Bila shaka uliona sherehe za ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA yanayoendelea nchini Afrika Kusini.Kama jibu ni ndio,bila shaka unakumbuka wimbo alioimba R.Kelly akishirikiana na Soweto Gospel Choir.Hii hapa ni Official video ya wimbo huo;Burudika

You need to a flashplayer enabled browser to view this YouTube video

Pamoja na kupata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Ufaransa(Mabingwa wa Dunia mwaka 1998), timu ya taifa ya Afrika Kusini,maarufu kama Bafana Bafana,imeyaaga mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA yanayoendelea nchini mwao.

Kwa maana hiyo,Afrika Kusini imeweka pia historia ya kuwa timu ya kwanza katika historia ya miaka 80 ya  mashindano ya Kombe la Dunia kutolewa katika raundi ya kwanza ikiwa mwenyeji.

Kutoka kundi A timu zinazosonga mbele ni Mexico na Uruguay(zote kutoka Amerika ya Kusini). Swali kubwa wanalojiuliza mashabiki wa soka ulimwenguni ni Je; huo ndio mwisho wa Vuvuzela?

Dalili kwamba mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia yanayoendelea huko Afrika Kusini yanaweza kuwa machungu kupita yote kwa bara la Afrika yanaweza kuwa yameanza rasmi kuonekana hivi leo baada ya timu ya Taifa ya Cameroon,maarufu kama Indomitable Lions(Simba wasiofugika) kuwa timu ya kwanza kutolewa katika mashindano hayo.

Cameroon,timu ambayo ilikuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikitajwa kama “tumaini la Afrika”,imeyaaga mashindano hayo baada ya kufungwa jumla ya magoli 2-1 na Denmark.

Kwa maana hiyo kutoka kundi E,Uholanzi imejihakikishia kuendelea na mashindano(Best 16) huku Japan ikisubiri kuumana na Denmark katika mchezo ambao utaamua nani aendelee na nani atoke.Kutoka katika kila kundi timu mbili tu ndizo zinazoendelea.

Ninapoandika post hii,Afrika Kusini wapo uwanjani wakimenyana na Mexico.Wanaongoza goli 1-0.

Kwa bahati mbaya,Mzee Madiba ameshindwa kuhudhuria ufunguzi wa fainali hizo kutokana na kifo cha kitukuu wake,Zenani Mandela,kilichotokea jana usiku kwa ajali ya gari.

(AP Photo/Nelson Mandela Foundation, Debbie Yazbek)

Pichani juu ni Mandela na wajukuu zake.Kutoka kushoto ni Thembela Mandela,Zenani Mandela(aliyefariki) na Mbuso Mandela.

Unaweze kutizama video kidogo ya Mandela na kitukuu wake aliyefariki kwa kubonyeza hapa.

UPDATE: Mchezo kati ya South Africa na Mexico umekwisha.Matokeo ni 1-1. Goli la South Africa lilifungwa na Siphiwe Tshabalala kunako dakika ya 55.Mexico walisawazisha kunako dakika ya kwa goli rahisi lililofungwa na Rafael Marquez kunako dakika 79.

Baada ya miaka,miezi,wiki na siku hatimaye yamebaki masaa machache tu kabla filimbi ya kwanza kupulizwa kuashiria kuanza kwa kivumbi cha kuwania ubingwa wa dunia wa soka.Ni wakati wa World Cup 2010.Kwa mara ya kwanza kabisa kindumbwendubwe hicho kipo barani mwetu,Afrika.

Wataalamu na watabiri mbalimbali wa soka wameshaanza kazi zao.Wacheza kamari nao hawapo nyuma.Kuna kulia na kucheka.Mfalme wa soka ulimwenguni,Pele,ametoa utabiri wake.Anasema anaziona Brazil na Spain zikiumana katika fainali.Lakini anasema pia angependa sana kuona timu ya Afrika ikifika fainali.

Mchezo wa fungua dimba hapo baadaye ni kati ya wenyeji Afrika Kusini na Mexico(South Africa Vs Mexico).Historia inaonyesha kwamba hakuna timu wenyeji iliyowahi kupoteza au kufungwa katika mchezo wa fungua dimba.Je South Africa wataendeleza historia hiyo?

Mchezo wa kesho unafanyikia katika uwanja ujulikanao kama Soccer City(pichani) uliopo jijini Johannesburg.Ulianza kujengwa mwaka 1986 na kufunguliwa rasmi mwaka 1987 na una uwezo wa kuchukua watu 94,000 ukitoa watu wa habari na VIP.Uwanja huo upo maeneo ya Soweto(chanzo cha jina ni South West Town.Ni uwanja wenye historia kemkem.Hapo ndipo utakapofanyika pia mchezo wa fainali tarehe 11 Julai.

Wakati homa ya Kombe la Dunia ikiwa ndio inazidi kupaa,ulimwengu unasubiri kwa hamu kitu kimoja.Je,Rais mstaafu wa nchi hiyo,Nelson Mandela “Madiba”,ataweza kuhudhuria japo mchezo huu wa ufunguzi?Mimi binafsi ningefurahi sana kumuona Mzee huyo akihudhuria japo mchezo huo wa ufunguzi kwani mchango wake katika kuzileta fainali hizo barani Afrika ni mkubwa sana.Bila shaka utakumbuka kwamba,alipotoka jela mwaka 1990,hapo hapo katika uwanja wa Soccer City ndipo alipowahutubia watu wake kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27.

Baadhi ya wageni wengine maarufu na viongozi  wanaotarajiwa kuhudhuria ufunguzi wa fainali hizo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban-Ki-Moon, Rais wa Mexico,Felipe Calderon,Makamu wa Rais wa Marekani,Joe Biden, na Mwenyeji wao,Jacob Zuma.Lakini waliotia fora zaidi ni majirani zetu Kenya ambao watawakilishwa na viongozi wao wote wa juu kabisa  Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga(sijui nchi wamemuachia nani).

Kivutio kingine kinatarajiwa kuwa mwimbaji maarufu wa muziki wa R&B kutoka nchini Marekani,R.Kelly,ambaye anatarajiwa kuimba wimbo wake wa “Sign of Victory” ambao ni anthem maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa  Kombe la Dunia.Ataimba kwa kushirikiana na Soweto Spiritual Singers. Wasanii wengine wanaotarajiwa kushiriki ufunguzi huo ni pamoja na Hugh Masekela, Femi Kuti na bendi ya Osibisa kutoka nchini Ghana.

Mpira utakaotumika ni Jabulani.Ingawa umelalamikiwa na makipa kadhaa(akiwemo Muharami Mohammed wa Taifa Stars) kwamba haufai na unawapa shida,FIFA wamesisitiza kwamba ndio utakaotumika.Jabulani ni neno la kiZulu linalomaanisha “kuleta furaha kwa kila mtu”.

Jabulani

Ratiba kamili ya Fainali hizi unaweza kuipata kupitia mtandao wa FIFA kwa kubonyeza hapa.Pia jamaa wa SoccerNet.com wana ratiba nzuri zikiwa na masaa ya hapo ulipo(local time).Kama hukufanikiwa kuliona tamasha la ufunguzi (2010 FIFA Official World Cup Kick Off Concert) bonyeza hapa.Jamaa wa Vevo bado wanalionyesha kwa kulirudia kila mara.It is Time For Africa.Viva Africa!!

Baada ya mchezo wa fungua dimba, Ufaransa(mabingwa wa dunia mwaka 1998) watakipiga na Uruguay.

Huyu jamaa anaitwa “Zakumi”. Alizaliwa tarehe 16 Juni mwaka 1994.Ndiye Official Mascot wa Kombe la Dunia mwaka huu.Lakini Mascot ni nini?Bonyeza hapa kujua zaidi.

Kiungo mchezeshaji wa Timu ya Taifa ya Soka ya Ghana na klabu ya Chelsea ya Uingereza,Michael Essien(pichani), atazikosa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Kwa mujibu wa tovuti ya Chama cha Soka cha Ghana(GFA),kiungo huyo ambaye kwa muda sasa amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya goti,hatoweza kupona mpaka hapo mwishoni mwa mwezi wa saba(Julai) na hivyo kumaliza kabisa matumaini ya kuweza kucheza katika fainali hizo.

Uamuzi wa mwisho wa kumuondoa Essien katika kikosi cha Ghana(Black Stars) ulifikiwa na chama hicho cha soka kwa kushauriana kwa karibu na timu yake ya Chelsea pamoja na daktari wake na pia madaktari wa Timu ya Taifa ya Ghana.

Pamoja na kwamba hatocheza,habari zinazidi kupasha kwamba Michael Essien ataambatana na timu hiyo kwenda Afrika Kusini na kwamba atasaidia katika masuala mengine ya kiufundi.Ghana wapo kundi D pamoja na Ujerumani, Australia na Serbia. Wataingia uwanjani kwa mara ya kwanza tarehe 13 Juni kupambana na Serbia.

Hii ingekuwa mara ya pili kwa kiungo huyo kucheza katika fainali za Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo miaka minne iliyopita katika fainali zilizofanyikia nchini Ujerumani. Je,Ghana wataweza kufanya vizuri bila kiungo wao mahiri Michael Essien?

Zimebaki takribani siku 15 kabla kipute cha kugombea Kombe la Dunia la Soka hakijaanza huko nchini Afrika Kusini au “bondeni” kama ambavyo wengine wanapaita.

Jumla ya timu 32 zinashiriki fainali za kombe la dunia la mwaka huu ambazo kwa mara ya kwanza kabisa,zinafanyikia barani Afrika. Wawakilishi wa bara la Afrika katika fainali za mwaka huu ni wenyeji Afrika Kusini, Nigeria, Ghana,Ivory Coast, Cameroon na Algeria.

Licha ya hii kuwa mara ya kwanza kwa nchi yeyote ya bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, hakuna timu ya Afrika iliyowahi kuchukua ubingwa au hata kufikia nusu fainali.Mafanikio ambayo bara la Afrika linajivunia nayo mpaka hivi leo ni kufikia hatua ya robo fainali ambapo Senegal(ilifika hatua ya robo-fainali mwaka 2002 kabla ya kutolewa na Uturuki kwa goli kwa 1-0) na Cameroon(mwaka 1990 ilifikia hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa na Uingereza kwa jumla ya goli 3-2)

Wachambuzi mbalimbali wa soka hawaipi Afrika nafasi ya kufanya vyema japokuwa ni wenyeji kwa sababu mbalimbali kama vile kuwa katika makundi magumu;mfano hapa unatolewa kwa kundi G ambalo ndani yake kuna Ivory Coast,Brazil,Portugal na Korea Kaskazini. Wengi hawaipi Ivory Coast nafasi ya kuendelea raundi ya pili na kwa maana hiyo kuziacha ama timu za Brazil na Portugal ambazo zinapewa zaidi nafasi ya kusonga mbele.

Sababu zingine zinazotolewa ni ukosefu wa uzoefu(Ghana  na Ivory Coast zinashiriki kwa mara ya pili wakati Algeria inashiriki kwa mara ya tatu baada ya kutofanya hivyo kwa muda mrefu)

Pamoja na hayo, kwa upande mwingine wale wanaozipa nafasi timu kutoka barani Africa wanajitia moyo wa ushindi kwa sababu ukweli ni kwamba bara la Afrika  lina wachezaji lukuki katika ligi za Ulaya jambo ambalo linatuhahakishia kwamba timu za Afrika zilizofuzu zinao wachezaji wengi tu wenye  ufundi na uzoefu(skills and experience) na mikikimikiki ya mashindano makubwa kama ya Kombe la Dunia.

Je, Africa tutacheka au tutaendelea kulia na kununa? Miongoni mwa timu hizi ambazo picha zake zipo hapo chini ni ipi ambayo unaishabikia? Ni ipi ambayo unaipa nafasi ya juu kufanya vyema zaidi kuliko zingine? Kwanini unaipa nafasi hiyo?

South Africa

Cameroon

Algeria

Ivory Coast

Ghana

Nigeria

Editor’s Note: World Cup 2010 ni tukio kubwa na la kipekee ambalo bila shaka litafuatiliwa na mabilioni ya watu ukiwemo wewe msomaji na mtembeleaji,msomaji na mchangiaji wetu.Kwa kutambua hilo,BC itakuwa,kwa msaada na ushirikiano wa wapenzi,wataalamu na wafuatiliaji wa soka,itakuwa ikikuletea chambuzi mbalimbali kuhusu fainali hizi.Asanteni

Pamoja na ushabiki wote wa soka nchini ambao siku hizi umejikita sio tu katika timu za Yanga na Simba bali pia timu mbalimbali zinazoshiriki ligi kuu ya nchini Uingereza(English Premier League), bado wengi tunakubaliana kwamba hakuna tukio la soka ulimwenguni linaloshinda mashindano ya kugombea Kombe la Dunia la Soka( Soccer World Cup).

Ubishi na ushindani wa Arsenal, Chelsea, Manchester United, Liverpool, Newcastle nk unapofikia ukingoni,macho na masikio huelekezwa katika Kombe la Dunia. Pale ndipo penye msisimko wa aina yake.Vipaji visivyo vya kawaida huonekana pale. Ndoto hutimizwa pale na pia ndoto huyeyuka au kuota mbawa na kupaa kama vile afanyavyo mwewe baada ya kukidakua kifaranga.

Kama unavyojua,mwaka huu kipute kipo barani kwetu. Hii ni mara ya kwanza kwa bara la Afrika kupewa nafasi ya kuandaa kombe la dunia. Ni mwaka ambao una matumaini mapya kwani ukitazama kwa makini,bara la Afrika lina wasakata kabumbu mahiri sana wanaocheza katika vilabu mbalimbali ulimwenguni hususani barani Ulaya.Mimi sina timu huko Ulaya;ila Real Madrid na Arsenal wakifungwa huwa sijisikii raha! Utaniita mshabiki?

Sasa kama ilivyo kwa matukio mengi makubwa ya michezo duniani,muziki huwa haukosi.Kunakuwa na wimbo maalumu kwa ajili ya mashindano(tournament’s official song). Kombe la dunia pia.Kwa mwaka huu, wimbo Waving Flags (kwa Kiswahili rahisi naweza kusema Kupeperusha Bendera) kutoka kwa mwanamuziki Knaan .Huu ndio World Cup 2010 Official Song.

Knaan ni mzaliwa wa Somalia. Kwa sasa makazi yake ni Toronto,Canada. Ni miongoni mwa wanamuziki wenye asili ya Afrika wanaofanya vizuri sana katika anga za muziki ulimwenguni. Bonyeza hapa ili kutembelea tovuti yake na pia hapa ili kusoma zaidi kuhusu historia yake.

Haya sasa,wimbo huo.Tupeperushe bendera.Je Afrika tutatoka kimasomaso huko Kusini mwa bara letu? Imebaki miezi michache.Usikilize wimbo Waving Flags hapo chini

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Picha na habari kwa hisani ya GetMziki.Watembelee kusikia pia Remix ya wimbo huu.

↑ Go Back to Top of Page