Ijumaa imewadia.Kama kawaida hii ni siku ambayo watu wengi,hususani wanaofanya kazi ya Jumatatu hadi Ijumaa,huwa wanaisubiri kwa hamu. Hapo sijasema kwamba wikiendi hii ni “Mwisho wa Mwezi”.Kila mtu anazo.Bahati nzuri ni kwamba bado tupo katika Mwezi wa Toba kwa hiyo vibweka huko mitaani navyo huwa vinapungua. La sivyo,ungesikia vibweka kutoka katika baa ya kona.Sikia vicheko.Sikia jinsi baa medi anavyokaripiwa akichelewa kuweka bia mezani.Jeuri ipo.Pesa huwa inaongea.
Nasi hapa BC,tupo kwa ajili ya kuendeleza jadi.Ijumaa ni siku ya kujifaragua kidogo.Zamani walikuwa wanasema siku ya “kuruka majoka”.Ni wakati wa Zilipendwa. Leo tungependa kukuhamisha kidogo msomaji na mpenzi wa safu hii ya kila Ijumaa.Hatukupeleki mbali sana.Ni hapo DRC.Zamani iliitwa Zaire.Ilikuwa maarufu sana ulimwenguni hususani baada ya ule mpambano wa ndondi za uzito wa juu baina ya Mohamed Ali na George Foreman mwaka 1974. Enzi za Mobutu Seseseko Nkuku wa Zabanga.
Wimbo unaitwa Mamou(Tu Vois?) kutoka kwa gwiji la magwiji katika Afro-Rumba.Si mwingine bali mzee mzima Francois Luambo Makiadi maarufu kama Franco.Wimbo huu ni hadithi tamu sana.Hadithi ya mapenzi,uongo katika mapenzi,maisha nk. Zamani nakumbuka tulikuwa tukitaniana kwamba wimbo huu na mwingine hivi wa Madilu System,ulikuwa ukiuanza basi unasafiri kutoka Dar-es-salaam mpaka Morogoro na bado unaburudika tu.
Naamini wimbo huu unaweza kukukumbusha mbali.Usiwe mchoyo basi wa kuwaambia wenzako kupitia sehemu ya maoni kwamba Mamou inakukumbusha wapi.Ulikuwa unasakata Rhumba sehemu gani? Nakutakia wikiendi njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Ukitaka kusoma tafsiri ya Kiingereza ya wimbo huu bonyeza hapa.

Kama wewe mwenyewe haijawahi kukutokea,basi huenda unamjua mtu au watu ambao ishawahi kuwatokea.Kama ndivyo,basi usisite kumpelekea mwenzako link ya burudani yetu ya leo.
Mtu kampenda mwenzake.Wenyewe wamependana.Kwa bahati mbaya,watu kibao(mara nyingi marafiki na familia) wanasema haiwezekani ukampenda yule bwana au yule bibie.Hafai kabisa.Ana kila aina ya sifa mbaya hapa mjini.Achana naye!
Penzi linakuwa limeingiliwa.Vitisho vya kila aina vinaingizwa.Ukimuoa au ukiolewa na yule jamaa,urafiki mimi na wewe basi.Tutapingua undugu aisee.Sokomoko ndani ya penzi.Hali kama hiyo ikikutokea unafanyaje?Unatia pamba masikioni na kuacha waseme kwa matumaini kwamba usiku ukifika watalala au?
Maudhui hayo ndiyo yaliyopo kwenye burudani ya leo,ya weekend hii ya “Zilipendwa”.Ni ujumbe kutoka kwa Mbaraka Mwinshehe & the Morogoro Jazz Band.Wimbo unaitwa Wacheni Waseme kutoka katika album ya Masimango.Siku za nyuma tuliwahi kuandika kwa kirefu kuhusu historia ya Mbaraka Mwinshehe ambaye bila shaka sote tunakubaliana kwamba he is among the best talented musicians Tanzania have ever had.
Kila mara ninaposikiliza nyimbo za Mbaraka Mwinshehe huwa nakumbuka mji wa Morogoro.Napata picha ya ule udongo mwekundu.Nakatiza pembeni ya Uwanja wa Jamhuri.Taratibu napita karibu na Bwalo la Umwema.Naona upande wa nyuma wa hospitali ya mkoa Morogoro.Vijana waliovalia suruali na sketi za kijani wanakatisha.Enzi hizo rangi hizo zilikuwa na maana kweli.Ukivaa kijani maanake ni kwamba uli-faulu mitihani yako ya darasa la saba.Ninavyozidi kuelekea juu,naiona Morogoro Hotel.Oh Morogoro.
Burudika msomaji.Weekend Njema
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Je,kuna siri ya watu wawili?Yawezekana.Haiwezekani.Ukishamwambia mtu mmoja sio siri tena!Kweli?
Ushawahi kuambiwa na mtu “hii ni siri,usimwambie mtu” au kwa kizungu “this is between you and me,don’t tell anyone”.Basi ni kwanini hakuna siri ya watu wawili?Ina maana katika watu wawili mmoja hawezi kukaa na kitu moyoni,asimwambie mtu?Ndivyo binadamu tulivyo?
Ninapoandika hapa,najaribu kuwaza kuhusu mambo mbalimbali ambayo niliwahi kuyafanya nikitegemea kwamba yangekuwa siri lakini yakageuka kuwa sio siri baada ya kuthubutu kumwambia mtu mmoja mwingine! Kwanini mtu yule au watu wale hawakuchukulia maanani maneno kama “hii naomba iwe siri baina yangu na wewe pekee,asijue mtu tafadhali”.Hivi ni kweli haiwezekani kutunza siri?
Maudhui hayo ndio yaliyopo kwenye Zilipendwa ya Ijumaa hii.Wimbo unaitwa Siri Yako kutoka kwao Bima Lee Orchestra. Burudika.Ijumaa Njema.Weekend Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Unakumbuka Kisa Cha Mesenja Kuleta Balaa kutoka kwao hawa hawa Bima Lee?

Mambo vipi,shikamoo,marahaba,habari gani msomaji?Natumaini hujambo.Sisi hapa BC wote wazima kabisa.
Ijumaa ndiyo hiyo imewadia tena.Siku zinakwenda kama kimbunga cha nyikani.Lakini Ijumaa humaanisha burudani kupitia hapa BC.Ni wakti wa Zilipendwa.
Huu ni wakati wa kuenzi enzi ambazo,kama tungeendelea nazo,bila shaka leo hii nasi tungekuwa tuna midundo,sauti nk ambazo zikipigwa tu,kila mtu angejua huo ni mziki kutoka Tanzania. Si unajua leo hii ukisikia mdundo fulani tu unajua huo ni kutoka Afrika Kusini?Au ukisikia mdundo fulani unajua huo ni kutoka Ghana au Nigeria au Somalia?
Kuna watu ambao ni wagumu sana kuomba msamaha hata pale wanapokuwa wamekosea.Neno Samahani kwao ni kama jela.Akilitoa anahisi amepungukiwa akili hivi.Kuna ubaya gani kuomba msamaha unapokosea?Binadamu hatujakamilika.Tunakosea.Ni jukumu letu kuomba msamaha tunapokosea.
Maudhui hayo ndiyo yaliyopo katika wimbo wetu wa leo.Unaitwa Fikiri kutoka kwao DDC Mlimani Park Orchestra maarufu Sikinde.Pata Burudani.Weekend Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.


Pichani juu ni Dr.Remmy Ongala.Tuliwahi kuandika kwa kirefu historia yake.Unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa. Katika miaka ya nyuma,yeye na Orchestre Super Matimila,ndio walikuwa kitambulisho kizuri cha muziki kutoka Tanzania katika nchi za Ulaya na hata Marekani ya Kaskazini.Alipendwa sana wakati alipokuwa akihudhuria matamasha ya WOMAD.
Mpaka leo hii,watu wengi wa ughaibuni ambao hawatoki Tanzania,hupenda kumuulizia na kutaka kujua yuko wapi na anafanya shughuli gani na kama bado anajishughulisha na muziki.Jibu la maswali hayo linaeleweka;Remmy Ongala siku hizi ni mlokole.Kama bado anajishughulisha na muziki,basi ni ule wa kiroho.Ule wa kumsifu na kumtukuza Muumba.
Remmy Ongala na Orchestre Super Matimila,ndio wanaotupa burudani ya wikiendi hii.Wimbo unaitwa Kipenda Roho.Anasema Kipenda Roho hula nyama mbichi.Kipenda Rohooo…msikilize na furahia mwisho wa wiki.Asante.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Prof.Jay,The Heavy Weight MC

Kama ipo wiki ambayo nilitamani sana ifikie ukingoni,hii bila shaka ni mojawapo.Kwa kiasi fulani nilikuwa nimeshachoka na “watangaza nia”.Naona kila mtu anaitumia ipasavyo haki yake ya msingi.Watetezi wanasema huo ndio ukuaji wa demokrasia.
Wasiwasi wangu ni kwamba kwa namna fulani,imeshageuka kuwa fasheni.Si unajua tunavyopenda kuigana?Mmoja akianza kitu basi wengine ni lazima wafuate.Unataka kuniambia umesahau biashara ya salon ilipoanza? Au daladala za watu binafsi ziliporuhusiwa?
Kwa “waliotangaza nia” na kuchukua fomu, naomba uwasikilize kwa makini.Sentensi na misemo inakuwa ni ile ile.Ahadi zinakuwa zinafanana.Huyu akiahidi kwamba ataanzisha kituo cha televisheni mahali ambapo hata umeme haujafika,mwingine bila hata kufikiria naye anasema hivyo hivyo.Mwananchi wa kawaida,kichwa kinapata kizunguzungu.Amwamini nani?Mbona wote wanaongea sawa na ahadi zao zinafanana? Labda nikamsikilize kasisi kanisani au sheikh msikitini? Mmh huko nako kuna mengi.Kama jiwe la msingi liliwekwa na fulani,kuna jipya?
Kwa hiyo nikawa natamani wikiendi iwadie kwani sijasikia sana kuhusu wanaotangaza nia katika siku za wikiendi.At least sio hadharani.Labda kule kwenye moja moto,moja baridi.Kichwa kikianza kuwa kizito,lugha inabadilika na sera za kweli zinaanza kutolewa.Ngoja wanichague,I can’t wait kuwa na “shangingi” langu na dereva.Mimi na safari,safari na mimi.Pembeni toto ya kona.Mheshimiwa Mbunge(MP).
Enewei,maisha yanasonga.Burudani ni jadi yetu hapa.Wimbo wa leo unaitwa Namsaka Mbaya Wangu
kutoka kwao Dar-es-salaam Int’lJazz Band chini ya Jabali la Muziki,Hayati Marijani Rajabu.
Burudika na wimbo Namsaka Mbaya Wangu.Wikiendi Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Picha kwa msaada wa Werner Graebner
Sijui wewe mwenzangu,ila mimi nahisi siku zinakwenda kwa kasi ya ajabu.Wiki inavyokatika huwa nashindwa kujua hata imeishaje! Nikizingatia kwamba tayari tupo katika ngwe ya pili ya mwaka 2010,napata wasiwasi kidogo.Je ntatimiza malengo yangu niliyojiwekea siku ile ya mwaka mpya wakati ving’ora vikilia kutoka bandarini,taa zikiwaka na kuzimika?
Pamoja na kupatwa na wasiwasi ninapoangalia mzunguko wa saa,huwa napata faraja kujua kwamba wiki ndio inakatika na kwa maana hiyo,weekend imewadia.Ni muda wa kupumzisha akili kidogo.Ni muda wa kuburudika na “Zilipendwa” kama ilivyo jadi yetu hapa BC. Najua pengine bado unawajibika wakati wa weekend.Sawa.Lakini kuna pumziko fulani.Barabarani magari yanakuwa yamepungua.Mitaani kunakuwa kweupe kidogo.
Kwa upande mwingine,fainali za Kombe la Dunia la FIFA ndio zishamalizika.Pweza Paulo kajipatia umaarufu wa kutosha.How could he be right all the time? Naambiwa sio Paulo Pweza peke yake aliyekuwa sahihi katika utabiri.Nasikia hata Spika wa Bunge letu,Mheshimiwa Sitta alitabiri kwamba Spain “itafanya vizuri sana”. Lakini kali ni kutoka kwa Nabii Joshua(kama hujawahi kumsikia nisamehe).Yeye alitabiri vyema kabisa mechi ya ufunguzi katika ya South Africa na Mexico. Alisema Mungu kamwambia South Africa watafunga goli kwanza ila wasipolilinda litarudishwa!.Upo hapo? Mambo ya common sense hayo.
Enewei,fainali zimeisha vyema.Afrika Kusini wametutoa kimasomaso maana jamaa wa magharibi walikuwa wamechachamaa kweli wakisema Afrika hakuna nchi inayoweza kuandaa mashindano makubwa kama yale. Kumbe hawakujua kwamba waafrika,pamoja na mambo yetu yote,tunasikilizana.Wale “chinjachinja” wakaambiwa tulizeni mzuka wakati wa fainali na kweli jamaa wakatulia kimyaa.Ngoma ipo kwa Brazil sasa.Jamaa wanaanda fainali za mwaka 2014.Kule napo nasikia fujo kama kawaida.Kuna Favela.
Turudi kwenye burudani sasa.Leo tunao Jamhuri Jazz Band.Wimbo unaitwa Wasiwasi Ondoa. Jamhuri Jazz Band ilianzishwa katika miaka ya 50s kule mkoani Tanga.Wakati huo kulikuwa hakuna Tanzania bali Tanganyika.Mwanzoni bendi hiyo iliitwa Young Nyamwezi Band.Mabadiliko yalifuata baada ya kupata ufadhili wa bwana mmoja aliyeitwa Joseph Bagabuje.Baadaye Bagabuje alikuja kuwa mtanganyika wa kwanza kuwa Meneja wa Amani Tea Estate.
Miongoni mwa wanamuziki ambao baadaye walijiunga na bendi hiyo na kuisaidia kukua zaidi ni pamoja na wana-ndugu Wilson Kinyonga na George Kinyonga. Walijiunga na Jamhuri Jazz Band mwaka 1966 kabla hawajimega mwaka 1970 na kwenda kuunda Arusha Jazz Band na baadaye Simba Wanyika.
Usikilize Wasiwasi Ondoa kwa kubonyeza player hapo chini.Weekend Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Mwisho wa wiki unapowadia,sio kila mtu huwa na furaha. Raha au karaha hutegemea sana na mipango yako ya wikiendi,yanayojiri katika jamii yako,hali ya mfuko wako,ulipo nk.Pia lipo suala zima la “upweke” au loneliness kama wanavyosema wenzetu wa magharibi.
Upweke unaweza kuufananisha na maradhi wakati mwingine. Upweke unaotokana na kuwa mbali na “better half” wako ndio unaweza kuwa maradhi kabisa. Hapa nazungumzia ile hali ya kuketi nyumbani kwako unasubiri kilicho chako.Kila baada ya dakika kadhaa unakwenda kuchungulia dirishani.Ni yeye kawasili? Kama unajua anakuja kwa gari basi kila usikiapo mngurumo wa gari,damu inakusisimka,macho yanakutoka na shauku kibao moyoni. Simu ikiita unatoka mbio kuikimbilia.Sijui ni yeye au…?
Kwa upande mwingine,unapokuwa unajua kabisa kwamba mpenzi wako yuko mbali na hakuna uwezekano wa kuonana naye leo au kesho,simanzi huwa kubwa zaidi.Pamoja na hayo,bado waweza kuwa na shauku.Waweza kutizama dirishani ukitamani kumtuma njiwa akupelekee salamu. Bahati mbaya ni kwamba njiwa haonekani.Kinachoonekana nje ni mvua tu.Na kama ujuavyo binadamu,mvua ikianza kila mtu hutafuta pa kujibanza!
Hali ninayoizungumzia hapo juu ndio maudhui ya “Zilipendwa” yetu ya leo. Wimbo unaitwa Dirishani kutoka kwa Hayati Patrick Balisidya na Afro 70 Band. Bila shaka msomaji utakubaliana na mimi kwamba ni vigumu kuzungumzia muziki wa Tanzania bila kugusia mchango wa Hayati Patrick Balisidya na kundi zima la Afro 70. Hawa jamaa walitamba sana miaka ya 70. Ni bendi iliyokuwa chini ya uongozi mahiri wa Patrick Balisidya ambaye wengi waliopata kumfahamu au kufanya naye kazi wanasema; He was the most humble man they have ever met and truly down-to-earth gentleman!
Patrick Balisidya alizaliwa tarehe 18 Aprili mwaka 1946 huko Mvumi mkoani Dodoma.Baada ya kumaliza shule alifanya kazi ya ufundi kwa muda mfupi kabla ya kuanza rasmi shughuli za muziki mnamo mwaka 1967 akiwa kama mpiga gitaa wa bendi ya Dar-es-salaam Jazz Band.
Kufikia mwaka 1970, Patrick Balisidya alikuwa ashaanzisha bendi yake iliyojulikana kama Afro 70,bendi ambayo ilitokea kuwa moto wa kuotea mbali. Afro 70 walitamba sana na mtindo wao uliojulikana kama “Afrosa”. Mtindo huu ulitumia zaidi vionjo na ala kutoka mkoani Dodoma hususani kabila la wagogo. Mpaka hivi leo baadhi ya vibao vyake kama vile “Harusi” ni vya kuotea na ni moja ya nyimbo zinazopendwa sana hususani wakati wa sherehe za harusi.Nyimbo nyingine zilizowahi kutamba ni kama vile Wikiendi na Tausi bila kusahau “anthem” ya Harusi.
Patrick Balisidya alifariki dunia tarehe 7 August mwaka 2004 huko Kibaha mkoani Pwani.Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Burudika na kibao Dirishani hapo chini.Wikiendi Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Pichani ni Afro 70 Band. Picha hii ni kwa hisani kubwa ya Brother John Kitime. Thank you John for bringing back to life all the great memories of Tanzanian Music scene especially the kind of music that we now call “Zilipendwa”.Can’t we call them “Tunazipenda”?

