,tungefurahi kama utatuambia aidha kwa kupitia kwenye sehemu ya maoni au kwa kutuandikia e-mail.Kuendelea kwake kutategemea sana mchango wako.
Pia kama wewe ni mwandishi na ungependa kuandika katika mtindo huu huu wa Tips for Personal Development,usisite kutuandikia.Leo tunaanza na mada iliyopo hapo chini.Asante kwa ushirikiano.
KWANINI SIFANIKIWI VYA KUTOSHA?
Tamaa ya mafanikio katika maisha ni safari ndefu. Kwa wengi wetu ni safari ya kudumu. Kila mara tunataka zaidi. Tunataka kuwa kama fulani au fulani.Tunatamani kuwa na kiasi cha fedha kama au kuliko fulani.Kuwa na mke au mume mzuri na mwenye heshima kama fulani. Na kwa wale ambao maisha yao huendeshwa na tamaa za kuwa maarufu basi kila leo huwa wanataka kuwa kama mwanamuziki,muigizaji filamu,mwanasiasa fulani na vitu kama hivyo.
Ingawa ni vigumu sana kwa binadamu kufikia mahali ambapo anaweza kusema kwamba amesharidhika vya kutosha na alichonacho na hataki nyongeza yeyote zaidi,yawezekana kabisa mtu akafikia mahali pa kuridhisha ingawa hiyo haimaanishi kwamba akipata nafasi ya kupata zaidi hatoitumia. Hapa tunaweza kusema mtu anakuwa ameridhika kwa kiasi cha hali ya juu.
Lakini kwanini basi baadhi yetu tunashindwa kufikia japo robo tu ya mafanikio tunayoyatamani? Ni mambo gani yanatukwamisha? Leo nimeona tuongelee kidogo sababu kadhaa ambazo zinatufanywa wengi wetu tukwame na hata kuishia kulaumu watu wengine bila kutambua kwamba yawezekana sababu sio ukosefu wa elimu ya kutosha,mtaji wala chochote kile bali sisi wenyewe;
-
Hujiamini vya kutosha: Ukijaribu kuangalia au kufuatilia maisha ya watu ambao sote tunaamini kwamba wana mafanikio zaidi yetu utagundua jambo moja muhimu;Wanajiamini.
Wanaamini kwamba wanalo jambo au mambo ya msingi wanayoweza kuchangia katika jamii. Wanajiamini na wana madhumuni ya makusudi kuhakikisha kwamba jamii itawakumbuka.
Watu hao pia huwa ni wajuzi wa kuketi chini wakajikosoa wenyewe na kisha kusonga mbele zaidi na zaidi.
Je wewe hapo ulipo una kitu gani cha kipekee? Unayo maarifa au ujuzi (skill or talent) gani maalumu ambao hujaufanyia kazi kwa sababu ya kutojiamini tu? Kwanini usiamke leo ukaanza kujiamini zaidi kisha uone jinsi utakavyobadilisha muelekeo? (more…)

