
Ingawa kila siku idadi ya bloggers wa kitanzania inazidi kuongezeka,idadi ya wanawake wanaoblog bado ni ndogo ikilinganishwa na wale wa kiume.Yawezekana ni kwa sababu wanawake bado hawajapata mwamko wa kutosha au pengine ni kitu ambacho bado wanakipa kisogo.
Lakini pamoja na idadi ya wanawake kuwa ndogo,wanaofanya hivyo wanafanya kazi nzuri sana ya kuwawakilisha wanawake wenzao.Miongoni mwa wanawake hao ni pamoja na Shamim Mwasha au Zeze kama anavyojulikana kwa watu wake wa karibu.
Iwe ni shughuli yenye mvuto wa kitaifa au wa mtu binafsi(hususani zile zenye kuwagusa wanawake zaidi),ukihudhuria na kutizamatizama katika watu waliopo mstari wa mbele katika kuchukua kumbukumbu iwe ni kwa kutumia picha za mgando(still photos) au videos,bila shaka waweza kumuona Zeze.Ukimsalimia atakujibu na kukurushia tabasamu ambalo naweza kusema ni “signature” yake.
Hivi karibuni nilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ambayo utayasoma hivi punde.Zeze ambaye blog yake inakwenda kwa jina www.8020fashions.blogspot.com, anaweka bayana mambo kadhaa kuhusu harakati zake kama mwandishi wa habari(taaluma yake) na pia blogger pamoja na ujasiriamali.
Yote tisa,kumi ni kwamba siku chache zijazo,Shamim kupitia blog yake ya 8020fashions,anasheherekea miaka mitano(5) tangu aanze shughuli ya kublog au Libeneke la kublog kama ambavyo rafiki yangu Issa Michuzi hupenda kuiita shughuli hii.Nimemuuliza pia maswali machache kuhusu siku hiyo maalum kwake na kwa wapenzi wa blog yake ambayo itafanyika pale Diamond Jubilee tarehe 30 October,2011.Twende pamoja katika mahojiano yafuatayo;
BC: Umekuwa uki-blog kwa muda gani mpaka hivi sasa?Nini kilikusukuma katika kuanzisha blog yako?
SM: Huu ni mwaka wangu wa tano sasa tangu nianze hili libeneke.Kikubwa kilichonisukuma kilikuwa ni nia yangu ya kutangaza biashara ya duka langu la nguo liitwalo 8020 Fashion lililopo Sinza.Nikaona nifungue blog ili niwe naweka nguo na bidhaa zingine kadiri zinavyowasili dukani.Sasa kama ujuavyo si kila siku naweza kuwa na new arrival na ili watu warejee kuangalia blog ndio nikaanza kuweka picha za matukio mbalimbali huku nikiwa nimejikita kwenye fashion zaidi katika kuonyesha nini kilivaliwa wapi na nani na mambo kama hayo.
BC: Kitaaluma wewe ni mwandishi wa habari. Sasa ukiwa kama blogger,unadhani kuna tofauti gani za kimsingi kati ya mwandishi wa habari wa kawaida na blogger? Je,kuna misingi ambayo wote (a journalist and a blogger) wanayotakiwa kuzingatia?
SM: Ni kweli kabisa,ipo tofauti kubwa sana. Kama ujuavyo blogger inakuwa ni mimi kama mimi ambapo nisipo-update ni blog inakuwa imelala doro. Hivyo kuwa kama blogger inabidi uwe na juhudi binafsi za kujituma kitu ambacho ni tofauti na mwandishi wa habari ambapo hata wewe usipoenda kazini au kufanya kazi gazeti ni lazima litoke tu.
BC: Blog yako imejikita zaidi katika kuandika habari za urembo,shughuli kama vile harusi,kitchen party,fashion shows nk.Ni kwanini uliamua kuwa na “niche” kama hiyo?

Dr.Harith

Leo karibia vitabu 70 vimeshaandikwa na wataalamu toka ndani na nje ya Tanzania toka 1964 kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar; mbali ya maelfu ya makala na maandishi ya taasisi za kidunia. Ila kitabu hiki kilichotoka karibuni kimechimba shimo ambalo halijawahi kufikiwa.
Mwandishi wa kitabu hiki kinachoongelewa Tanzania nzima sasa hivi na huenda kikavuka mipaka na kuingia nchi nane zinazopakana na Jamhuri ya Muungano, ni Dk Harith Ghassany. Kina kurasa 500 na kinazungumzia namna gani Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalipikwa Dar es Salaam, Algeria, mashamba ya mkonge ya Tanga na kupakuliwa Zanzibar. Kinauliza na kujibu maswali mengi yanayoathiri si tu visiwa vya Pemba na Unguja bali muungano wake na bara.
Soma mahojiano kati ya Dr.Harith Ghassany na mwandishi Freddy Macha kwa kubonyeza hapa.

Mpendwa Jakaya,
NAFAHAMU vyema kwamba unaijua vyema nchi uliyoirithi na dola uliyokabidhiwa. Hata hivyo halitakuwa jambo baya iwapo nitayakariri baadhi ya masuala makuu ambayo nadhani wewe na sisi raia zako tutakabiliana nayo katika kipindi cha miaka hii mitano ya uongozi wako.
Naamini kwamba hatuna budi kuwa na mjadala wa kudumu kuhusu masuala ya kitaifa, hata kama tayari tunayajua. Binadamu hachelewi kusahau, na hata asiposahau, hakosi kuyazoea mambo yaliyomzunguka na kuyaona kama ya kawaida na yasiyostahili tafakuri ya kina ya kila siku.
Kwanza umerithi nchi yenye “amani na utulivu”. Hii ni kweli, hasa tukizingatia kwamba tunaishi ndani ya Bara lenye misukosuko mingi na ya kila mara. Tumewashuhudia majirani zetu kadhaa wakikumbwa na milipuko isiyoisha na iliyoambatana na vita, ghasia na umwagaji mkubwa wa damu.
Hayo, Mwenyezi Mungu ametunusuru, na hatuna budi kushukuru kwa hilo, na kutafuta kila njia ya kuiendeleza hali hii tuliyo nayo, na hata kuiboresha…

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers & General Enterprises Ltd na mjasiriamali, Bw. Eric Shigongo(pichani), anatarajiwa kuhutubia nchini Marekani katika Mkutano maalum ulioandaliwa na Watanzania waishio nchini humo (Diaspora Council of Tanzanians in America – DICOTA).
Katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku nne kuanzia Julai 1, mwaka huu katika jiji la Minneapolis, Marriott Hotel, Minnesota, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Aman Abeid Karume, amealikwa kuwa mgeni rasmi. Viongozi wengine watakaohudhuria mkutano huo ni pamoja na maofisa waandamizi na wafanyabishara wakubwa kutoka Serikali ya Tanzania na Marekani.
Aidha, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Bw. Reginald Abraham Mengi, naye ni miongoni mwa wageni waalikwa wa mkutano huo ambao unafanyika kwa mara ya pili nchini humo ukiwakutanisha Watanzania waishio ughaibuni. Mada mbalimbali zitatolewa na Watanzania waishio ndani na nje ya Marekani.
Katika mkutano huo, Bw. Shigongo anatarajiwa kutoa mada itakayoelezea jinsi ya kufanikiwa kiuchumi katika mazingira ya Tanzania na anatarajiwa kuwahamasisha Watanzania waishio ughaibuni kuwekeza nyumbani Tanzania.
Katika siku za hivi karibuni, Bw. Shigongo amejipatia umaarufu kwa kutoa elimu, ushauri kwa vijana na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu nchini kupitia mikutano na hafla mbalimbali anazoandaa au kualikwa kwa lengo la kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wa kitanzania.
Kwa taarifa zaidi juu ya mkutano huo tafadhali tembelea ukurasa wa Diaspora Council of Tanzanians in America-DICOTA)

Imeandikwa na Na Angela Semaya wa Habari Leo
MAISHA yake sasa yamebadilika, amelazimika kuwa mtumwa wa kujificha kwa kuvaa vazi aina la Hijab ambalo anasema kwake limegeuka kuwa vazi analoliheshimu na kulithamini kwa kuwa ndio msiri wake mkubwa siku hizi, hii yote ni gharama inayotokana na moyo wake wa ujasiri na ushupavu uliotokana na kutumia kalamu yake kufichua uovu na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuuawa kwa imani za kishirikina.
Kwa walio wengi ndani na nje ya Tanzania, jina la Vicky Ntetema sio geni masikioni mwao kwani ni mwandishi mahiri wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Ntetema aliyezaliwa miaka 51 iliyopita ameibuka kuwa mwandishi mahiri, jasiri na shupavu baada ya kufichua siri ya kutisha kutokana na uchunguzi wa mauaji ya albino na familia zao akitaka kujua kwa undani sababu hasa za mauaji na ukatili dhidi ya albino. Hatimaye kazi yake hiyo imemuwezesha kupata Tuzo ya Ujasiri katika fani ya Uandishi wa Habari inayotolewa na International Women’s Media Foundation.
HABARI LEO Jumapili iliamua kumtafuta Vicky baada kutaka kufahamu kwa undani wa kilichomsukuma kufuatilia habari hiyo na kwa kiwango gani amefanikiwa, maisha yake kwa ujumla na kuhusiana na tuzo hiyo.
Ntetema ambaye alifanya uchunguzi wake kwa siri bila woga anasema Novemba, 2007 alipokea ujumbe wa maneno ukimuelezea kuhusu matukio ya kuuawa albino na kukatwa viungo vyao kwa imani za kishirikina, lakini awali naye hakuamini kama hicho kitu kinawezekana.
Na baada ya kufuatilia kwa muda na kujithibitishia habari hizo, alianza kuishawishi BBC, lakini walionekana kusitika wakiwa na mashaka kwamba kweli inawezekana kuwepo kwa matukio hayo? Hata hivyo anasema hakukata tamaa aliwasiliana na waandishi wengine walioko katika maeneo husika nao walimsaidia kuchunguza na kumpa taarifa zaidi.
Wakati akiendelea na uchunguzi wake aligundua kuwa waganga wa kienyeji ndio waliokuwa wakisababisha mauaji ya albino kwa kuwaambia wateja kuwa wanaweza kupata utajiri kwa kutumia viungo vya walemavu hao, ndipo alipoamua kuishawishi tena BBC huku akiendelea na uchunguzi wake kwa njia ya simu kwa kuwasiliana na watu wa Kanda ya Ziwa.
Kile alichokuwa amekusudia kukifanya na kukifichua, kilithibitishwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye Mwezi Machi, 2008 alikemea vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya albino na kuweka wazi kuwa tayari watu 19 walishauawa.
“Baada ya Rais kutangaza hivyo, nikasema kama kiongozi wa nchi amekemea kiasi hili na ametaja hadi maeneo yanayohusika na matukio hayo…kwa sababu ya kuwa na uhusiano mzuri na wahariri nilipeleka maombi yangu bila kusita wanisaidie ili niweze kwenda kabisa eneo husika ingawa waliniambia kwa kipindi hicho hawakuwa na bajeti,” anasema.
Dhamira yake ilimsukuma Ntetema kuchukua fedha zake za mshahara na kuamua kwenda Mwanza kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi wake. Anasema kazi hiyo ilimlazimu kuzunguka sehemu mbalimbali hadi akajikuta ameishiwa fedha na kulazimika kuomba kwa mama yake. 
Hivi karibuni,pale jijini London,kulifanyika kongamano la watanzania wanaoishi ughaibuni. Lilikuwa ni kongamano la pili la namna hiyo na kwa sababu hiyo liliitwa Diaspora 2.
Miongoni mwa mambo mapya katika kongamano hilo,ilikuwa ni pamoja na kualika rasmi waandishi na hususani waandishi wa mitandaoni kama vile bloggers.Almaarufu Issa Michuzi alikuwa miongoni mwa sio tu waalikwa,bali pia watoa mada(mahojiano naye kuhusu uzoefu wake kufuatia kongamano lile yapo mbioni). Mwandishi mwingine mkongwe na blogger aliyekuwepo katika mkutano huo ni Freddy Macha. Mbali ya kuwa mwandishi,blogger,Freddy pia ni mwanamuziki na muelemishaji hususani katika masuala ya afya na michezo ya kujihami au kujikinga(self-defense). Unaweza kusoma mahojiano yangu ya kina naye kwa kubonyeza hapa na hapa.
Baada ya kongamano lile,Freddy aliketi chini na kuandika kuhusu yaliyojiri kwenye kongamano na zinapoelekea zama hizi za tekinolojia ya habari na mawasiliano. Bonyeza hapa usome alichokiandika Freddy Macha. Usisahau pia kusoma makala zake katika gazeti la Mwananchi kila Jumapili.

Na Freddy Macha
Mwezi jana tulitoa sehemu ya kwanza ya mahojiano na mmoja wa wataalamu na wasomi wetu mkazi na mhadhiri anayeishi Uingereza Dk. Imani Silver Kyaruzi. Kitabu chake mkakata “Mbinu za Ujasiriamali” kitasaidia sana kuendeleza uchumi na akili za Mtanzania hasa yule anayependa kujiendeleza au kufanya biashara. Kilichapwa na “Mkuki Na Nyota” mjini Dar Es Salaam mwaka jana.
FM: Turudi katika uandishi Tanzania. Mkuki na Nyota ni wachapishaji pekee wanaowakilishwa kidogo nje, wenye tovuti na wanaojitahidi. Je kitabu kinauzwa vizuri? Ulichapisha nakala ngapi? Je, wasomaji wengi wako nje au ndani? Unayo njia ya kuyajua hayo?Unaridhishwaje na hali ya uandishi na usomaji wa vitabu nchini.
Dk. Imani Kyaruzi: Mkuki na Nyota wanao mpango wa kukiendeleza na kukisambaza kitabu hiki nchini kote. Kazi hii imeanza tayari na ninategemea mawasiliano hivi karibuni. Nakala zilizochapishwa ziko katika maelfu na ninaweza tu kuongelea wanunuzi wa bara la Ulaya. Wakati wa unzinduzi nilifanikiwa kusaini nakala nyingi sana na kitabu kilipokelewa vizuri na umati wa Watanzania waishio Uingereza. Baadhi ya nakala zilienda Ujerumani kwa wasomaji wa huko na marejesho yanaridhisha.
Nia ni kuwafikia wasomaji wa ndani na kazi hii itaanza baada ya majuma mawili. Ningependa kutoa mafunzo nyumbani wakati wa kukitangaza kitabu hiki.
Kuhusu uandishi na usomaji, inasikitisha sana kwani tumezoea kuona vitabu vya kina Michael Porter na kina Mr Smith na ninafikiri Watanzania tukianza kuandika italeta changamoto kwa waandishi walioko nyumbani ambao naamini wako wengi, tu. Kwa upande wa usomaji sina uhakika na hilo, ila tu ningependa kusisitiza kuwa vitabu vya mitaala hadi Chuo Kikuu viwakilishwe na vitabu vilivyoandikwa na wazalendo na vyenye kulenga katika hali halisi ya nchi. Hii ni muhimu kwani vitabu vyenye maudhui ya Kiulaya vinawatayarisha vijana wetu kutumikia nchi gani? 
Mwaka jana mmoja wa wataalamu na wasomi wetu mhadhiri anayeishi Uingereza Dk. Imani Silver Kyaruzi alitoa kitabu moto moto “Mbinu za Ujasiriamali” kitakachosaidia sana uchumi na akili za Mtanzania hasa yule anayependa kujiendeleza au kufanya biashara. Kitabu hiki kilichochapishwa na “Mkuki Na Nyota” mjini Dar Es Salaam ni kidogo chenye kurasa 50. Hivi karibuni alifanya mahojiano na Freddy Macha. Hii ni sehemu ya Kwanza ya mahojiano hayo.

Dr.Kyaruzi(kulia) akiwa na Katibu Wa Chama cha Watanzania nchini Uingereza,Suzan Mzee(kushoto) wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho Birmingham-October 2008.
FM :Muundo au fani yako ni kuuliza maswali na kupanga vichwa rahisi vya kuelewa kimaneno. (“Je wewe unauza nini?” ” Je unahitaji watu wa kushirikiana nao?”).
Twaweza kusema kazi yako ya kufundisha (Mhadhiri, Uingereza) imeathiri muundo wa kuandika kitabu hiki kizuri chenye lugha nyepesi kueleweka?
Dk. Imani Kyaruzi: Kweli kabisa…niliamua kutumia lugha nyepesi na yenye kueleweka baada ya kugundua kuwa watu wengi (wafanyabiashara) wanashindwa kufuatilia maelezo yaliyomo katika vitabu vya kimataifa vya ujasiriamali. Si Tanzania tu, bali hata hapa Ulaya wafanyabiashara hawana muda wa kusoma madoido ya kisomi yasiyoeleweka! Ila kwa upande mmoja haikuwa rahisi kuandika kitabu hiki kwa lugha kiswahili kwani nina muda mrefu tangu nimeondoka Tanzania na lugha imebadilika sana. Utakuta katika baadhi ya maneno nimejaribu kufikiri katika lugha zote mbili na kutafuta maneno yatakayofaa kuufikisha ujumbe bila kuupotosha. 

Maggid Mjengwa sio jina geni.Bila shaka kabisa umewahi kumsikia,kumsoma na pengine hata kutembelea blog yake ambayo kimsingi ni kimbilio la yeyote yule anayependa kupata picha halisi ya maisha ya mtanzania wa kawaida hususani yule anayeishi kijijini kama ilivyo kwa babu na bibi yangu.Wasomaji,watembeleaji na wachangiaji wa blog yake wanapenda kumuita “Mwenyekiti”.
Yeye ni miongoni mwa waandishi wa makala zenye kuchoma kama sio kugusa hisia za wengi.Ukitaka kujua historia yake ya uandishi unaweza kuipata kwa kusoma mahojiano tuliyowahi kufanya naye siku za nyuma kwa kubonyeza hapa.
Maggid ni mpenzi wa michezo hususani wa soka.Ni mnazi wa Simba.Ni upenzi huo wa soka na michezo kwa ujumla ambao ulimfanya aanzishe gazeti lililoitwa “Gozi Spoti” ambalo lilidumu mitaani mpaka hivi karibuni alipoamua kulisitisha.
Jambo jema ni kwamba, kuondoka kwa “Gozi Spoti” kulifanyika kwa makusudi ili kulipisha gazeti jipya litakalojulikana kama Kwanza Jamii ambalo litaingia mitaani siku si nyingi chini ya usimamizi wa Ikolo Investment Ltd kampuni iliyo chini ya mwenyewe “Mwenyekiti”.Kwa hiyo tunaweza kabisa kuongeza cheo kimoja kwa “Mwenyekiti” na kumuita Mjasiriamali.
Kwanza Jamii ni jarida la uchambuzi wa masuala yanayohusu na kuigusa jamii.Haya ni pamoja na siasa,uchumi,elimu,michezo na utamaduni.Pia yatakuwemo masuala ya mazingira,jinsia na ukimwi . Ni jarida litakalokuwa linatoka kila siku ya Jumanne.
Tumepata nafasi ya kufanya mahojiano mafupi na ‘Mwenyekiti” kuhusiana na ujio wa jarida hili na pia kumdadisi kuhusu anachokiona kila atembeleapo vijiji na vijiji vya Tanzania.Anaona nini?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; 

Hivi majuzi,Mzee wetu, Rashid Mfaume Kawawa, alizindua kitabu kinachoelezea maisha yake.Kitabu hicho ambacho kimeandikwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Chuo Cha Mwalimu Nyerere Cha Kivukoni,Prof.John Magoti,kimepewa jina la Kawawa.Uzinduzi huo ulifanyikia Ikulu jijini Dar-es-salaam.
Ingawa tunaweza kusema imemchukua muda mrefu sana Mzee Kawawa kuandika kitabu chake,ni lazima tumpongeze sana kwa uamuzi wake huo ambao sio tu wa busara bali pia ni mfano wa kuigwa.
Tulipofanya mahojiano na Mheshimiwa Zitto Kabwe mwaka juzi,tuliliongelea suala la kuandika vitabu na kujisomea.Mh.Kabwe alionekana kukerwa na tabia ya viongozi wetu(na hata sisi wananchi wa kawaida) kutopenda kusoma achilia mbali kuandika! Ni utamaduni ambao tupende tusipende hatuna budi kuiga.
Uandishi ukisindikizwa na usomaji ni msingi mzuri wa maendeleo.Wenzetu katika nchi zilizoendelea ni mabingwa wa kujisomea.Miji ya wenzetu imezungukwa na maktaba. Ukiingia kwenye ndege,treni au basi sio ajabu kukuta watu kadhaa wakijisomea vitabu,magazeti nk.Kwanini wanapenda kusoma?Jibu ni rahisi;wanapenda kuongeza ujuzi,kujielimisha na hivyo kuendelea kuwa mbele katika suala zima la maendeleo.
Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria uzinduzi wa kitabu cha Kawawa ni pamoja na maraisi wastaafu Ally Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa. Swali ambalo lilibakia kichwani kwangu ni kwamba viko wapi vitabu vyao? Ni lini tutasoma kitabu cha Mwinyi,Mkapa,Warioba au hata Edward Lowassa na wengineo?
Ni matumaini yetu kwamba Kawawa amefungua tu njia na kwamba wengine watafuata.Hongera sana Mzee Kawawa.
Pichani ni Mzee Kawawa na Rais Kikwete wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.Kwa nyuma unaweza kumuona Rais Mstaafu B.W.Mkapa.Picha kwa hisani ya Ikulu.


sending...